Idadi ya watahiniwa wa shule ambao wameanza kufanya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne (NECTA) mwaka 2026 imeongezeka kwa watahiniwa 74,202, sawa na asilimia 13.02, ambapo jumla ya watahiniwa 667,040 wameshaanza kufanya mtihani huo, ikilinganishwa na watahiniwa 569,883 kwa mwaka 2025.
Hayo yamebainishwa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), Profesa Said Mohamed, jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, akieleza kuwa mtihani huo utamalizika Novemba 6, 2026, katika shule za Sekondari na vituo vya watahiniwa wa kujitegemea nchini.
Kati ya watahiniwa hao, 644,085 ni watahiniwa wa shule, huku 22,955 wakiwa watahiniwa wa kujitegemea, ambapo watahiniwa wa shule, wavulana ni 297,309 na wasichana ni 346,776, huku kwa upande wa watahiniwa wa kujitegemea, wavulana ni 10,223 na wasichana ni 12,732.
Jumla ya vituo 7,067 vitatumika kwa ajili ya kufanyia mtihani huo, zikiwemo shule za sekondari 6,265 na vituo 802 vya watahiniwa wa kujitegemea. Aidha, Profesa Mohamed ametoa wito kwa jamii kutoa ushirikiano unaohitajika ili kuhakikisha mtihani huo unafanyika kwa amani na utulivu.

