By Dorlingson Edward Edwin
Je, umewahi kujiuliza nini hutokea pale jamii inayotegemea mifugo inapokosa malisho, jamii inayotegemea misitu inapokosa mimea ya asili, au jamii inayotegemea kilimo inaposhindwa kutambua msimu sahihi wa kupanda?
Kwa jamii nyingi za asili, mabadiliko haya si suala la kubadilika kwa hali ya hewa pekee. Ni mabadiliko yanayoweza kubadili namna wanavyozalisha chakula, kujipatia kipato, kuishi, kuhifadhi utamaduni na kurithisha maarifa kutoka kizazi kimoja hadi kingine.
Jamii nyingi za asili zinategemea moja kwa moja rasilimali za mazingira kama ardhi, misitu, maji na wanyamapori kwa ajili ya maisha yao.
Kwa mfano, wafugaji wanapokabiliwa na ukame wa muda mrefu, upatikanaji wa maji na malisho kwa mifugo hupungua. Hali hii inaweza kuwalazimu kuhama kutafuta maeneo yenye rasilimali hizo, kuongeza gharama za ufugaji na kuhatarisha kipato cha familia.

Kwa wakulima, mabadiliko ya misimu ya mvua yanaweza kuvuruga kalenda ya kilimo, kupunguza uzalishaji wa chakula na kuwalazimu kubadilisha aina za mazao wanayolima.
Hali kama hii pia inawakumba wavuvi na jamii zinazotegemea misitu, kutokana na mabadiliko katika mifumo ya ikolojia na upatikanaji wa rasilimali za asili.
Athari za mabadiliko ya tabianchi kwa jamii za asili
Kwa jamii za asili, ardhi si eneo la kuishi au kuzalisha chakula pekee. Ni sehemu ya historia, utambulisho, utamaduni na urithi wao.
Mabadiliko ya tabianchi yanaposababisha mafuriko, ukame, moto wa misitu na uharibifu wa mifumo ya ikolojia, yanaweza kuathiri maeneo ambayo jamii zimeishi kwa muda mrefu.
Wakati mwingine, familia hulazimika kuhama na kutafuta maeneo mengine yenye maji, chakula na mazingira yanayowezesha shughuli zao za kila siku, si hivyo tu, mabadiliko hayo yanaweza pia kuathiri maarifa ya jadi.
Kwa mfano, wazee katika jamii wanaweza kuwa na maarifa kuhusu misimu ya mvua, aina za mimea ya dawa, mbegu za asili na tabia za wanyama. Maarifa haya hutokana na uzoefu wa muda mrefu wa kuishi na mazingira.
Lakini misimu inapobadilika, mimea inapopotea au wanyama wanapobadilisha maeneo yao ya kuishi, baadhi ya maarifa hayo yanaweza kutotumika tena kama ilivyokuwa awali.
Hali hii inaweza kuvuruga namna maarifa yanavyorithishwa kutoka kwa wazee kwenda kwa vijana na kuhatarisha mwendelezo wa baadhi ya mila na desturi.
Takwimu na ushahidi
Kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa ya mwaka 2025, inayohusu hali ya jamii za asili duniani katika kipindi cha mgogoro wa tabianchi, jamii hizo zinawakilisha takribani asilimia tano ya watu duniani, lakini zinasimamia na kulinda wastani wa asilimia 80 ya bioanuwai iliyobaki duniani.

Aidha, tathmini ya Jopo la Kimataifa la Sayansi kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi, IPCC, inaonesha kuwa mabadiliko ya tabianchi yanaathiri mifumo ya maisha, utofauti wa tamaduni na lugha, usalama wa chakula, afya na ustawi wa jamii za asili.
Takwimu hizi ni ushahidi tosha kuwa kuwa jamii zinazotegemea sana mazingira kwa ajili ya maisha yao zinakabiliwa na changamoto zinazovuka mipaka ya mazingira na kugusa ustawi wao wa kijamii na kiuchumi.
Katika mkutano wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya tabianchi, COP31, uliofanyika Antalya, Uturuki, suala hili lilijadiliwa kupitia Jukwaa la Jamii za Asili na Jamii za Maeneo Husika, LCIPP.
Katika mkutano wa Annual Gathering of Knowledge Holders, uliofanyika Novemba 9 na 10, mwaka 2026, washiriki walijadili namna mabadiliko ya tabianchi yanavyoathiri maisha na mifumo ya jamii mbalimbali.
Msisitizo mkubwa katika mikutano hiyo ilikuwa ni kutambua maarifa ya jamii za asili, kuzingatia uzoefu wao na kuhakikisha wanashiriki katika maamuzi yanayohusu mazingira na maisha yao kwa sababu jamii hizi si waathirika pekee wa mabadiliko ya tabianchi. Pia zina maarifa na uzoefu unaoweza kusaidia kutafuta suluhisho.
Ni muhimu kupaza sauti na kusisitiza kuwa Kulinda jamii za asili dhidi ya mabadiliko ya tabianchi si kulinda maisha yao pekee bali ni kulinda maarifa, tamaduni na mifumo ya asili ambayo imekuwa na mchango mkubwa katika uhifadhi wa mazingira kwa vizazi vingi.


