Na Dominic Allen
Muungano wa kutetea haki za Wamasai, Maasai International Solidarity Alliance (MISA), umetoa tamko kupinga vikali mapendekezo ya Tume mbili za Rais zilizoundwa kutathmini masuala yanayolalamikiwa na wakazi wa wilaya ya Ngorongoro pamoja na kutathmini uhamaji wa wananchi kutoka Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, ambapo wamesema kuwa mapendekezo hayo hayazingatii maoni ya wananchi, na yanaweza kuongeza migogoro badala ya kuitatua.
Katika tamko hilo lililotolewa jana Machi 18, 2026 kufuatia ripoti zilizowasilishwa Machi 12, 2026, MISA wamesema baada ya kufanya tathmini ya kina, wamefikia uamuzi wa kuyakataa mapendekezo hayo yote. “Baada ya kuyapitia kwa makini, tunakataa kabisa mapendekezo ya Tume hizi,” imeeleza sehemu ya tamko hilo.
MISA wameeleza kuwa mchakato wa Tume hizo ulikuwa na kasoro tangu mwanzo, na kwamba haukulenga kusikiliza wananchi bali kuhalalisha maamuzi yaliyokwishafanyika. “Tangu mwanzo, masharti ya kazi ya Tume yaliundwa ili kuhalalisha maamuzi yaliyokuwa tayari yamefanyika. Tume zote mbili zilijikita zaidi katika namna ya kutekeleza uhamishaji kutoka Tarafa ya Ngorongoro badala ya kushughulikia matatizo yaliyowasilishwa na wakazi,” limeeleza tamko hilo.
Kwa mujibu wa MISA, licha ya wananchi wengi kujitokeza kutoa ushahidi wakitarajia kupata suluhisho la migogoro ya ardhi, maoni yao hayakuzingatiwa, ambapo wameonya kuwa utekelezaji wa mapendekezo hayo unaweza kuongeza migogoro iliyopo badala ya kuipunguza.
MISA wamesema kuwa ripoti za Tume hazikuwa na uhuru wala sio za kuaminika katika kutathmini hali halisi ya wananchi wa Ngorongoro, Loliondo, Sale na Msomera, ambapo kwa kiasi kikubwa zimetegemea nyaraka za sera zilizowahi kupingwa na kurudia sababu ambazo zimekuwa zikitumika kuhalalisha kuondolewa kwa wafugaji wamasai katika ardhi yao ya asili.
Aidha, tamko hilo la MISA limeeleza kuwa hitimisho la Tume za Rais limeegemea kwenye takwimu zenye upungufu na upendeleo, “Hitimisho lililotolewa linategemea makadirio yaliyopitiliza ya idadi ya watu, matumizi ya takwimu zisizo sahihi kuhusu binadamu, mifugo na wanyamapori, pamoja na migongano mikubwa ya kimaslahi ya taasisi, huku likipuuza ushahidi wa kisayansi unaopingana na mitazamo ya serikali,” limefafanua tamko hilo.
Vilevile, MISA wamepinga vikali hoja kwamba uwepo wa Wamasai ni tishio kwa uhifadhi wa mazingira, ikisisitiza kuwa jamii hizo zimeishi kwa muda mrefu kwa kushirikiana na wanyamapori.
“Kwa vizazi vingi, sisi Wamasai tumeishi Ngorongoro kwa mfumo wa kuishi pamoja na wanyamapori. Maisha yetu ya ufugaji si tishio kwa uhifadhi; kinyume chake, maarifa yetu ya jadi na mifumo ya matumizi ya ardhi ya kijamii imekuwa ikiendeleza mfumo huu wa ikolojia kwa karne nyingi,” limeeleza tamko hilo.
Kwa upande mwingine, MISA wameeleza wasiwasi juu ya kupuuzwa kwa athari za upanuzi wa shughuli za utalii, hoteli za kifahari na uwindaji, huku jamii za wafugaji zikibebeshwa lawama kuhusu uharibifu wa mazingira.
Katika sehemu nyingine, MISA wamekemea kitendo cha Tume hizo kutoiwaijibisha serikali kwa kuondoa baadhi ya huduma za kijamii katika Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, jambo lililopelekea baadhi ya wakazi kukubali kuondoka kutokana na kukosa huduma muhimu.
“Jamii zetu zimekumbwa na vikwazo visivyokubalika katika huduma za msingi, upatikanaji wa ardhi na miundombinu ya kijamii, hali iliyowalazimisha watu wetu kuondoka katika makazi yao si kwa hiari bali kwa shinikizo la kunyimwa mahitaji muhimu,” wameeleza MISA.
MISA wamelaani ukimya wa Tume hizo kuhusu madai ya unyanyasaji dhidi ya Wamasai, ikisema hali hiyo inaashiria upendeleo. Pia imeeleza wasiwasi wake kuhusu matukio ya hivi karibuni ya ukamataji wa wakazi na kuamriwa kuondoka katika maeneo yao ili kupisha shughuli za utalii.
Kuhusu Ziwa Natron, MISA wamepinga vikali mapendekezo ya kuligeuza kuwa hifadhi ya wanyamapori, ikisisitiza kuwa eneo hilo ni ardhi ya vijiji kwa mujibu wa sheria za Tanzania.
“Tunapinga kauli kwamba Ziwa Natron ni Eneo la Hifadhi ya Wanyamapori (GCA). Eneo hili lina vijiji 26 na zaidi ya watu 70,000, na kwa mujibu wa sheria za Tanzania, hakuna GCA inayoweza kuanzishwa katika ardhi ya vijiji,” wameeleza MISA.
Wamesisitiza msimamo wao wa kupinga uhamishaji wa aina yoyote kutoka katika maeneo yao. “Tutaendelea kusimamia haki yetu ya kubaki na kuishi katika maeneo haya,” limeeleza tamko hilo, huku likitoa wito kwa serikali kutambua na kulinda haki zao.
MISA wametoa wito kwa jumuiya ya wafadhili wa kimataifa, mashirika ya uhifadhi, Shirikisho la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira (IUCN) pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kuunga mkono maono ya uhifadhi ya Wamaasai, na kuacha kuendeleza mifumo ya uhifadhi ambayo haiheshimu watu wa jamii za asili.
Mwandishi: Dominic Allen
Mhariri: Yohani Gwangway


