
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, amesisitiza kuwa viongozi wa dunia wanapaswa kuchukua hatua za haraka na madhubuti ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Amebainisha hayo katika mkutano wa Cop31 wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi unaojadili masuala mbalimbali yanayohusiana na mabadiliko ya tabianchi, yakiwemo ukame, usalama wa chakula na hatua za kukabiliana na athari za mabadiliko hayo duniani unaofanyika huko Antalya, Uturuki ambao imeanza Novemba 9,2026.
Guterres ameonya kuwa matukio ya hali mbaya ya hewa yameongezeka na kuingia katika hatua mpya ya hatari inayotishia maisha ya watu pamoja na uchumi wa dunia. Onyo hilo linakuja kufuatia matukio mbalimbali ya majanga ya hali ya hewa, yakiwemo mawimbi ya joto kali yaliyoikumba Ulaya, moto wa misitu nchini Indonesia na mafuriko yaliyosababisha maafa nchini Nepal.
Tangu kufanyika kwa mkutano wa kwanza wa COP (COP1) jijini Berlin, Ujerumani, mwaka 1995, dunia imekuwa na zaidi ya miongo mitatu ya jitihada za pamoja za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Katika kipindi hicho, mikutano hiyo imeendelea kupanuka kutoka jukwaa la kuanzisha misingi ya ushirikiano wa kimataifa hadi kuwa mikusanyiko mikubwa inayowakutanisha wawakilishi kutoka karibu nchi zote duniani.
Mkutano wa Vyama (COP) ndio chombo kikuu cha kufanya maamuzi chini ya Mkataba wa Mfumo wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC), uliopitishwa mwaka 1992.
