Na Dominic Allen
Kundi la Hamas limewaachilia mateka watatu wa kike wa Israel waliyokuwa wanashikiliwa huko Gaza huku Israel ikiwaachia huru wafungwa 90 wa Kipalestina hapo jana, ikiwa ni siku ya kwanza ya kusitisha mapigano ambayo yamesimamisha vita vilivyodumu kwa takriban miezi 15 vilivyoharibu Ukanda wa Gaza na kuchochea hali ya taharuki Mashariki ya Kati.
Shangwe zilitawala huko Ramallah katika Ukingo wa Magharibi, Gaza wakati mabasi yaliyoleta wafungwa wa Kipalestina yalipowasili, ambapo maelfu ya watu walikuwa wakisubiri kuwapokea wafungwa wa Kipalestina walioachiliwa huru na Israel. Hamas wamesema kuwa walioachiliwa kutoka magereza ya Israel ni wanawake 69 na wavulana 21.
Huko Tel Aviv, mamia ya Waisrael walishangilia kwa furaha wakati wakifuatilia matangazo ya moja kwa moja kutoka Gaza yaliyoonesha mateka watatu wa kike wakiingia kwenye gari la Msalaba Mwekundu wakiwa wamezungukwa na wapiganaji wa Hamas.
Israel na Hamas wamefikia muafaka wa kusitisha mapigano huko Gaza, kupeleka misaada, na mateka 33 kati ya takriban 100 wa Israel na wa kigeni waliobaki kuachiliwa huru katika awamu ya kwanza ya wiki sita, kwa kurudisha wafungwa karibu 2,000 wa Kipalestina walioko magerezani Israel. Hata hivyo inaaminika kuwa wengi wa mateka waliokuwa wanaoshikiliwa na Kundi la Hamas wanahofiwa kuwa wameshafariki.
Makubaliano hayo ya kusitisha mapigano katika eneo la Gaza yamewaruhusu Wapalestina kurudi katika maeneo yao yaliyoharibiwa kwa mabomu, kuanza kujenga upya maisha yao, huku malori ya misaada yakileta misaada muhimu.
Mwandishi: Dominic Allen
Mhariri: Yohani Gwangway


