By Veronica Mlyatu
Jamii ya Wahadzabe wa Kata ya Lake Eyasi, Wilaya ya Karatu mkoani Arusha, imegoma kwa kuzuia magari ya watalii kuingia katika maeneo yao, ikidai haki ya kunufaika na mapato yanayotokana na shughuli za utalii ili kusaidia maendeleo ya jamii, ikiwemo kugharamia elimu ya watoto wao.

Mgomo huo ulioambatana na maandamano umeanza Novemba 12, 2026, na kufikia leo Novemba 14 ni siku tatu mfululizo na kusitisha ni mpaka pale mambo yao yatakapokaa sawa, ambapo jamii hiyo inadai kuwepo kwa usawa katika mgawanyo wa mapato ya utalii.
Katibu wa jamii ya Wahadzabe wa Kata ya Lake Eyasi, Wilaya ya Karatu mkoani Arusha, Ismail Nyerere, amesema jamii hiyo inataka kupata gawio la haki kutokana na mapato ya utalii, badala ya kuendelea kushiriki katika shughuli hizo bila kunufaika nazo.

Akizungumza na Land Dwellers, Ismail amesema suala hilo limewaumiza wanajamii wengi na kusababisha idadi kubwa ya watu kujitokeza katika maandamano hayo wakidai haki yao ya kunufaika na utalii unaofanyika katika maeneo yao.
Amesema jamii hiyo inataka kunufaika na utalii wa ndani wanaousimamia na kuufanya wenyewe, ili mapato yanayotokana na shughuli hizo yaweze kuchangia kuboresha maisha yao.
Kwa upande wa Halmashauri, Ismail amesema halmashauri haijataka kusikiliza bali walisema hii imeandikwa ni lazima itekelezwe na wao wakatoa wito kama jamii kuwa halmashauri izingatie kwa hilo ili jamii na yenyewe iweze kunufaika kwa chochote.

Kutokana na hali hiyo, jamii imeitaka Halmashauri kusikiliza kilio chao kwa kuzingatia madai yao ili nao waweze kupata sehemu ya mapato yanayotokana na utalii unaofanyika katika maeneo yao.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa jamii ya Wahadzabe, Msafiri Tom, akizungumza na mwandishi wetu Dominic Allen, ameitaka Serikali kuhakikisha haki inatendeka kwa kuzingatia usawa na bila upendeleo, huku bei za huduma za utalii zikiwekwa wazi na kutekelezwa kwa uhalali, bila kujali ukubwa au udogo wa mtu, ili kila mmoja anufaike kwa haki sawa.


