Na Yohani Gwangway
Mafanikio Yaliyopatikana Jul 2023– Nov 2024
Meneja Msaidizi kutoka Kurugenzi ya Masoko ya Fedha Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Dkt. Anna Lyimo amesema kuwa benki hiyo imeongeza akiba ya dhahabu fedha yenye thamani kutoka dola za kimarekani milioni 23 hadi dola za kimarekani milioni 30.32 kati ya kipindi cha mwezi Julai mwaka 2023 hadi mwezi Novemba mwaka huu, ambapo kwa sasa hivi BOT ina akiba ya dhahabu fedha kilogramu 366.55.
Dr. Lyimo amesema kuwa kwa upande mwingine akiba ya Benki Kuu ya Tanzania katika manunuzi ya dhahabu safi imefikia kilogramu 872.05 zenye thamani ya dola za kimarekani milioni 74.04. Manunuzi haya ni kutoka kwa wauzaji mbalimbali pamoja na masoko ya dhahabu nchini Tanzania ambayo yananunua dhahabu kutoka kwenye viwanda vya uchenjuaji dhahabu.

Kwa mujibu wa taarifa ya BOT mafanikio yao katika kununua dhahabu na kuweka akiba ni kutokana na jitihada mbalimbali zilizowekwa na serikali ikiwa ni pamoja na punguzo la malipo ya mrabaha kutoka 6% mpaka 4% kama inavyolipwa kwa wauzaji kwenye viwanda vya kuchenjulia dhahabu nchini. Sababu nyingine ni kununua dhahabu inayotokana na malipo ya 1/3 ya malipo ya mrabaha pamoja na dividends yanayotarajiwa kulipwa (in kind) kwa mujibu wa sheria.
Kwa sasa Benki Kuu ya Tanzania inapata urahisi wa kununua dhahabu zake kutoka kwa wachimbaji wakubwa pamoja na wadogo kutokana na mabadiliko na maboresho katika Sekta ya Madini kati ya mwaka 2018 na 2019.
“Mwaka 2018-2019 tunafahamu kuwa serikali ilifanya mabadiliko makubwa sana kwenye Sekta ya Madini na wakaanzisha viwanda vya kuchenjua dhahabu kwa hiyo sasa hivi dhahabu tukinunua tuna mtu ambaye anaenda kutupimia na siyo sisi tena”. Aliongeza Dkt. Lyimo.
Benki Kuu ya Tanzania imeamua kuanza kununua dhahabu kwa mara nyingine tena baada ya kile kipindi cha mwaka 1990 hadi mwaka 2003 ambapo walisitisha kutokana na changamoto mbalimbali ili kuimarisha akiba yake ya fedha za kigeni na kupunguza utegemezi Tanzania kwa mataifa ya nje.

Maamuzi ya Benki Kuu ya Tanzania kununua dhahabu kwa mara nyingine yameanza mwaka 2022 huku Dkt. Lyimo akieleza kuwa haya ni maamuzi ya busara kwa taifa letu. Mataifa mengi yameanza kununua dhahabu na kuweka kama akiba hasa baada ya mwaka 2010 ikiwa ni muda mfupi mara baada ya kutokea kwa mtikisiko wa Uchumi Duniani ulioathiri mataifa mbalimbali.
“Ina maana kuna kitu kimetokea hapa, dunia ikabadilisha mtazamo na kufanya manunuzi ya dhahabu yatoke chini na kupanda juu. Kilichotokea baada ya mtikisiko wa uchumi duniani (Global Financial Crisis) ni kuwa nchi zote duniani ziligundua kuwa ukikaa na pesa kama pesa, bado haujapona, pale ndiyo wakarudi katika manunuzi ya dhahabu”. Alifafanua Dkt. Lyimo.

Historia ya ununuzi wa dhahabu kama akiba ya fedha za kigeni imeonesha mfanano wa muda mrefu. Ripoti mbalimbali zinaonesha kuwa kila thamani ya dola ya Marekani inaposhuka, thamani ya dhahabu huimarika katika soko la dunia na wakati thamani ya dola inapopanda, dhahabu hushuka thamani. Licha ya matukio haya, Dkt. Lyimo anaeleza kuwa ununuzi wa dhahabu ndiyo njia imara ya kuwa na pesa za kigeni pamoja na kuimarisha thamani ya pesa zetu.
Benki Kuu ya Tanzania inatoa mafunzo ya siku mbili kwa waandishi wa habari takribani 36 kutoka mikoa 6 yanayolenga kuwajengea uwezo wa kuandika habari za kifedha na kiuchumi.

Faida za Benki kununua dhahabu ni kama zifuatazo;
- Kuimarisha akiba ya fedha za kigeni kwa taifa na kupunguza utegemezi wa nje.
- Kutoa kiwango cha kujiamini kuhusu hali ya kifedha.
- Kuweka soko la kuvutia kwa wasambazaji wa dhahabu wa ndani.
- Kuonesha uthabiti wa sarafu ya ndani.
- Kusaidia kukidhi mahitaji ya fedha za kigeni na deni la nje.
- Kuhifadhi akiba kwa ajili ya majanga au dharura za kitaifa.
- Kutumia rasilimali yetu ya dhahabu kwa manufaa ya kiuchumi.
Mwandishi: Yohani Gwangway
Mhariri: Dominic Allen


