Na Yohani Gwangway
Taifa la Tanzania kwa miaka mingi limekuwa mfano barani Afrika na kote duniani kutokana na utulivu na amani. Msingi ya Taifa inayotajwa katika katiba ikiwa ni Uhuru, Umoja, Udugu na Amani.
Matukio ya watu kupotea na wengine kutekwa yameanza kuharibu taswira ya Tanzania pamoja na watu wake siku za hivi karibuni. Katika maeneo mbalimbali ya Tanzania kumekuwa na matukio ya watu kupotea kwa muda, kupotea kabisa na wakati mwingine kuchukuliwa na watu wasiojulikana na kuokotwa wakiwa na majeraha au wakiwa wamepoteza maisha.
Baadhi ya watu wamekuwa wakilinyooshea mkono Jeshi la Polisi kwa kushindwa kudhibiti matukio haya na wakati mwingine kutajwa kama wahusika wa matukio haya. Hii inatokana na baadhi ya watu waliopotea kwa siku kadhaa, kukutwa kwenye mikono ya Jeshi la Polisi kwa madai kuwa walikuwa wana makosa ya aina fulani.
Maumivu ya ndugu, simanzi na masononeko yanayotokana na kutofahamu alipo mwenzao hudumu kwa miaka mingi na wengine hadi kwenda kaburini wakiwa hawajui alipo ndugu yao. Ni kwa sababu hii inayogusa mioyo yetu kama binadamu, tunahitaji kujiuliza swali moja, ni lini matukio haya yatakoma?
Ni wazi kuwa haitakuwa rahisi kutafuta jawabu la tatizo ambalo halijajajulikana chanzo chake. Hii inaturudisha nyuma na swali kubadilika kuwa nani anahusika na utekaji Tanzania? Au kwa lugha nyingine “watu wasiojulikana” ni nani hasa? Ikiwa swali la msingi ni nani yupo nyuma ya utekaji nchini Tanzania, basi ni muhimu pia kuelewa ni nani hutekwa? Hawa wanaopotea wana sifa zipi?
Mifano hii inatia simanzi, huzuni na wakati mwingine hasira. Lakini hatuna budi kuitumia ili kuweka sawa historia na kuelewa mawanda mapana ya tatizo hili.
Ni takribani miaka 6 sasa hajulikani alipo mwandishi wa habari wa Gazeti la Mwananchi, Azory Gwanda. Pia ni miaka karibu 7 tangu alipopotea Msaidizi wa Mwenyekiti Freeman Mbowe wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Ben Saanane.
Azory Gwanda ni mume, baba na mtoto kwa wazazi wake. Wazazi wake wamehangaika na maumivu ya kujua alipo mtoto wao bila mafanikio. Mke wake ambaye alisubiri mume wake kurejea siku anapotea huenda aliandaa chakula na maji ya kuoga wa ajili mume wake. Nao watoto wa Azory nao walimsubiri baba yao arejee nyumbani na kumlaki akiwa na zawadi. Ila yote haya hayakuwezekana. Na hadi leo Azory Gwanda hajaonekana.

Azory Gwanda
Kwingineko, Ben Saanane naye alikuwa ni mume na baba. Familia yake imehangaika kumtafuta kwa miaka mingi bila mafaniko. Katika matukio haya yote watanzania walibaki na maswali bila majibu.

Ben Saanane
Ni karibu kabisa na kupona nafsi zetu kwa kusahau kuwa Ben Saanane na Azory Gwanda bado hawajarejea, matukio haya yanarejea upya na kutuumiza mithili ya kidonda kilichokaribia kupona na kutoneshwa upya.
Na kwa mantiki hii tafakari yetu juu ya matukio haya ya zamani na mapya ni Je, Utekaji ni fumbo linalotushinda? Je, hatuwezi kutatua suala hili? Je, hatuwezi kujua wahusika? Je, hatuwezi kujua walipo ndugu zetu waliopotea? Na kama hatuwezi kujua, nani anatakiwa kujua zaidi ya mamlaka zilizopo kisheria?
Matukio ya watu kupotea ya hivi karibuni
Mkoani Tanga mnamo tarehe 15 Juni 2024, Kombo Mbwana alitoweka, familia yake pamoja na ndugu wa karibu kuanza kumtafuta kwa zaidi ya siku 29. Baadaye ndugu zake waliripoti kutoweka kwa ndugu yao katika kituo cha polisi.
Licha ya juhudi zote, Kombo Mbwana hakupatikana hadi baadaye ambapo Jeshi la Polisi lilijitokeza kumshikilia Kombo Mbwana tangu tarehe 9 tofauti na taarifa za ndugu. Jambo hili lilizua sintofahamu iliyopelekea ndugu kuhoji kwanini ndugu yao ashikiliwe kinyume na sheria
Hatimaye Ndugu zake walifungua kesi mahakamani kudai Kombo aachiwe huku wakidai fidia kwa tukio hilo la Kombo kushikiliwa kinyume na utaratibu. Licha ya juhudi hizi hadi tunaandika makala hii Kombo hajaachiwa huku kesho yake ikiwa haijulikani.
Tukio hili linaibua maswali juu ya mazingira ya Ukamataji yaliyotumika na polisi na endapo yanazingatia Kanuni za Polisi (Police General Order-PGO) pamoja na taratibu za ukamataji (arresting procedures).
Sura ya 272 Kifungu cha 7 (a) ya Kanuni za Polisi inayozungumzia Ukamataji na Upekuzi inamtaka afisa wa polisi kumweleza mtuhumiwa sababu ya kukamatwa kwake.
Sheria na Kanuni hizo zinamtaka askari polisi kujitambulisha na kueleza kosa alilofanya mtuhumiwa.
Ukiachana na tukio la Kombo, Edgar Mwakalebela (maarufu kama Sativa) ambaye ni mkazi wa Dar es salaam naye alitoweka katika mazingira ya kutatanisha. Kwa mujibu wake, Edgar alieleza kuwa alitekwa na watu wasiojulikana na baadaye kupelekwa katika kituo cha Polisi Oysterbay. Hii ni baada ya kupatikana
Simulizi ya Edgar inaeleza kuwa waliomkamata walimtoa Oysterbay na baadaye kupelekwa mkoa wa Arusha. Hapo ndipo safari ilipopadilika na kuelekea Katavi ambapo Edgar alipatikana akiwa amepigwa risasi ya kichwa iliyotokea katika taya zake ni kumsababishia madhara makubwa. Tukio hili lilizuia hisia tofauti hasa katika mitandao ya kijamii huku wengi wakichukizwa na kilichotokea.
Baada ya Edgar (Sativa) kupatikana alipatiwa matibabu ambapo Rais wa Jamahuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alichangia kiasi cha pesa milioni 35 kusaidia matibabu yake.
Licha ya Edgar kupata nafuu na kurudi nyumbani lakini hadi leo hakuna uchunguzi ulioweka wazi wahusika wa utekaji huu . Pia Jeshi la Polisi halijachukua hatua kwa madai ya Edgar kuwa alichukuliwa katika kituo cha polisi cha Oysterbay.

Kombo Mbwana

Edgar Mwakalebela (Sativa)
Edgar na Kombo siyo mwisho wa simulizi hizi za kutisha za utekaji nchini Tanzania kwani mwezi Agosti mwaka huu Deusdedith Soka ambaye ni mwenyekiti wa Baraza la Vijana la CHADEMA (BAVICHA) Temeke kuchukuliwa na watu waliodhani kuwa ni polisi. Soka alichukuliwa akiwa na wenzake wawili Frank Mbise na Jacob Mlay.


Frank Mbise
Siku 5 baadaye Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa, Freeman Mbowe aliitisha mkutano na waandishi wa habari. Katika mkutano huu Mbowe alieleza kuwa wamepata taarifa za ukweli kutoka vyanzo vyao kuwa Jeshi la Polisi kituo cha Chang’ombe ndiyo waliomkamata Soka na wenzake.
Mbowe alieleza kuwa askari mmoja wa kituo hicho alimpigia Soka aende kituo cha polisi ili achukue pikipiki yake ambayo ilikuwa inashikiliwa na Polisi. Taarifa hiyo ilieleza Soka aliwapitia marafiki zake Mbise na Mlay kwenda kituo cha polisi na baada ya hapo hawakuonekana tena.
Sifa za watu wanaopotea/kutekwa
Katika matukio mengi ya zamani na yanayoendelea sasa, wengi wa watu wanaopotea au kutekewa wanaonekana kuwa ni wanaharakati hasa wengi wao wakitoka vyama vya upinzani. Baadhi yao ni wakosoaji wa mifumo iliyopo na wanaohitaji kuleta mabadiliko wakiwemo wafanyabiashara wa kawaida.
Jambo hili linazua maswali juu ya usalama wa wakosoaji wa serikali na mifumo ya nchi. Je, wakosoaji wako salama kiasi gani? Ni lini kutakuwa na uhakika wa kuona mitazamo tofauti kuwa siyo uadui? Kama Taifa tunahitaji mjadala kuhusu hili na pengine kuangalia suala hili kwa mustakabali ya taifa letu.
Msimamo wa Bunge
Mjadala juu ya utekaji nchini Tanzania ulifika bungeni baada ya Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Aida Khenani (kupitia CHADEMA) kupendekeza hoja ya dharura katika Bunge la Tanzania, katika mazingira ambayo hayakutegemewa, Spika wa Bunge Dkt. Tulia Ackson aliikataa hoja hiyo kwa madai kuwa yeye hana taarifa juu ya matukio hayo ya utekaji. Msimamo wa Dkt. Tulia Ackson ni msimamo uliopokelewa kwa namna tofauti huku akipata ukosoaji mkubwa kutoka watetezi wa haki za binadamu.
Baadhi ya maswali muhimu kwa Dkt. Tulia Ackson, ni kwanini aliamua kukataa hoja iliyotokana na mbunge ambaye ni mwakilishi wa wananchi? Je, madai ya Spika kuwa hana taarifa za matukio hayo inatosha hoja hiyo kutojadiliwa licha ya vilio kutoka kona mbalimbali? Je, kunaweza kukawa na mambo muhimu kiasi gani katika bunge kiasi cha kushindwa kujadili masuala ya usalama wa watu?
Katika hatua nyingine wakosoaji mbalimbali kupitia mitandao ya kijamii walisema kauli ya Spika kuwa hoja hiyo haikufuata utaratibu wa bunge na ililetwa kimihemko, ni kauli inayovunja moyo hasa kwa familia zilizopotelewa na ndugu zao.
Msimamo huu wa bunge, ulionesha wazi nia ya bunge hilo kupitia kiongozi wake Dr. Tulia Ackson kutojali kelele, vilio na maumivu ya wahanga wa utekaji nchini Tanzania. Katika taifa linalojali misingi yake ikiwa ni pamoja na tunu za taifa, huenda msimamo huu ungeegemea upande wa vilio vinavyonyima usingizi baadhi ya wananchi wa Tanzania.
Msimamo wa Mahakama
Baada ya kupotea kwa baadhi ya vijana ambao ni viongozi wa CHADEMA, akiwemo Deusdedith Soka, Wakili Paul Kisabo alifungua kesi dhidi IGP, DZPC, ZCO OCCID Temeke na OCS. Kesi hii ilifunguliwa Mahakama Kuu Tanzania Kanda ya Dar es salaam. Maamuzi ya kesi hiyo iliyofunguliwa kwa hati ya dharura mbele ya Jaji Wilfred Dyansobera yalileta majonzi zaidi baada ya Jaji kusema kuwa hakuna ushahidi unaojitosheleza kuwa Soka na wenzake wanashikiliwa na Jeshi la Polisi.
Maamuzi haya yalitaka wale walioshtakiwa kufanya uchunguzi na kujua walipo Soka na wenzake. Ndugu waliofika mahakamani waliangua vilio kutokana na hukumu hii. Maamuzi haya yanaweka maswali mengine juu ya utendaji wa Mahakama hasa pale suala la dharura linapofika mezani kwake.
Msimamo wa Jeshi la Polisi
Kwa nyakati kadhaa Jeshi la Polisi nchini Tanzania limekuwa likituhumiwa kwa baadhi ya matukio ya utekaji wa raia hasa wakosoaji wa serikali. Kwa upande wao Jeshi la Polisi kwa mara kadhaa limekanusha kuhusika na madai ya utekaji kwa kueleza kuwa Jeshi la Polisi linazingatia maadili katika kufanya kazi zake.
Msimamo huo wa Jeshi la Polisi unalipeleka taifa katika mjadala muhimu wa kujua, je, kuna usalama kiasi gani kama watekaji hawa hawajulikani na walipotea hawawezi kutafutwa na Jeshi la Polisi?
Kwa mujibu wa sheria iliyoanzisha Jeshi la Polisi yaani The Police Force and Auxiliary Service Act ya mwaka 1939 kazi ya Jeshi la Polisi ni kulinda raia na mali zake. Baadhi ya wakosoaji wanadai haitoshi kwa Jeshi la Polisi kudai kuwa halihusiki na utekaji, bali lilitakiwa kuja na majibu ya nani anahusika na matukio hayo.
Kitendo cha Jeshi la Polisi kutokuwa na majibu, kunaweka alama ya kuuliza juu ya wajibu wao kikatiba wa kulinda raia na mali zao. Zaidi ya haya tafsiri ya baadhi ya raia ni kuwa huenda wasiwe salama pale ambapo wakiitwa na mtu yeyote na pia hakuna chombo kinaweza kuwatetea.
Hitimisho hili linatokana na msimamo wa Bunge, Mahakama na majibu ya Jeshi la Polisi juu ya maswahibu ya utekaji na watu kupotea katika baadhi ya maeneo hapa nchini.
Je, tunahitaji chombo huru cha uchunguzi?
Kutokana na matukio yanayoendelea na mengine ambayo huhusisha Jeshi la Polisi kama taifa tunahitaji kukaa pamoja na kuangalia namna ya kutengeneza chombo huru kinachochunguza baadhi ya matukio hapa Tanzania. Matukio mengi huchunguzwa na Jeshi la Polisi licha ya wao wenyewe kutuhumiwa.
Kanuni ya Haki za Asili yaani The Principle of Natural Justice inakataa dhana ya mtuhimiwa kujichunguza mwenyewe. Hata kama siyo kweli kuwa Jeshi la Polisi linahusika, ni muhimu sana kuwa na chombo nje ya Jeshi la Polisi litakalochunguza siyo tu matukio ya utekaji na kupotea kwa watu, bali hata matukio mengine ambayo yanahitaji wachunguzi huru nje ya Jeshi la Polisi.
Kwa mfano, nchi ya Kenya ilipitia changamoto kadhaa miaka ya nyuma hadi mwaka 2011 walipoanzisha Mamlaka huru ya kuchunguza Jeshi la Polisi inayoitwa Independent Policing Oversight Authority (IPOA). Baada ya kuanzishwa kwake, IPOA ilipewa mamlaka ya kuchunguza uhalifu unaofanywa na Jeshi la Polisi. Mamlaka hii ilianzishwa kutokana na matukio ya huko nyuma ambapo Jeshi la Polisi lilitumia nguvu dhidhi ya raia lakini lilijichunguza lenyewe na hivyo kuonesha mazingira ya kutokutoa haki.
Madhara ya kunyamaziwa kwa matukio haya
Kutokana na uhalisia kuwa kuna matukio yanatokea hata kama hatujui wahusika, kunaweza kusababisha wananchi kuishi kwa hofu na kutojiamini. Wananchi wanapoona hakuna majibu kutoka serikalini kupitia vyombo vyake, mwisho wake ni wananchi kujichukulia sheria mkononi kutokana na matukio haya. Yafuatayo ni baadhi ya madhara yanayoweza kutokea katika jamii.
Madhara ya matukio haya yanaweza kuharibu uchumi wa familia ambazo zimepoteza nguvu kazi na watu waliokuwa tegemeo katika familia. Hali hii ya watu kupotea isipodhibitiwa uchumi wa familia moja moja utaanguka na kuleta matatizo makubwa kama kushindwa kusomesha watoto na kushindwa kupata huduma za msingi kutegemeana na aliyepotea au kutekwa. Na kwa msingi huu, serikali kupitia mamalaka zake inatakiwa kuhahakikisha inakomesha matukio haya.
Kwingineko kijamii jambo hili linaathiri familia zilizopoteza wapendwa wao kisaikolojia. Kitendo cha mama, watoto au baba kutojua ndugu yao alipo kinasababisha huzuni ya muda mrefu ambayo inaweza kuleta hata sonona kwa wahusika. Katika taifa lolote ustawi wa watu ni jukumu la kwanza la serikali. Hivyo basi ni jukumu la serikali ya Tanzania kuangalia ustawi wa watu wake kwa kukomesha matukio haya ili kuwapa furaha na amani wananchi wake.
Hitimisho
Majibu ya maswali katika makala hii yanaweza kupatikana kwa kurejea katika miongozo ya nchi hii kama Katiba, Sheria, Tunu na Tamaduni zetu. Ni kwa msingi huu taifa letu linatakiwa kurejea katika misingi yake na imani yake. Mwelekeo wa matukio yetu yanahitaji kuonesha Tanzania yenye kesho iliyo bora.
Tanzania inaamini katika baadhi ya tunu za Taifa (National Values) ambazo ni Utu, Uzalendo, Uadilifu, Umoja, Uwazi, Uwajibikaji na Lugha ya Taifa. Tunu hizi ni misingi ambayo taifa linasimamia na kila matendo au maamuzi yetu lazima yaakisi Tunu ambazo kama taifa tulikubali kuziishi.
Taifa linalojali utu, kama ilivyo tunu yetu, linahitaji kupambana na matendo yote maovu dhidi ya watu wake yakiwemo ya kupotea na kutekwa ambayo hayatoi tafsiri nzuri. Ni jukumu la wananchi wa Tanzania, pamoja na serikali kuhakikisha kuwa tunu za taifa zinalindwa na kila maamuzi ama matendo yanayofanyika yanaakisi tunu ambazo tunaziamini.
Mwandishi: Yohani Gwangway
Mhariri: Dominic Allen

