Mustakabali wa Hewa Safi kwa kila kiumbe

Na Dominic Allen

Msingi wa maisha ya viumbe hai yaani binadamu, wanyama, ndege, wadudu na mimea ni uwepo wa hewa safi katika mazingira yanayowazunguka viumbe hao. Katika kutambua umuhimu wa hewa safi, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mnamo Novemba 26, 2019 liliteua siku ya Septemba 07 kila mwaka kuwa ni siku ya kimataifa ya kuadhimisha Hewa Safi kwa Anga la Bluu duniani.

Siku hii maalumu imelenga kuweka msisitizo na kuongeza uelewa kwa umma katika ngazi zote juu ya umuhimu wa hewa safi katika maisha ya kila siku ya mwanadamu na viumbe vingine. Pasi na shaka uwepo wa dunia bila hewa safi ni sawa na gofu au jumba bovu linalotaraji kuanguka muda wowote.

Ikiwa kauli mbiu ya mwaka huu katika maadhimisho ya siku hii adhimu ni ‘Wekeza kwenye Hewa Safi Sasa’ ni vyema kujiuliza ni wapi tulipotoka, wapi tulipo na wapi tunapoelekea kwenye masuala mazima ya usafi wa Hewa hapa duniani.

Uchafuzi wa Hewa

Suala la uchafuzi wa hewa ulimwenguni limekuwa ni pasua kichwa kwa miaka ya hivi karibuni, Shirika la Afya Duniani (WHO) kupitia tafiti zake linatuarifu kuwa kwa mwaka 2019 asilimia 99 ya watu ulimwenguni wanaishi katika maeneo ambayo yana uchafuzi wa hewa ambao umepitiliza kiwango kilichowekwa na shirika hilo.

WHO inaongeza kuwa uchafuzi wa hewa hupelekea vifo vya mapema. Takribani watu milioni 6.7 kila mwaka hupoteza maisha na uchafuzi wa hewa ukichangia vifo hivyo.

Vyanzo vikuu vya uchafuzi wa hewa ulimwenguni vimegawanyika katika makundi mawili ambapo kundi la kwanza ni uchafuzi unaotokana na shughuli za binadamu ambazo ni shughuli za usafiri za vyombo vya moto kama vile magari, treni n.k, pia moshi wa viwandani na gesi zitokanazo na uzalishaji wa kemikali.

Kundi la pili ni uchafuzi wa hewa unaotokana na vyanzo vya asili; kama vile kuungua kwa misitu, majivu na gesi zitokanazo na mlipuko wa volcano, gesi kama vile Methane ambayo chanzo chake ni kuoza kwa mabaki ya viumbe vilivyokufa ardhini n.k.

Vyanzo vikuu vya uchafuzi wa anga na hewa ulimwenguni.

Uchafuzi wa hewa hauna jema hata kidogo kwani kuna madhara lukuki yatokanayo na uchafuzi wa hewa. Madhara haya yamewalenga siyo tu binadamu na viumbe vingine bali hata mazingira kwa ujumla.

Kwa upande wa wanadamu, uchafuzi wa hewa umekuwa chanzo cha magonjwa ya mfumo wa upumuaji kama vile Nimonia na magonjwa mengine ya macho na ngozi. Mbali na hayo, magonjwa ya moyo na kansa ya mapafu pia husababishwa na uchafuzi wa hewa.

Ripoti ya ‘Hali ya Hewa (SoGA)’ ya mwaka 2021 iliyotolewa na taasisi ya Health Effects kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF) inasema kuwa takribani watu milioni 8.1 kote duniani walipoteza maisha kutokana na hewa chafu.

Ripoti hiyo inaongeza kuwa kwa mwaka 2021 watoto 700,000 wenye umri chini ya miaka 5 walipoteza maisha kwa kuvuta hewa chafu, hii inaonesha sura halisi ya madhara ya uchafuzi wa hewa kwa maana sasa inashika nafasi ya pili kwa kusababisha vifo duniani.

Kama ilivyo kwa wanadamu, uchafuzi huu wa hali ya hewa una athari kwa wanyama, mimea na mfumo wa ekolojia kwa ujumla.

Chembechembe zitokanazo na hewa iliyochafuliwa hurudi ardhini na kuchafua udongo na vyanzo vya maji ambavyo hutumiwa na viumbe hai waishio ardhini na majini.

Chembechembe za Sulfur dioxide na Nitrogen oxide kwenye hewa zikichanganyika na maji na oksijeni angani zinaweza kupelekea mvua za asidi yenye madhara kwa binadamu, wanyama na mazingira kwa ujumla.

Pia, ongezeko la joto duniani ambalo ni changamoto inayoukabili ulimwengu, uchafuzi wa hewa unatajwa kuwa miongoni mwa chanzo chake.

Juhudi za Jumuiya za Kimataifa

Kote ulimwenguni wanaangalia kila namna ya kupambana na uchafuzi wa hewa, lengo likiwa ni kuboresha mazingira na kuwa na hewa safi kwa manufaa ya viumbe na mimea.

Moja ya juhudi za kupambana na changamoto ya uchafuzi wa mazingira, Mkataba wa Kimataifa wa Kyoto ambao umelenga kushughulikia na kuyalinda mazingira ulianza kutekelezwa kwa mara ya kwanza mwaka 1997 yakiwa ni makubaliano baina ya nchi 192 ulimwenguni kote, japokuwa mataifa kama Marekani, Sudan Kusini n.k bado hayajasaini mkataba huo wenye lengo chanya kwa mustakabali wa mazingira yetu.

Nchi zilizosaini mkataba huo wa Kimataifa wa Kyoto na hata zile ambazo hazijasaini tayari zimetunga sheria ili kudhibiti uzalishaji na uchafuzi wa hewa katika nchi zao.

Mwaka 2006 Shirika la Afya Ulimwenguni lilitoa mwongozo mpya wa ubora wa hewa, ambao umelenga kupunguza kwa asilimia 15 vifo vitokanavyo na uchafuzi wa hewa duniani.

Malengo ya Maendeleo Endelevu yana uhusiano wa moja kwa moja na uwepo wa hewa safi, mfano lengo nambari 03 ambalo ni Ustawi na Afya Bora, ili litimie basi kama wanadamu tunayoitaka kesho yetu bora tunatakiwa kuhakikisha tunapambana na uchafuzi wa hewa ambao umekuwa ni chanzo cha magonjwa mbalimbali ambayo yameanishwa hapo awali.

Lengo nambari 11 – Jumuiya na Miji Endelevu, pasi na shaka ili kufikia lengo hilo hakuna budi kuyalinda mazingira kwa kudhibiti uzalishaji na uchafuzi wa hewa kwa ujumla.

Tanzania na Utunzaji wa Hewa

Nchini Tanzania suala la uchafuzi wa hewa bado ni changamoto inayohitaji ufumbuzi, kwani shughuli za usafiri hasa maeneo ya mijini na moshi kutoka viwandani zinatajwa kuwa miongoni mwa sababu zinazochafua hali ya hewa kutokana na uzalishwaji wa hewa chafu ya Kaboni Monoksaidi kutoka kwenye vyombo vya moto kama vile magari, pikipiki n.k pamoja na viwanda.

Shughuli za majumbani kama vile matumizi ya mkaa na kuni huchangia kwa kiasi kikubwa cha ongezeko la hewa chafu katika mazingira ya Tanzania, vile vile uchomaji wa misitu bado ni mwiba unaohitaji kuondolewa ili kufikia malengo ambayo kama taifa tumejiwekea katika sekta ya mazingira.

Kushindwa kudhibiti ipasavyo takataka kutoka viwandani nchini Tanzania hupelekea takataka hizo kwende kwenye vyanzo vya maji ambapo maji yaliyochafuliwa huyeyuka kupitia njia ya mvuke, hivyo uwezekano wa kunyesha kwa mvua yenye maji yasiyo salama kwa matumizi ni mkubwa.

Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 2021 nchini Tanzania ina maono ya kuwa na ‘Tanzania endelevu ambayo ni salama, safi mazingira bora’ lakini ili kufika hapo hatuwezi kuliacha nyuma suala la utunzaji wa hali ya hewa.

Katika sura ya kwanza kifungu 1.2.6 cha Sera ya Mazingira kinakiri uchafuzi wa mazingira umekuwa na athari kubwa sio tu kwenye maji na ardhi bali pia kwenye hewa changamoto ambayo imepelekea madhara makubwa kwa wanadamu na mazingira kwa ujumla.

Tanzania ni nchi ambayo ina ndoto ya kuchimba mafuta na gesi asili ndoto ambayo imedumu tangu kuvumbuliwa kwa gesi asili katika kisiwa cha Songo Songo mwaka 1974 ikifuatiwa na uvumbuzi wa gesi hiyo katika Ghuba ya Mnazi mwaka 1982.

Mwaka 2004 na 2006 uzalishaji wa gesi asili katika kisiwa cha Songo Songo na Ghuba ya Mnazi ulianza; swali la kujiuliza tumejiandaaje kama taifa kufanya uzalishaji huo lakini vile vile tukitunza mazingira, hasa hali ya hewa.

Sera ya Mazingira inakiri kuwa usimamizi wa uzalishaji wa mafuta na gesi asili unakumbwa na changamoto kama vile kushindwa kudhibiti vilivyo uzalishaji au uchafuzi wa hewa unaotokana na udhalishaji wa mafuta na gesi asili.

Kwa mantiki hiyo, kama hatuna usimamizi mzuri katika uzalishaji wa mafuta na gesi ya asili, basi tutarajie madhara makubwa katika mazingira ikiwemo uchafuzi wa hewa na hii itakuwa ni laana tena siyo baraka.

Ikiwa ni malengo ya sera kudhibiti uchafuzi wa mazingira ili kuwa na mazingira salama na yaliyo bora, vyombo husika vinapaswa kupitia upya na kuyasimamia yale ambayo wameazimia katika utunzaji wa mazingira.

Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004, sehemu ya 5 ya Usimamizi wa Mazingira, Uhifadhi wa Angahewa Kifungu 1 (a) Waziri, kwa kushauriana na Wizara ya sekta husika, ana mamlaka ya kufanya au kuagiza watu wengine kufanya uchunguzi wa kitaifa na kutambua maendeleo katika maarifa ya kisayansi yanayohusu vitu, kazi na vitendo vinavyoondoa tabaka la ozoni ya stratosfia na vijenzi vya stratosfia, kiasi cha kuathiri afya ya umma na mazingira.

Katika sheria ya Usimamizi wa mazingira sehemu ya 8 ya Uzuiaji  na Udhibiti wa Uchafuzi, kifungu cha 4 kimetoa katazo kwa mtu yeyote kutoa aina yoyote ya uchafu ambao utasababisha uchafuzi wa hewa, kinyume na viwango vilivyobainishwa au vitakavyobainishwa chini ya sheria hiyo.

Ili kupunguza uchafuzi wa mazingira sheria imetoa viwango vya adhabu kwa yeyote atakayepatikana na hatia ya uchafuzi wa mazingira, ambapo atatozwa faini isiyopungua shilingi Milioni 3 na isiyozidi shilingi Milioni Hamsini au kifungo kisichozidi miaka 12 jela au vyote viwili. Je, hii inatosha katika mapambano dhidi ya uchafuzi wa mazingira? La hasha, elimu kwa jamii bado inahitajika kwa kiasi kikubwa kuliko awali ili kuendana na kasi ya mabadiliko katika maisha ya mwanadamu ya kila siku.

Japo sheria hii imeainisha kufanyika kwa tathmini ya athari kwa mazingira kabla ya taka zenye madhara hazijatupwa udongoni, ardhini, hewani au kwenye vyanzo vya maji, bado jitihada za makusudi zinahitajika kuanzia ngazi za chini ili kudhibiti uchafuzi wa hewa.

Tanzania na Mikataba ya Kimataifa

Tanzania kama yalivyo mataifa mengine kote ulimwenguni inapambana kwa hali na mali kuhakikisha mustakabali wa taifa letu kwenye sekta ya mazingira unakuwa ni bora na salama.

Ili kufikia lengo hilo, mikataba kadhaa ya kimataifa kuhusu utunzaji wa mazingira imepitishwa; Je, italeta matokeo chanya yale tunayoyatarajia?

Mkataba wa Vienna unaohusu hifadhi ya Tabaka la Ozoni ulisainiwa na nchi wanachama mwaka 1985. Mkataba huu ulilenga kuweka ushirikiano miongoni mwa nchi wanachama katika kupeana taarifa za tafiti kuhusu maendeleo ya tabaka la Ozoni lililokuwa limeanza kumo’ngonyoka.

Lengo la Mkataba huo ni kulinda Tabaka la Ozoni na kulinda afya ya binadamu na mazingira dhidi ya madhara yanayotokana na kuharibiwa kwa tabaka la Ozoni.

Tanzania ikiwa ni nchi mwanachama wa mkataba huo inapaswa siyo tu kushiriki kwa jina bali matendo ya Sera, Sheria na Kanuni zinazohusu mazingira yaakisi lengo mkataba huo.

Mkataba wa Vienna unaenda sambamba na Itifaki ya Montreal, yenye lengo la kudhibiti kemikali zinazomongónyoa tabaka la Ozoni kulinda afya ya binadamu na mazingira dhidi ya madhara yanayotokana na kuharibiwa kwa tabaka la Ozoni.

Tanzania inatakiwa kuangalia upya kama usimamizi na udhibiti wa uchafuzi wa mazingira uliyopo sasa unatosheleza kufikia maazimio yaliyowekwa na Itifaki hiyo.

Uzalishaji wa kemikali kutoka viwandani na zile zitokanazo na shughuli za binadamu bila kutarajiwa kumehatarisha usalama wa hali ya hewa. Katika kupambana na changamoto hiyo Tanzania imejiunga na kuwa nchi mwanachama wa Mkataba wa Stockholm kuhusu Udhibiti wa Kemikali zinazodumu kwenye Mazingira kwa Muda Mrefu (Stockholm Convention on Persistent Organic Pollutants- POPs).

Kupitia mkataba huu ushirikiano baina ya Tanzania na jumuiya ya kimataifa katika nyanja za utafiti na uendelezaji wa teknolojia za kudhibiti kemikali zinazodumu kwenye mazingira kwa muda mrefu umeimarika, ijapokuwa uelewa mdogo wa jamii kuhusu kemikali zinazodumu kwenye mazingira kwa muda mrefu imekuwa kikwazo kufikia lengo husika la kulinda afya ya binadamu na mazingira kutokana na athari za kemikali zinazodumu kwenye mazingira kwa muda mrefu.

Bila shaka ili kutanua uelewa kwa wananchi kuanzia ngazi za chini, mipango na mikakati thabiti inahitajika kwa hali na mali ili kuepukana na changamoto hii.

Kuifikia nchi ya ahadi

Tanzania inapaswa kuangalia mambo yafuatayo ili kuondokana na jinamizi hili ya uchafuzi wa hewa ambalo ni tishio ulimwenguni kote.

Mosi, kuboresha usafiri wa umma hasa maeneo ya mijini ili kuepukana na msongamano wa vyombo vya moto vya usafiri ambavyo huzalisha hewa chafu ya Kaboni Monoksaidi ambayo huchafua hali ya hewa na kuongezeka joto duniani.

Pili, usimamizi bora na udhibiti wa takataka zinazozalishwa viwandani ambazo baadhi hutiririka kuelekea kwenye vyanzo maji lakini pia ardhini. Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 inatakiwa isimamiwe na kidete na mamlaka husika kuhakikisha takataka ziwe ni taka ngumu au vimininika vinadhibithiwa kama inavyoelewa na sheria husika pamoja na Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 2021.

Tatu, mamlaka zinazohusika na uhifadhi wa misitu kama vile Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) zinatakiwa kudhibiti ipasavyo na kutoa adhabu zinazostahili kwa wale wanachoma misitu kwani hupelekea siyo tu kuchafua hali ya hewa bali pia kuharibu ekolojia katika eneo husika.

Nne, uboreshwaji wa huduma za kijamii hasa katika matumizi ya nishati za kupikia. Ulimwengu wa sasa jamii inapaswa kuondokana na matumizi ya mkaa na kuni kama chanzo cha nishati ya kupikia na kugeukia kwenye matumizi ya nishati ya gesi na umeme. Lakini serikali ya Tanzania inatakiwa kufahamu kuwa ili wananchi wake waweze kuachana na nishati ambazo ni chanzo cha uchafuzi wa hewa basi maisha yao yanatakiwa yaboreshwe kwanza.

Sera, Sheria, Kanuni na Mikataba ya Kimataifa ambayo Tanzania imesaini pekee haiwezi kutufikisha katika nchi ya ahadi ya kuwa na hewa safi kama hakutakuwa na uwajibikaji kuanzia ngazi ya kaya mpaka ngazi ya taifa.

Serikali ya Jamhuri ya Tanzania inapaswa kutilia mkazo kwa vitendo katika utekelezaji wa mipango na mikakati yake ili kuifikia nchi ya ahadi.

Kila mwananchi anapaswa kuwa balozi wa mazingira kwa kutambua umuhimu wa hewa safi kwa maisha ya kila kiumbe ulimwengu maana bila uwepo wa hewa safi yote tuyafanyayo ni kazi bure.

Mwandishi: Dominic Allen
Mhariri: Yohani Gwangway

Hot this week

Mnyonge, mnyongeni ila haki yake mpeni

By Dorlingson Edward Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS), leo...

CHADEMA kutoa msimamo wake kuhusu maridhiano

By Veronica Mlyatu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetoa...

Popular Articles

Safari ya Mashimba katika kutetea jamii ya Wahadzabe

Nchini Tanzania  kuna jumla ya makabila zaidi ya 120...

Polisi waendelea kuwashikilia viongozi wa CHADEMA

Ni siku ya kwanza tangu kukamatwa kwa viongozi wa...

Siku ya Vijana Duniani.

Kwa sasa ni kijana wa miaka 25 ambaye amejiajiri...

BWAWA LA ARBA’AT  LASABABISHA MAAFA NCHINI SUDAN

Watu 30 mashariki mwa Sudan na na wengine 60...

Sand Mining in Tanzania: Trails of Destruction in Lake Victoria and its Environs

By Dominic Allen On November 14th, 2021 in the Geita...

 Utekaji: Fumbo linalotushinda?

Na Yohani Gwangway Taifa la Tanzania kwa miaka mingi limekuwa...

Abduction: Is it a riddle we can’t solve?

By Yohani Gwangway For many years Tanzania has been an...

Clean Air for Every Creature

By Dominic Allen Survival of all living and non-living organisms...
LAND DWELLERS FACT CHECK HUB VERIFY FACTS STOP MISINFORMATION Trusted Fact-Checking in Tanzania Beyond What You Know VERIFY NOW

Related Articles

Popular Categories

DWELLERS CHECK-HUB Verify Facts. Stop Misinformation Trusted Fact-Checking in Tanzania • Beyond What You Know VERIFY NOW