“Niliwahi kufikiria kunywa sumu”: Dimbwi la madeni kwa wafanyabishara

Na Yohani Gwangway

Ashura ni mjasiriamali na mama wa watoto watatu ambaye anaishi katika Wilaya ya Nyamagana  jijini Mwanza. Takriban miaka mitatu iliyopita Ashura alikuwa katika ndoa na mume wake wakiwa na furaha na amani. Lakini kwa sasa ndoa ya Ashura imevunjika baada ya ugomvi kati yake na mume wake uliotokana na kitendo cha ashura kukopa pesa kwa siri kutoka taasisi ndogo za fedha yaani Microfinance na baadaye kushindwa kulipa kutokana na riba kuwa kubwa hivyo deni kuongezeka.

Simulizi  hii ya  Mama wa Makamo mwenye umri wa miaka 42 ambaye ni mhanga wa  ya madhila ya kukopa kwenye tasisi ndogo za fedha ambaye sasa ndoa yake imevunjika baada ya kuibuka mgogoro katika familia yake. Katika sehemu hii ya pili ya makala hii tutaangazia madhara yatokanayo na kutosimamiwa vizuri kwa sheria ya fedha ya mwaka 2018 ya taasisi ndogoza fedha ambazo zipo chini ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Utoaji wa huduma  za kifedha wa taasisi ndogo za fedha nchini Tanzania upo chini ya Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018 pamoja na Kanuni zake (watoa huduma ndogo za kifedha wasiopokea amana). Kwa mujibu wa Wizara ya fedha hapa nchini, kiwango cha riba ambacho kitatozwa kwa waombaji wa mikopo kutoka kwenye taasisi hizo ni asilimia 3.5 kwa mwezi.

Wafanyabiashara hasa wadogo hujikuta wakizama katika dimbwi la madeni baada ya kushindwa kulipa mikopo hiyo kutokana riba kubwa, jambo linalopelekea madhara mengine mengi katika maisha yao ya kila siku.

Migogoro ya ndoa na ndoa kuvunjika

Kati ya wakopaji zaidi ya 10 waliohojiwa, angalau mmoja aliwahi kukutana na chngamoto ya migogoro kwenye ndoa yake au kufahamu mtu mwingine ambaye ndoa yake iliingia kwenye migogoro kutokana na kushindwa kulipa mikopo hii.

Ashura ambaye simulizi yake ilianza katika sehemu ya kwanza ya makala hii anawakilisha kundi la mamia ya wanawake hapa nchini ambao ni wahanga wa mikopo ya taasisi ndogo za fedha ambazo baadhi hazifuati miongozo, kanuni na sheria ya iliyopo. Baada ya mume wa Ashura kugundua kiasi cha fedha wanayodaiwa aliamua kumtimua mke wake na ndoa yao kuvunjika.

Licha ya Ashura kumbembeleza mume wake ndoa yao ilifikia tamati mwaka 2023. Baadhi ya vitu vyao vya ndani vilichukuliwa ikiwemo Televisheni, Masofa, Kabati na vitu vingine vya thamani kama fidia ya deni hili. Kwa sasa Ashura ameanza maisha upya akiwa hana mtaji, ndoa yake ikiwa imevunjika huku baishara aliyokuwa anaifanya ikiwa imekufa.

“Mume wangu aliwaruhusu wachukue vitu vyetu ila alisema ndoa haiwezi tena kuendelea. Vitu vingi vilichukuliwa na mtaji wangu mdogo uliobaki nilimpa mume wangu ili awape wanaotudai. Sasa hivi hakuna kinachoeleweka na ninaona nimeanza maisha upya.”

Katika eneo la Nyahingi wilaya ya Nyamagana jijini Mwanza, Amina ambaye ni mama wa mtoto mmoja alikimbia nyumba yake baada ya kudaiwa na taasisi moja ya mikopo iliyo katika kata ya Mkolani. Amina aliyekuwa amekopa shilingi milioni 1.8 alishindwa kulipa deni hilo jambo lilipelekea deni lake kufikia shilingi milioni 4.

Amina alikuwa akiishi mwenyewe katika nyumba yake na baada ya kushidwa kurejesha alitoroka kuepuka wanaomdai. Baada ya Amina kuondoka, maafisa waliotoka katika taasisi hiyo walifika kwake na kungoa madirisha ya Alluminiam huku wakiondoka na vitu vilivyo nje ya nyumba yake.

“Niliona usumbufu ulizidi nikaamua kuondoka ili niwatafutie hela yao. Baada ya kuondoka hajapita hata siku tatu, majirani walinipigia simu kuwa madirisha ya nyumba yako yamengolewa na maafisa wa taasisi iliyokuwa inanidai. Ilikuwa aibu kwa sababu watu wengine walikuwa hawajui kama nadaiwa. Walichukua madirisha na nje kulikuwa na banda la kuhamisha la kuku nalo walilibeba.” Maelezo ya Amina kuhusu mkopo aliouchukua.

Kushuka kwa kiwango cha uzalishaji

Visa na mikasa vya wakopaji imeleta athari mbalimbali katika maisha yao. Maira ambaye  ni mchuuzi wa samaki aliposhindwa kulipa deni analodaiwa baiskeli zake mbili  ambazo ndiyo anzitumia katika usambazaji zilichukuliwa. Wakati huu Miara alishindwa kufanya kazi yake kwa ufanisi kwa sababu hakuwa na usafiri. Licha ya kupamabana kurudisha baiskeli moja, Maira alipoteza baiskeli nyingine.

Kwa Maira, kuchukuliwa baiskeli yake ya pili ambaye ilimuwezesha kuzunguka akiwa na msaidizi wake kumepunguza ufanisi katika kazi yake. Yeye anaona kuwa kutokuwa na uelewa kulimpoza licha ya kuhitaji fedha wakati anachukua mkopo.

“Wakati nachukua mambo hayakuwa magumu. Niliona nitamudu kulipa mkopo ndani ya muda. Walipochukua baiskeli yangu ya pili ambayo alikuwa anatumia msaidizi wangu, usambazaji wa Samaki umeshuka na kipato pia kimepungua,” Maira akieleza matokeo ya kushindwa kulipa mkopo kwa wakati.

Msongo mawazo kwa wakopaji

Wakati wengine wakilalamika, Kwa Ashura ambaye ambaye sasa hana mtu wa kumsaidia baada ya ndoa yake kuvunjika, msongo wa mawazo ni tatizo lingine analokabiliana nalo na mawazo ambayo yamekuwa yakimsononesha akiwa na kumbukumbu ya ndoa yao ya amani ambayo sasa imebaki historia.

“Napata wakati mgumu nikiwaza maisha yangu yalivyobadilika, mimi siyo wa mume, siyo wa hela. Hata watu wa karibu yangu wanaona  nimekosea na marafiki wengine wananitenga. Suala hili limenipata mimi japo na wengine linawapata. Wakati mwingine silali usiku nikiwaza cha kufanya kurekebisha makosa yaliyotokea. Nimepanga kuendelea kumbembeleza mume wangu kwa sababu bado hajaoa mwanamke mwingine,” anaeleza Ashura, mhanga wa ukopaji wa riba kubwa.

Wakati Ashura akipitia hali hii, Amina Mohamed ambaye naye alishindwa kurudisha mkopo anaodaiwa na baadaye kuondoka sasa amerudi katika nyumba ambayo tayari imeondolewa madirisha. Kama ilivyo kwa Amina simulizi ya mikopo hii kwake ni ya shubiri licha ya umuhimu wake kwa jamii kama miongozo ingegekuwa wazi na kusimamiwa na mamlaka zinazohusika.

“Ninasikitika kuanza upya nyumba ambayo tayari nikuwa hatua za mwisho za umaliziaji. Nimepata fedheha kwa ndugu zangu na marafiki zangu wa karibu. Kwanza hata kipindi ninadaiwa jinsi nilivyokuwa ninafuatwa ilizusha maswali. Na mambo haya yakitokea jamii inajua huyu ana hali mbaya kiuchumi. Hili linakuwa siyo jambo lako tena,” alisema Amina kuhusiana na magumu anayopitia sasa hivi.

Nchini Tanzania matukio ya watu kuwa na sonona pamoja na matatizo ya afya ya akili yanayosababisha kufanya maamuzi mabaya yamekuwa yakiripotiwa kila kukicha. Licha ya kuwa hakuna ushahidi wa moja kwa moja kuwa madeni ni sehemu ya sababu ya watu kuchukua hatua kama kujiua au kutupa hata watoto kutokana na ugumu wa maisha, lakini huenda jambo hili linaweza kupelekea watu kufanya maamuzi ya aina hii kama hatua hazitachukuliwa

“Fikiria unajifungia ndani ili usionekane. Unalia hata masaa mawili ukitoka nje hakuna anayeelewa matatizo yako. Unaficha ili kila mtu asijue matatizo. Haya mambo yanaweza kusababisha mtu kufanya maamuzi mabaya. Binafsi niliwahi kufikiria kunywa sumu lakini kila nilipomwangilia mtoto wangu niliahirisha,” Amina akizungumzia jinsi mawazo yalivyomtesa.

Kushindwa kulipa mkopo na kufilisiwa

Wateja wanaopitia madhila ya kukopa bila kufahamu kiwango halisi cha riba au kuelewa kiwango hicho kimahesabu wamekuwa wakiingia kwenye madeni, wengine kufiliswa na wengine kuyumba kiuchumi . Katika Mkoa wa Mwanza kuna matukio ya watu kufilisiwa au kuchukuliwa vitu muhimu. Baadhi ya waliokumbana na matukio haya kama Ashura na Amina wanaona kuwa bado ufuatiliaji siyo mzuri.

“Vitu vinachukuliwa na taasisi ambazo zina ofisi. Zinaonekana na zinajulikana na ofisi za mitaa yetu. Hata siku moja sijawahi kusikia viongozi wakidadisi mambo yanayotokea kwa taasisi hizi.” Amina kuhusu watu kufilisiwa.

Land Dwellers ilijaribu kuwatafuta baadhi ya viongozi wa mitaa minne katika Wilaya Nyamagana ambao kwa nyakati tofauti walisisitiza hawako tayari kuzungumzia jambo hili kwa kuwa halipo chini ya usimamizi wao lakini pia kuna mambo ya uchaguzi yanayoendelea nchini ambayo yanaweza kuchonganisha wananchi na serikali.

Land Dwellers imedadisi jambo hili na kugundua kuwa ni kweli baadhi ya taasisi hizi zinafilisi wateja wao bila kufuata kanuni ya dhamana iliyowekwa na Sheria Ndogo ya Fedha ya mwaka 2018 na Kanuni zake za mwaka 2019. Matukio ya watu kuchukuliwa vitu kama masofa, kabati, pikipiki, baiskeli, televisheni, vitanda na vingine vya thamani yameripotiwa licha ya wafanyabishara wengine kutokuwa tayari kueleza kwa undani.

Jambo hili liliwasilishwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ambao ndiyo wasimamizi wa taasisi ndogo za fedha(Microfinance). Kwa upande wa BoT inadai kuwa taasisi zinazotoza riba kubwa ni zile ambazo hazina ofisi na pia hazijasajiliwa.

“Hili linatokana na uwepo wa watoa huduma ndogo za fedha wanaofanya bishara bila kuwa na ofisi, leseni/kibali au kusajiliwa ambao kwa kiwango kikubwa wamekuwa hawaendeshi bishara zao kwa kufuata Sheria, kanuni na Miongozo iliyowekwa.” Maelezo ya Benki Kuu yaliyotumwa kwa Land Dwellwers kupitia njia ya maandishi.

Pia, BoTilikiri kuwa kuna tatizo hili hata kwa taasisi zilizosajiliwa ambazo hawataki kufuata sheria na miongozo iliyopo huku BoT ikisema kuwa kwa upande mwingine jambo hili linasababishwa na uelewa mdogo wa wananchi kuhusu masuala ya fedha.

“Vilevile kuwepo kwa watoa huduma wenye leseni ambao hutoa mikopo bila kuzingatia matakwa ya sheria na kanuni ya usimamizi wa watoa huduma ndogo za fedha ikiwemo kanuni ya kumlinda mtumiaji wa fedha. Pia uelewa mdogo wa Wananchi kuhusu masuala ya fedha.” Taarifa ya BoT kwa Land Dwellers.

Taarifa ya benki kuu ilisisitiza kuwa wanaendelea kutoa elimu kwa wananchi pamoja na watoa huduma wasio na leseni ambapo hadi sasa wametoa elimu katika mikoa ya Kigoma, Mwanza, Mara Morogoro Arusha na Manyara ambazo zaidi ya washiriki 600 walifikiwa.

Kwa nyakati tofauti tofauti BoT pia imekuwa ikishirikiana Jeshi la Polisi kufanya operesheni maalum katika maeneo mbalimbali nchini dhidi ya taasisi ndogo za fedha zinazotoa huduma hizo bila kuwa leseni.

“Aidha Benki Kuu kwa kushirikiana na Jeshi la polisi imefanya na inaendelea na operesheni maalum ya kuchunguza, kuwakamata na kuwafikisha Mahakamani watoa huduma wasiokuwa na leseni ambao wameendelea kukaidi maagizo. Hadi mwezi Juni 2025 jumla ya watoa huduma zaidi ya 30 wasiokuwa na leseni walifikishwa Mahakamani… Kwa mwaka wa fedha 2024/2025 Benki Kuu ilitoa onyo kwa taasisi zaidi ya 30 na imefuta leseni moja (1) na kusitisha leseni moja,” imeeleza taarifa ya BoT.

Mwandishi: Yohani Gwangway
Mhariri: Dominic Allen

Hot this week

Mnyonge, mnyongeni ila haki yake mpeni

By Dorlingson Edward Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS), leo...

CHADEMA kutoa msimamo wake kuhusu maridhiano

By Veronica Mlyatu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetoa...

Popular Articles

Safari ya Mashimba katika kutetea jamii ya Wahadzabe

Nchini Tanzania  kuna jumla ya makabila zaidi ya 120...

Polisi waendelea kuwashikilia viongozi wa CHADEMA

Ni siku ya kwanza tangu kukamatwa kwa viongozi wa...

Siku ya Vijana Duniani.

Kwa sasa ni kijana wa miaka 25 ambaye amejiajiri...

BWAWA LA ARBA’AT  LASABABISHA MAAFA NCHINI SUDAN

Watu 30 mashariki mwa Sudan na na wengine 60...

Sand Mining in Tanzania: Trails of Destruction in Lake Victoria and its Environs

By Dominic Allen On November 14th, 2021 in the Geita...

 Utekaji: Fumbo linalotushinda?

Na Yohani Gwangway Taifa la Tanzania kwa miaka mingi limekuwa...

Abduction: Is it a riddle we can’t solve?

By Yohani Gwangway For many years Tanzania has been an...

Mustakabali wa Hewa Safi kwa kila kiumbe

Na Dominic Allen Msingi wa maisha ya viumbe hai yaani...
LAND DWELLERS FACT CHECK HUB VERIFY FACTS STOP MISINFORMATION Trusted Fact-Checking in Tanzania Beyond What You Know VERIFY NOW

Related Articles

Popular Categories

DWELLERS CHECK-HUB Verify Facts. Stop Misinformation Trusted Fact-Checking in Tanzania • Beyond What You Know VERIFY NOW