Siku ya Maji Duniani: Zaidi ya watu bilioni 2.2 wanakumbana na Uhaba wa maji

Na Yohani Gwangway

Dunia huadhimisha Siku ya Maji tarehe 22 Machi ya kila mwaka ikiwa ni kumbukumbu ya kuhimiza upatikanaji wa maji pamoja na kutekeleza Lengo Namba 6 la Maendeleo Endelevu duniani ambalo ni upatikanaji wa maji safi na salama kwa kila mtu hadi kufikia mwaka 2030. Kauli mbiu ya mwaka huu ni “Uhifadhi wa Barafu”.

Maadhimisho ya siku hii yalianza kuadhimishwa  tangu mwaka 1993 baada ya  Umoja wa Mataifa (UN) kuazimia kuwa na siku inayoenzi upatikanaji wa rasilimali hii muhimu kwa binadamu, wanyama na viumbe vyote hai. Ikiwa idadi ya watu kote duniani inakadiriwa kufikia watu bilioni 8.2 mwaka huu, matumizi ya maji yanaongezeka.

Maji yamekuwa yakitumika katika kwa matumizi ya nyumbani kama kunywa, kupikia na kufulia nguo huku kukiwa na matumizi mengine ya usafi, kumwagilia, matumizi ya viwanda pamoja na mahitaji mengine.

Siku hii inaadhimishwa huku takriban watu bilioni 2.2 kote duniani hawapati maji safi na salama, kwa mujibu wa  takwimu za Umoja wa Mataifa (UN) za mwaka 2022. Kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa kumekuwa na uhaba wa mvua unaosababisha ukame katika sehemu mbalimbali za dunia. Mabadiliko ya tabia ya nchi kwa sasa ndiyo yanaathiri jamii nyingi katika sekta za uzalishaji hasa kilimo.

Madhara ya ukame tangu  2002-2021

Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa (UN), kuanzia mwaka 2002 hadi 2021, ukame umekumba zaidi ya watu bilioni 1.4 huku ukisababisha vifo zaidi ya 21,000. Ukame huu umetokea katika mataifa tofauti tofauti na kusababisha dunia kushindwa kupata angalau chakula kwa matumizi ya binadamu. Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa (UN) , Ukame umesababisha hasara ya dola bilioni 170 katika kipindi cha miaka 19, yaani kuanzia mwaka 2002 hadi 2021. Kwa hiyo tunapoadhimisha Siku ya Maji Duniani, hii ni kumbukumbu muhimu ili kutambua umuhimu wa rasilimali ya maji.

Hali ya matumizi ya maji duniani

Kati ya viumbe wote duniani, binadamu ndiye anayetumia kiasi kikubwa cha maji kutokana na matumizi binafsi ama shughuli mbalimbali. Shughuli ya kilimo hutumia maji mengi yanayozalishwa duniani kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa (UN). Shughuli ya kilimo pekee huchukua asilimia 70 ya maji, huku asilimia 20 ikiwa ni viwanda na asilimia 12 ni matumizi ya kawaida ya nyumbani pamoja na mijini.

Lengo Namba 6 la Maendeleo Endelevu ni kuwa kila mtu apate maji pamoja na kuboresha usafi ifikapo mwaka 2030. Umoja wa Mataifa (UN) uliweka Viashiria 6 katika kutekeleza lengo hili. Viashiria hivi vinapima ni kwa kiasi gani lengo linafikiwa. Viashria vya lengo hili ni kama ifuatavyo;

Maji safi ya kunywa

Kwa sasa takwimu za Umoja wa Mataifa (UN) ambazo zilikusanywa kutoka kwa mataifa yote ambayo ni wanachama wa umoja huu zinaonesha kuwa angalau watu bilioni 6 kote duniani sawa na silimia 73 wanapata huduma ya maji safi ya kunywa.  Hii ni moja ya kiashiria muhimu cha mataifa mengi kupiga hatua licha ya changamoto za utunzaji wa vyanzo vya maji, ukame na uharibifu wa mazingira. Huu ni wastani wa upatikanaji wa huduma ya maji ya kunywa kwa mataifa wanachama wa UN. Bado kunahitajika juhudi za kuhakikisha idadi kubwa ya watu inafikiwa na huduma ya maji kote duniani.

Usafi wa mazingira pamoja na usafi binafsi

Kiashiria hiki kinalenga kuonesha upatikanaji wa huduma ya maji yanayoweza kusaidia usafi wa mazingira, kama vile usafi wa maliwato, maji ya kufulia na usafi binafsi ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa maji ya kuoga kwa kila familia. Kwa takwimu zilizotolewa na Shirika la Kimataifa la kuhudumia Watoto (UNICEF) pamoja na Shirika la Afya Duniani (WHO) mwaka 2022, hali ya upatikanaji wa maji kwa ajili ya masuala ya usafi dunia imefikia asilimia 57 huku kwa upande wa usafi binafsi dunia ikifikia asilimia 75. Hii inamaanisha kuwa bado huduma ya maji kwa ajili ya usafi bado haijatosheleza huku angalau robo tatu ya watu duniani wakipata maji kwa ajili ya usafi binafsi. Kufikia asilimia 100 ya kiashiria hiki kunahitaji juhudi za pamoja kati ya serikali pamoja na wadau wengine.

Ubora wa maji

Umoja wa mataifa katika lengo lake Namba 6 la upatikanaji wa maji pamoja na usafi wa mazingira wameweka pia kiashiria cha ubora wa maji. Ubora wa maji hupimwa kisayansi kwa kujua maji hayo yamebeba nini na yanafaa kwa matumizi gani. Kwa maana hiyo suala siyo tu usambazaji wa maji, lakini suala muhimu ni kuhakikisha maji yenye ubora yanawafikia wananchi. Katika kiashiria hiki Umoja wa Mataifa (UN)  unasema kwa sasa dunia imefikia asilimia 56 ikiwa ni wastani wa takwimu za ubora wa maji kutoka kwa wanachama mbalimbali. Kwa lugha rahisi ni kuwa ni angalau nusu tu ya watu wote duniani wanapata maji yenye ubora unaotakiwa kwa matumizi ya aina fulani. Hapa pia bado safari ni ndefu kutokana na uchafuzi wa mazingira pamoja na vyanzo vya maji. Kama mazingira yatakuwa safi na vyanzo vya maji vitalindwa ni rahisi kupata maji yenye ubora kwa matumizi ya binadamu na wanyama wengine

Mfumo wa ikolojia unaohusiana na maji

Katika kuangalia upatikanaji wa maji, Umoja wa Mataifa (UN) umeweka kiashiria cha mataifa husika kupima na kurekodi mabadiliko ya mfumo wa ikolojia unaohusiana na maji. Mabadiliko yoyote katika mfumo wa ikolojia ikiwa na pamoja na mimea au aina ya viumbe waliopo pamoja na masuala mengine yanaweza kuathiri upatikanaji wa maji. Kwa sasa Umoja wa Mataifa (UN) unasema kuwa kuna mabadiliko ya haraka katika mabonde ya maji kwa asilimia 21. Shirika la Mazingira Duniani UNEP linasema kuwa mabadiliko haya yanatokea kwenye maziwa, mito na mikoko. Mabadiliko haya ni kama mafuriko, kuongezeka au kupungua kwa kina cha maji, mabadiliko ya barafu kwenye milima, kiwango cha misitu na mengineyo. Ni muhimu kuelewa kuwa ili kufikia Lengo Namba 6 la Maendeleo Endelevu, mabadiliko haya ya haraka yanahitaji kupunguzwa.

Usimamizi jumuishi wa rasilimali za maji

Umoja wa Mataifa (UN) umeweka kiashiria cha usimamizi jumuishi wa rasilimali za maji kati ya serikali na watu wake, taifa moja na taifa lingine au hata ukanda kwa ukanda ili kuwa na malengo ya pamoja juu ya matumizi sahihi ya rasilimali za maji. Kiashiria hiki kina mawanda makuu manne ambayo ni mazingira, taasisi na ushiriki wake, vyombo vya usimamizi pamoja na fedha kwa ajili ya miradi ya maji. Kwa sasa UN inasema kuwa wamefikia asilimia 57 ya kiashiria hiki muhimu cha usimamizi jumuishi.

Ufanisi katika matumizi ya maji

Kiashiria hiki kinapima ni kwa namna gani rasilimali iliyopo inaweza kutumika kwa ufanisi kwa kutumia teknolojia na njia za kisasa. Kwa mfano, kama mji unazalisha lita milioni 100 kwa siku basi angalau kuwe na njia bora ili kiwango hicho hicho kiwafikie watumiaji. Kama lita laki 3 kati ya hizo zitapotea njiani kutokana na ubovu wa miundombinu ya maji, basi bado hakuna ufanisi katika matumizi ya maji. Kwa sasa Umoja wa Mataifa (UN) unasema kuwa kutokana na matumizi ya njia za kisasa, basi kuna faida ya dola 21 kwa kila mita moja ya ujazo wa maji. Lengo la kishiria hiki ni kutumia kiwango cha chini cha rasilimaji maji kutokana na ufanisi na ubora wa njia za kisasa zinazotumika kuvuna rasilimali maji

Hali ya usamabazaji wa maji Tanzania

Nchini Tanzania jitihada mbalimbali zimefanyika katika kuhakikisha watu wanapata maji. Kwa mujibu wa taarifa ya Benki ya Dunia iliyochapishwa mwaka 2023, Upatikanaji wa maji ya kunywa  nchini Tanzania umefikia asilimia 74%, Upatikanaji wa maji kwa matumizi ya familia 72% na Upatikanaji wa maji ya tiriririka ya kunawa ni 41.%.

Taarifa ya serikali ya mwaka 2021

Kupitia Wizara ya Maji, serikali inasema upatikanaji wa huduma ya maji umeongezeka kutoka asilimia 64 mwaka 2019 hadi asilimia 72 mwaka 2021. Taarifa ya serikali inasema Vijiji 8,708 kati ya 12,327 vinapata huduma ya maji kutokana na miradi 1,139 iliyotekelezwa ya Wakala wa Usambazaji wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini, RUWASA.

Malengo ya serikali ya Tanzania

Serikali ya Tanzania inasema inataka watu kupata maji safi kwa asilimia 85 maeneo ya vijijini mwaka 2025, huku ikilenga asilimia 95 ya upatikanaji wa maji katika maeneo ya mijini. Tanzania inaonesha kuanzisha miradi mingi ya maji licha ya kukabiliwa na upotevu wa maji yasiyolipiwa pamoja na usimamizi mbaya wa miradi ya maji hapa nchini.

Kesho tuitakayo

Tanzania kama yalivyo mataifa mengine inahitaji kupiga hatua katika utoaji wa huduma ya maji. Na jambo la msingi zaidi ni taifa kuzingatia Viashiria 6 vya Lengo Namba 6 la Maendeleo Endelevu ambalo linalenga upatikanaji wa maji kwa watu wote duniani hadi kufikia mwaka 2030. Pia Tanzania inatakiwa kuzingatia kiashiria cha ubora wa maji, kwa sababu kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), watu bilioni 1.7 wanatumia maji yalichonganyikana na kinyesi ambayo yanahatarisha afya zao. Malengo ya pamoja na jumuishi yatasaidia Tanzania kupiga hatua katika usambazaji wa rasilimali hii muhimu kwa viumbe hai.

Mwandishi: Yohani Gwangway
Mhariri: Dominic Allen

Hot this week

Mnyonge, mnyongeni ila haki yake mpeni

By Dorlingson Edward Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS), leo...

CHADEMA kutoa msimamo wake kuhusu maridhiano

By Veronica Mlyatu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetoa...

Popular Articles

Safari ya Mashimba katika kutetea jamii ya Wahadzabe

Nchini Tanzania  kuna jumla ya makabila zaidi ya 120...

Polisi waendelea kuwashikilia viongozi wa CHADEMA

Ni siku ya kwanza tangu kukamatwa kwa viongozi wa...

Siku ya Vijana Duniani.

Kwa sasa ni kijana wa miaka 25 ambaye amejiajiri...

BWAWA LA ARBA’AT  LASABABISHA MAAFA NCHINI SUDAN

Watu 30 mashariki mwa Sudan na na wengine 60...

Sand Mining in Tanzania: Trails of Destruction in Lake Victoria and its Environs

By Dominic Allen On November 14th, 2021 in the Geita...

 Utekaji: Fumbo linalotushinda?

Na Yohani Gwangway Taifa la Tanzania kwa miaka mingi limekuwa...

Abduction: Is it a riddle we can’t solve?

By Yohani Gwangway For many years Tanzania has been an...

Mustakabali wa Hewa Safi kwa kila kiumbe

Na Dominic Allen Msingi wa maisha ya viumbe hai yaani...
LAND DWELLERS FACT CHECK HUB VERIFY FACTS STOP MISINFORMATION Trusted Fact-Checking in Tanzania Beyond What You Know VERIFY NOW

Related Articles

Popular Categories

DWELLERS CHECK-HUB Verify Facts. Stop Misinformation Trusted Fact-Checking in Tanzania • Beyond What You Know VERIFY NOW