Na Dominic Allen
Watu watatu wamehukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela au kulipa faini baada ya Mahakama ya Wilaya ya Magu kuwakuta na hatia ya kumiliki mifuko ya plastiki iliyopigwa marufuku nchini pamoja na viwatilifu ambavyo havijasajiliwa.
Hukumu hiyo imetolewa katika Mahakama ya Wilaya ya Magu na Hakimu Mkazi Erick Kimaro jana Mei 23, 2025 baada ya kuwakuta na hatia Emmanuel Mayuya (40) na Fabian Philipo (50), wakazi wa Kayenze, Geita ambao wamehukumiwa kifungo cha mwaka mmoja au kulipa faini ya shilingi laki moja, huku Otiko Mbasha (52) ambaye pia ni mkazi wa Chato mkoani Geita akihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela au kulipa faini ya shilingi milioni tano.
Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Nuru Nko amesema kuwa watu hao watatu walifunguliwa kesi ya jinai Na. 27974/2024 baada ya kukamatwa Septemba 12, 2024 katika kijiji cha Kageye, Magu mkoani Geita wakiwa na mifuko ya plastiki iliyopigwa marufuku kwa mujibu wa Kanuni ya 8(c) ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira, Tangazo la Serikali Na. 394 la mwaka 2019, pamoja na viwatilifu visivyosajiliwa kinyume na Kifungu cha 14(1) na 59(1)(h)(n)(b) na (2) cha Sheria ya Afya ya Mimea ya mwaka 2020, sambamba na Kanuni ya 39(4) ya Kanuni za Afya ya Mimea ya mwaka 2023.
Mahakama ya Wilaya ya Magu pia imetoa amri ya kutaifishwa kwa injini ya boti aina ya Suzuki, mtumbwi mmoja ulikuwa ukitumiwa kwa ajili ya kusafirisha mifuko ya plastiki, vilevile imeamuru kulipwa gharama za kuteketeza mifuko hiyo na viwatilifu hivyo.
Hata hivyo washtakiwa hao walisema hawakufahamu kuwa vitendo hivyo ni makosa, hoja iliyopingwa na upande wa mashtaka.
Ikumbukwe kuwa mapema Januari, 2025 Land Dwellers pia ilifanya uchunguzi kuhusiana na matumizi ya mifuko ya plastiki iliyopigwa marufuku nchini, na kubaini kuwa bado inaendelea kuingizwa, kuzalishwa na kutumika katika maeneo mbalimbali jijini Mwanza na Tanzania kwa ujumla, licha ya Serikali ya Tanzania mwaka 2019 kupiga marufuku kuingiza, kusafirisha nje ya nchi, kutengeneza, kuuza, kutunza na kusambaza mifuko hiyo, jambo linalopelekea uchafuzi wa mazingira na kuhatarisha afya za watu.
Mwandishi: Dominic Allen
Mhariri: Yohani Gwangway


