Mfumo wa awali wa utambuzi wa ahadi na hatua za kufikia uzalishaji halisi sifuri wa gesi joto, unaoitwa Net-Zero Recognition Framework (NZRF), umeanza kwa kujumuisha mipango nane inayokidhi vigezo vya ushiriki, ikiwa na wadau 78 waliojiunga kwa hiari katika kipindi cha miezi miwili kabla ya COP31.
Wadau hao wanajumuisha serikali za maeneo mbalimbali zinazowakilisha zaidi ya watu milioni 65, pamoja na kampuni na mashirika kutoka nchi 22. Baadhi ya kampuni hizo zinaendesha shughuli zake katika zaidi ya nchi 100 na zinatoka katika sekta mbalimbali za kiuchumi.
Mfumo huo umeweka hatua tano za kupima maendeleo ya wadau kuelekea kufikia uzalishaji halisi sifuri wa gesi joto. Hatua hizo ni kutangaza ahadi hadharani, kuandaa mipango ya mpito, kuonesha maendeleo ya utekelezaji, kutimiza malengo ya muda wa kati na kufikia lengo la mwisho la uzalishaji halisi sifuri.
Mkurugenzi wa Uwazi wa UN Climate Change, Xuehong Wang, amesema kuweka wazi maendeleo hayo kutasaidia kubaini mapungufu yaliyopo katika utekelezaji wa ahadi hizo.
Uzinduzi huo umefanyika sambamba na mijadala mingine ya COP31 iliyofanyika leo, ikihusisha utekelezaji wa Mkataba wa Paris, upatikanaji wa fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, ustahimilivu wa miji na hatua za kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi zisizo za kaboni dioksidi.
Katika mkutano wa viongozi kuhusu gesi hizo, UN Climate Change imeripoti ahadi mpya za ufadhili wa zaidi ya dola milioni 480 kutoka kwa taasisi za ufadhili wa hisani, pamoja na dola milioni 25 kwa ajili ya kuharakisha hatua za kupunguza uzalishaji wa gesi zenye uwezo mkubwa wa kuongeza joto duniani.


