Na Dominic Allen
Wananchi wa jamii ya wamaasai kutoka wilaya ya Ngorongoro, mkoani Arusha wametoa tamko kupinga ripoti za Tume mbili za Rais zilizoundwa kutathmini masuala yanayolalamikiwa na wakazi wa wilaya ya Ngorongoro pamoja na kutathmini zoezi la uhamishaji wa wakazi kutoka Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, ambapo wameeleza wasiwasi wao mkubwa juu ya hatma ya maisha yao.
Katika taarifa hiyo iliyotolewa Machi 20, 2026, wananchi hao wamesema kuwa mapendekezo ya Tume yaliyowasilishwa Machi 12, 2026 hayajaakisi uhalisia wa maisha yao wala kuzingatia maoni yao, huku zikiacha maswali muhimu bila majibu na kushindwa kutoa suluhisho la changamoto zinazowakabili.
“Tunalazimika kueleza wazi kuwa tuna wasiwasi mkubwa juu ya hatima ya maisha yetu. Kwa mtazamo wetu, ripoti hizo hazijaakisi uhalisia wa maisha yetu, hazijazingatia hata kidogo maoni yetu,” wamesema katika tamko hilo.
Jamii hiyo imeenda mbali zaidi kwa kutilia shaka uhalali na uhuru wa ripoti hizo, ya kwamba zimeegemea katika nyaraka zilizokwisha pingwa hapo awali, zikiwemo nyaraka za sera zinazodaiwa kuhalalisha kuwaondoa wafugaji wa kimaasai katika maeneo yao.

Wananchi hao wamesema maisha yao ya ufugaji si tishio kwa uhifadhi wa mazingira, kinyume na madai yanayojitokeza katika ripoti za Tume, badala yake, wanasisitiza kuwa kwa vizazi vingi wamekuwa wakishirikiana na mfumo wa ikolojia wa Serengeti na Ngorongoro kwa njia endelevu.
“Maisha yetu ya ufugaji si tishio kwa uhifadhi. Kinyume chake, maarifa yetu ya asili na mbinu zetu za usimamizi wa ardhi zimeendeleza mfumo huu wa ikolojia kwa karne nyingi,” wamefafanua.
Aidha, wametuhumu tume kwa kupuuza mchango wa shughuli za kibiashara katika kuathiri mazingira, ambapo wameeleza kuwa upanuzi wa miundombinu ya utalii kama hoteli za kifahari, barabara na msongamano wa magari ya watalii haujaangaliwa kwa uzito unaostahili.
“Tume hizi zinajaribu kuonyesha uwepo wetu kama chanzo kikuu cha shinikizo la kimazingira huku zikipuuza upanuzi wa haraka wa miundombinu ya utalii,” imeeleza sehemu ya tamko hilo.
Kuhusu suala la uhamishaji wa wananchi, jamii hiyo imesisitiza kuwa hatua zilizochukuliwa hapo awali hazikuwa za hiari, bali zilitokana na mazingira magumu yaliyowekwa kwa makusudi, ikiwa ni pamoja na kunyimwa huduma za msingi.
“Tunakiri kwamba sera za uhamishaji zilizotekelezwa katika miaka ya hivi karibuni ya Kuhamisha wananchi kutoka Tarafa ya Ngorongoro hazikuwa za hiari. Tumekuwa tukieleza mara kwa mara kwamba jamii zetu zimekumbwa na vikwazo visivyokubalika katika huduma za msingi, upatikanaji wa ardhi na miundombinu ya kijamii, hali ambayo kwa vitendo imelazimisha watu wetu kuondoka katika makazi yao kupitia kunyimwa huduma badala ya hiari,” wamesema.

Katika maeneo ya Loliondo na Sale, wananchi wamelalamikia ukosefu wa ushirikishwaji katika uanzishwaji wa Pori la Akiba la Pololeti, pamoja na uhaba mkubwa wa maeneo ya malisho, hali iliyosababisha vifo vya mifugo na hasara kubwa kiuchumi.
“Hata hivyo, Tume haijatoa majibu ya wazi kuhusu iwapo umegwaji wa ardhi ya vijiji vya Loliondo na Sale ulikuwa shirikishi kwa mujibu wa sheria,” wamesema.
Kwa mujibu wa tamko hilo, mifugo imeendelea kukamatwa ndani na nje ya eneo hilo, wakitozwa mamilioni ya fedha wengine wakitaifishwa na kuuzwa kwenye minada za wazi, na kiwaacha wananchi katika dimbwi la umaskini.
“Badala ya kushughulikia swala la msingi na kiini cha tatizo ambacho ni haki ya ardhi na ushirikishwaji, mapendekezo yamejikita zaidi katika masuala ya kiutawala kama miundombinu na usimamizi bila kupendekeza namna mgogoro wa ardhi pamoja changamoto ya mahitaji ya jamii yatakavyotatuliwa,” limeeleza tamko hilo.
Pia, wamepinga mapendekezo yanayohusu eneo la Ziwa Natron, wakisisitiza kuwa ni ardhi halali ya vijiji vilivyosajiliwa kisheria, yenye umuhimu mkubwa kiuchumi, kitamaduni na kiimani kwa jamii ya wamaasai.
Tamko hilo limeeleza kuwa Mlima Oldoinyo Lengai, uliopo katika eneo hilo, ni sehemu takatifu inayotumika kwa shughuli za kiimani na kitamaduni, hivyo maamuzi yoyote kuhusu eneo hilo yanapaswa kuzingatia haki hizo.
“Mlima Oldoinyo Lengai ni mlima mtakatifu unaotumika kwa ibada, matambiko na shughuli za kijadi. Hivyo, maamuzi yoyote yanayohusu eneo hili yanapaswa kuzingatia pia haki za kitamaduni na kiimani,” wamefafanua.
Wananchi hao wameweka wazi msimamo wao kwa kupinga vikali mapendekezo ya Tume za Rais, wakitaka serikali isiyafanyie kazi. Pia, wameeleza kuwa hawatakubali kwa namna yoyote ile uhamisho kutoka katika ardhi yao ya asili, wakisisitiza kuwa mipango ya kugeuza ardhi za vijiji kuwa Mapori ya Akiba kwa madai ya kuwa ni mapori tengefu ni kinyume na sheria na haki zao za msingi.
Aidha, wananchi hao wamesisitiza umuhimu wa ridhaa ya wananchi kuzingatiwa katika kila hatua ya maamuzi yanayohusu maisha yao. Wameeleza kuwa haki yao halali ya kubaki Ngorongoro na kuendeleza mfumo wao wa maisha ya ufugaji lazima iheshimiwe. Sambamba na hilo, wametaka ardhi ya Pololeti irejeshwe kwa jamii, huku wakitaka kukomeshwa mara moja kwa vitendo vya ukamataji wa mifugo, unyanyasaji na kukamatwa kiholela kwa wafugaji.
“Tunapinga mapendekezo ya Tume za Rais na Serikali isizifanyie kazi…Tunataka kuzingatiwa kwa ridhaa ya wananchi katika hatua zote Haki yetu halali ya kubaki Ngorongoro na vijiji vyetu kuendelea na mfumo wetu wa maisha ya ufugaji iheshimiwe,” msimamo wa jamii ya wamaasai.
Katika hatua nyingine, wameweka wazi kutokubali mabadiliko yoyote ya Sheria ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCA) yatakayohalalisha kuondolewa kwao, huku wakiitaka serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii kushughulikia vitendo vya unyanyasaji vinavyoendelea katika maeneo mbalimbali ikiwemo Pololeti, Ndutu, Oldupai/Irka, pamoja na maeneo ya Loliondo kama Lopolun na Sakala, wakidai kuwa vitendo hivyo vimeongezeka baada ya kutolewa kwa taarifa za tume.
“Sisi siyo maadui wa uhifadhi. Sisi ni walinzi wa mazingira na wanyama… Mustakabali wa mfumo wa ikolojia wa Ngorongoro na Serengeti haupatikani kwa kuwaondoa watu wa asili, unapatikana kwa kutambua na kuimarisha nafasi ya wamaasai kama walinzi wa kihistoria wa ardhi hii.” wamesema.
Wameelekeza wito wao kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Watanzania kwa ujumla pamoja na jumuiya ya kimataifa, wakitaka haki zao zitambuliwe na kuheshimiwa. Pia, wamezitaka taasisi za haki za binadamu na mashirika ya uhifadhi kushiriki katika mazungumzo ya kweli yatakayoweka mbele maslahi ya watu wa asili na kulinda mifumo ya maisha yao.
“Tunaiomba Serikali ya Tanzania, Watanzania wenzetu, jumuiya ya kimataifa, mashirika ya uhifadhi na taasisi za haki za binadamu kutambua haki zetu, kushiriki katika mazungumzo ya kweli, na kuunga mkono mifumo ya uhifadhi yanayoheshimu watu wa asili na maeneo yao,” wito wa jamii ya wamaasai.
Tangu kutolewa kwa ripoti za Tume hizo zilizowasilishwa kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan mnamo Machi 12, 2026 katika Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma, wakazi wa wilaya ya Ngorongoro, wanaharakati pamoja na watetezi wa haki za binadamu wameonesha kutoridhishwa na matokeo ya Tume hizo.
Mwandishi: Dominic Allen
Mhariri: Yohani Gwangway


