UYAM yaandika barua ya wazi kwa Rais Samia, ukosefu wa ajira kwa vijana nchini

BARUA YA WAZI KWA RAIS DOKTA SAMIA SULUHU HASSAN KUTOKA KWA UMOJA WA VIJANA WASIO NA AJIRA NCHINI TANZANIA

Mhe. Rais tunakusalimu kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Sisi ni Umoja wa Vijana tusio na Ajira ambao wengi wetu tupo mtaani tangu mwaka 2015. Lengo la barua hii ni kuomba serikali yako unayoiongoza kulivalia njuga na kulitafutia ufumbuzi suala la ukosefu wa ajira katika nchi yetu.

Mhe. Rais, Umojawa Mataifa unamtambua kijana kuwa ni mtu kuanzia umri wa miaka 15-24, Umoja wa Afrika ni miaka 15-35 na Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana ya mwaka 2007, inamtambua kijana kuanzia miaka 15-35. Lakini umoja wetu utawambua mpaka wenye miaka 44 kutokana na muda uliopotea katika kutafuta ajira.

Mhe. Rais, kwa mujibu wa Sensa ya Taifa ya mwaka 2022, vijana wanaoanzia umri wa miaka 15 hadi 35 ni 21,312,411 sawa na asilimia 34.5 ya idadi ya watu wote.

Kwa lugha rahisi hii ni sawa na kusema kuwa kila kundi la watu watatu nchini Tanzania, basi mmoja wao ni kijana aliye na umri kati ya miaka 15 hadi 35. Mhe. Rais, takwimu hizi zinadhihirisha kwamba, vijana ni nguvu kazi na rasilimaliwatu inayoweza kutumika kuleta mabadiliko chanya ya kisiasa, kijamii, na kiuchumi Tanzania.

Mhe. Rais, historia ya vijana kuleta mabadiliko katika taifa letu ni ya muda mrefu ikianza na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye akiwa na miaka 31 aliteuliwa kuwa Rais wa TAA baadaye TANU; Mwalimu Nyerere licha ya kuwa kijana aliendeleza juhudi za Taifa letu kupata uhuru hadi tulipopata uhuru kamili mwaka 1961.

Kwa heshima na taadhima, hata wewe Mh. Rais ukiwa miaka 20 ulianza kufanya kazi kwenye ofisi ya Mpango wa Maendeleo Zanzibar. Ushahidiwa wazi ni kuwa ulianza kutumikia taifa letu ungali bado kijana na sasa unaliongoza taifa.

Mhe. Rais, mifano hii miwili ya Baba wa Taifa hayati Mwalimu Nyerere na wewe Rais wetu inaonesha umuhimu wa kijana kuwajibika lakini pia kuaminiwa katika kusimamia mwelekeo wa taifa letu katika nyanja mbalimbali.

Mhe Rais, Sisi Vijana wa “Unemployed Youth Allied Movement” UYAM-Tanzania, tumekuandikia kwa lengo la kukubaliana na tafsiri ya Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa mwaka 2007, Toleo la mwaka 2024, kuwa ukosefu wa ajira ni hali ya mtu kukosa kazi kabisa. Inaweza kuonekana kama hali ya kukaa bure kwa kulazimika, watu wenye uwezekano wa kuzalisha kipato au kujiajiri ambao wana uwezo na wanataka kufanya kazi, lakini wameshindwa kupata kazi.

Ukubwa wa tatizo la ajira

Mhe. Rais, tatizo la ukosefu wa ajira nchini Tanzania lioneonekana kuwa kubwa kutokana na kuongezeka kwa wasomi katika taaluma mbalimbali. Kwa mfano, taarifa rasmi ya Taasisi ya Vyuo Vikuu nchini Tanzania, Tanzania Commission for Universities (TCU) ni kuwa kuna ongezeko la udahili wa wanafunzi wa masomo ya ngazi ya shahada kuanzia wanafunzi 65, 302 mwaka 2018hadi wanafunzi 133,617 mwaka 2024. Huu ni ushahidi wa ongezeko la watu ambao wakimaliza masomo yao wanaingia katika soko la ajira katika fani mbalimbali kila mwaka.

Mhe. Rais, kwa takwimu hizi ni kuwa kila mwaka takriban vijana 100,000 wanaingia katika soko la ajira nchini Tanzania. Vijana hawa wanahitaji kupata ajira serikalini, kwenye sekta binafsi au wao wenyewe kujiajiri katika sekta mbalimbali.

Wakati haya yanaendelea, kuna ongezeko la Udahili kwa shule za msingi pamoja na sekondari hapa nchini Tanzania. Ongezeko hili maana yake ni kuwa kutakuwa na ongezeko la uhitaji wa ajira hapa nchini.

Mhe. Rais, kuna sekta muhimu katika nchi yetu inahitaji wasomi hawa. Kwa mfano, hotuba ya aliyekuwa waziri wa Afya Ummy Mwalimu ya Makadirio ya Mapato na matumizi ya Fedha ya Wizara ya afya 2024/2025, inaonesha kuwa hadi kufikia mwezi Machi mwaka 2024 Sekta ya Afya ilikuwa na watumishi 126,925 huku mahitaji halisi yakiwa ni watumishi 348,923.

Hotuba hiyo ilieleza kuwa kwaSekta ya Afya pekee tuna upungufu wa asilimia 64 wa watumishi wa afya.

Mhe. Rais ipo mifano mingi ya sekta zinahitaji wataalam. Kwa heshima tunaleta kwako hotuba ya Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2022/2023 ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, ilieleza kuwa hadi kufikia 2026 kuna makadirio ya wanafunzi 23,600,000 wa shule za awali, msingi na sekondari hapa nchini.

Hotuba hii ilieleza kuwa mahitaji ya walimu katika shule hizo yatakuwa ni walimu 724,000

Mhe. Rais, ukiachana na sekta hizi tulizotaja bado kuna wahitimu katika sekta ya Ugavi, mawasiliano ya Umma, Uhusiano kwa Umma, Uhasibu, Uhandisi, sayansi ya jamii, rasilimali watu, Uchumi, Sheria na taaluma zingine ambao wanahitimu kwa maelfu hapa nchini. Wote hawa wanahitaji ajira serikalini, kwenye sekta binafsi au kujiajiri.

Mhe. Rais Umoja wa Vijana Wasio na Ajira hapa nchini, unaamini ni wakati sasa wa serikali kukaa chini na kuangalia upya namna ya kutengeneza ajira kwa vijana hawa, kuwawezesha kwa mitaji ili kuhakikisha kuwa vijana hawa wanalitumikia Taifa lao katika umri ambao wana nguvu ya kuzalisha.

Hali ya vijana kwa sasa

Mhe. Rais, kwa sasa vijana wengi wamekosa mwelekeo baada ya kuhitimu masomo yao. Kutokana na ufinyu wa ajira za moja kwa moja vijana baadhi waliotaka kujiajiri katika sekta mbalimbali wameshindwa kufanya hivyo kutokana na ukosefu wa ajira. Miongoni mwetu sasa wapo vijana wanasukuma matoroli huku wakiwa ni wataalamu wa afya, kati yetu wapo wanaoishi kwa michezo ya kubahatisha yaani betting huku wakiwa ni walimu bora.

Mhe. Rais ni kweli vijana wa Tanzania tunapenda kufanya kazi halali iwe ya kutumia akili ama kutumia nguvu. Licha ya hilo, Mhe. Rais sisi tunaona siyo sawa kwa kijana aliyesoma kwa takriban miaka 17 huku familia ikiuza vitu ili kumsomesha baadaye aishi kwa kusukuma toroli. Hii ni kutokana na ukweli kuwa haihitaji mtu kusoma miaka 17 ili aje kuwa msukuma toroli. Hela iliyotumika kumsomesha huku wazazi wengine wakiuza ardhi yao ili huyo kijana aje kuwa msaada haiwezi kurudishwa kwa kusukuma toroli.

Kwa heshima na taadhima tunakuomba Mhe. Rais pamoja na serikali yako mpitie upya hata dhana ya kijana kujiajiri. Kwa mfano, kuna wataalamu wa afya ambao wamejiajiri kwa kuuza nyanya huku takwimu zikionesha kuwa kuna uhaba wa wataalamu wa afya zaidi ya 150,000 hapa nchini. Ni kweli kuwa vijana wanatakiwa kujiajiri lakini kitendo cha kuwa na uhaba wa wataalamu wa afya huku wasomi hao wakiuza nyanya ni ushahidi wa matumizi mabaya ya rasilimali watu.

Mhe. Rais, ni imani yetu kuwa siyo lazima kijana kupoteza miaka 17 akisomea udaktari ili aje kuwa muuza nyanya. Hapa vijana tunaomba serikali iangalie upya dhana ya vijana kujiajiri.

Changamoto za vijana kujiajiri

Kukosa mitaji

Mhe. Rais, vijana wengi hapa nchini wanahitaji kujiajiri lakini wanakosa mitaji katika maeneo husika. Kwa mfano, vijana ambao wanaenda katika taasisi za mabenki ili kupata mikopo wanatakiwa kuweka hati ya nyumba, kadi ya gari au hati ya kiwanja kama kigezo cha kupewa mikopo. Jambo hili linafanya vijana kushindwa kupata mikopo hiyo. Kwa hali halisi ilivyo, ni jambo la kushangaza kuamini kuwa kijana aliyehitimu anaweza kuweka hati ya nyumba, kadi ya gari au hati ya kiwanja wakati ndiyo kwanza anahitimu na hana mali ya aina yoyote. Hili nilinalohitajika kuangaliwa upya ili vijana wa taifa hili waweze kupata mitaji

Kukosekana kwa ushirikishwaji wa vijana

Mhe. Rais, licha ya juhudi za serikali katika mambo mbalimbali ya vijana, bado kuna changamoto katika ushirikishwaji wa vijana katika mambo yanayowahusu. Kwa mfano, unaweza kuona mijadala na makongamano yanayofanya maamuzi ya hatma ya vijana, lakini wanaohusika kusimamia pamoja na kutoa maoni ni watu ambao siyo vijana. Hii inawafanya vijana kubaki nyuma kwenye ushiriki wa mambo yanayowahusu.

Miaka takriban 10 kulidhamiriwa kuanzishwa kwa Baraza la Vijana la Taifa. Baraza hili lilitakiwa kuanzishwa ili kusimamia ajenda za vijana pamoja na kuleta morali ya vijana kushirika katika maendeleo ya Taifa lao. Baraza la vijana hadi leo bado halijiaanzishwa. Mhe. Rais, kutokuanzishwa kwa baraza hili ambalo lilitakiwa kuwa sauti kwa vijana kunarudisha nyuma ushiriki wa vijana katika masuala ya msingi ya Taifa lao.

Elimu kutoendana na uhalisia wa maisha ya mtaani

Mhe. Rais hivi karibuni serikali yako imefanya marekebisho ya Sera ya Elimu. Kwanza tunakupongeza kwa marekebisho haya ya sera. Kijana mtanzania anaonekana kusoma mambo yasiyo na uhalisia na yasiyo na msaada katika kumudu mazingira yake. Kwa mfano, wanafunzi wa shule ya msingi wanafundishwa idadi ya miguu ya panzi, lakini baadaye wanakutana na changamoto halisi kama kukosa mitaji, mabadiliko ya tabia ya nchi, kukosa soko au namna ya kulima zao fulani kwa ajili ya kupata kipato. Katika mazingira kama haya idadi ya miguu ya panzi inakuwa haina msaada kwa kijana aliyekosa mtaji, soko au anayehitaji kuzalisha zao la aina fulani ili kujipatia kipato.

Jambo hili linasababisha kijana kufundishwa mambo mengi ambayokwa kiasi kikubwa hayasaidii kutatua changamoto hali za maisha yake. Hivyo basi, tunaiomba serikali yako iangalie mambo ya msingi ambayo yatamfaa kijana kufundishwa ili aweze kujitegemea kiuchumi na kuwa na mchango kwa taifa.

Kukosa elimu ya kidijitali

Mhe. Rais, mabadiliko ya sayansi na teknolojia yanafanya kubadilika kwa mahitaji ya soko la ajira, uchumi wa dunia sasa hivi unahamia katika ujuzi wa kutumia TEHAMA katika kuleta maendeleo. Kwa mfano, tajiri namba moja duniani Elon Musk anafanya uwekezaji mkubwa kwenye soko la uchumi wa kidijitali. Tajiri namba nne duniani Jeff Bezos yeye amewekeza kwenye Amazon ambayo ni platform ya kidijitali. Bilionea wa China Jack Ma ni mwanzislishi na mmiliki wa Alibaba.

Mhe. Rais, mifano hii inatuonesha kuwa kama taifa tunahitaji kuzalisha wasomi wanaoweza kuendana na uchumi wa kidijitali huku wakijiajiri katika maeneo tofauti. Serikali pia inatakiwa iangalie maendeleo ya teknoljia ikiwemo biashara za mitandaoni kama fursa za vijana wake na siyo kama tishio.

Mhe. Rais Sera ya Taifa Maendeleo ya Vijana ya Mwaka 2007, Toleo la mwaka 2024 imekiri kuwa vijana nchini Tanzania hawajandaliwa ipasavyo kutumia fursa na kunufaika na mapinduzi ya kidijitali.

Hivyo basi, vijana wapatiwe ujuzi na maarifa ya kutosha kupitia programu mbalimbali ambazo zitakuwa ni endelevu kuhusiana na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), lengo ni kuwa na kundi la vijana ambalo linatambua matumizi sahihi ya TEHAMA katika safari hii ya kuondokana na tatizo la ajira kwa vijana hapa nchini.

Kuanzishwa kwa miradi ya vijana ambayo hukosa ufanisi na ambayo huishia njiani

Mhe. Rais, tumeona juhudi za serikali yako pamoja na serikali zilizopita katika kulipunguza tatizo la ajira kwa vijana. Juhudi hizo zinaonesha kutoa mwanga kwa vijana. Lakini tumeona miradi hiyo ikiwa siyo endelevu na ambayo huanzishwa kwa matumaini makubwa lakini baadaye huishia njiani. Kwa mfano, mradi wa Building Better Tommorow (BBT) uliokuwa chini ya Wizara ya Kilimo ulianza ukiwa na lengo la kutoa fursa za vijana kujiajiri katika kilimo. Hadi sasa mradi huu unasuasua.

Mwaka 2024, Kaimu Mratibu wa Taifa wa mradi wa BBT, Michael Nyanga alisema kuwa lengo la mradi huo ni kuajiri vijana 3,000,000 katika Sekta ya Kilimo kufikia mwaka 2030.

Mhe. Rais, ahadi hii inaonekana haina uhalisia. Ili kufikia ahadi hii maana yake ni kuwa serikali inatakiwa kuajiri wastani vijana 500,000 kila mwaka. Ukweli unaoumiza ni kuwa mradi huu umeshindwa kuajiri hata zaidi ya vijana 3000 tangu kuanza kwake. Hivyo basi, Umoja wa Vijana wasio na Ajira unaitaka serikali iangalie upya mradi huu na miradi mingine inayofafanana na mradi huu ili iweze kuleta tija katika Taifa.

Mapendekezo yetu Vijana

a. Kuwezeshwa kwa upatikanaji wa mitaji

    Mhe. Rais, Umoja wa Vijana wasio na ajira, unapendekeza serikali kuhakikisha kuwa vijana wanapata mikopo yenye riba nafuu ili kupata mitaji katika shughuli wanayochagua kuifanya. Serikali ina wajibu na jukumu la kusaidia ustawi wa vijana ambao wengi wetu tunakosa mitaji ya kufanya biashara au kujihusisha na shughuli kama kilimo na ufugaji.

    Mhe. Rais,  Ibara ya 6 ya Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiuchumi, Kijamii na Kiutamaduni ambao Tanzania umesaini, unataka nchi mwanachama kutambua haki za kufanya kaziambayo inajumuisha haki ya kila mtu kuwa na fursa ya kipato kwa kufanya kazi ambayo ameichagua mwenyewe na kuiridhia na itapaswa kuilinda haki hii. Sisi vijana tunaomba serikali itulinde kwa kutupa mitaji. Hii inawezekana ikiwa serikali itashirikiana na taasisi za kibenki katika mradi maalum wa kusaidia vijana.

    b. Usimamizi mzuri waSera ya Taifa Maendeleo ya Vijana ya mwaka 2007

    Mhe. Rais tunatambua kuwa katika Sera ya Taifa Maendeleo ya Vijana ya Mwaka 2007, Toleo la mwaka 2024, imekiri kuwepo kwa tatizo la ajira kwa vijana nchini, na katika kutatua tatizo hilo, Sera imeeleza kuwa itaweka na kuhakikisha mazingira wezeshi ya kiuchumi ili kuvutia uwekezaji wa ndani na nje ya nchi katika maeneo yenye fursa za kutoa ajira; Kwa mfano viwanda vya kutengeneza bidhaa, kuimarisha mazingira wezeshi, kukuza na kuvutia sekta binafsi na wadau wengine wa ajira, kuelekeza uwekezaji kwenye sekta zenye kuajiri watu wengi pamoja na kuongeza upatikanaji wa elimu na mafunzo ya amali, kukuza ujasiriamali na kujiajiri na vile vile na kuimarisha uhusiano kati ya waajiri, wanaotafuta ajirana taasisi za mafunzo.

    Mhe. Rais ili kufikia malengo hayo, tunatoa wito kwa serikali na mamlaka zake zote zinazohusika na utekelezaji wa sera kusimamia ipasavyo ili kuondokana na tatizo la ukosefu wa ajira ambalo limekuwa mwiba kwetu sisi vijana.

    c. Kuwa na mfumo wa Elimu unaowezesha vijana kujitegemea

    Mhe. Rais kwa mujibu wa Sera ya Taifa Maendeleo ya Vijana ya Mwaka 2007, Toleo la mwaka 2024, inakadiriwa kuwa takribani vijana 1,000,000 huingia sokoni kila mwaka, huku 200,000 tu wakifanikiwa kupata ajira na 800,000 hawana uhakika wa ajira rasmi.

    Kwa takwimu hizo, tunatoa rai kwa serikali, taasisi za elimu pamoja na wadau mbalimbali wa elimu hapa nchini kupitia upya mfumo wetu wa elimu ili kutengeneza zao la wasomi na vijana ambao litakuwa na uwezo wa kutegemea kulingana na mafunzo na fani ambazo wamesomea.

    Mhe. Rais kwa kutengeneza mfumo wa elimu utakaowawezesha vijana kujitegemea utabadilisha mitazamo ya vijana kuacha kuweka tegemezi lao moja kwa moja kupata ajira serikalini na badala yake watakuwa na uwezo wa kutumia ujuzi waliopata kutoka shuleni na vyuoni kujikwamua kiuchumi.

    d. Serikali kupunguza matumzi yake ili kuweza kuajiri

    Mhe. Rais kutokana na uhalisia kuwa kuna vijana ambao wapo mtaani kwa muda mrefu, na kwakuwa kuna uhitaji wa wataalamu mbalimbali hapa nchini, tunaishauri serikali ipunguze matumzi yake. Kwa mfano, Umoja wavijana tusio na ajira tunaona kuwa siyo busara kumlipa mbunge shilingi 600,000 kwa siku kamaposho ya kuhudhuria Kikao cha Bunge, halafu kuna mwalimu amekosa nafasi ya kazi kwa takriban miaka 10.

    Mheshimiwa Rais sisi vijana tunaona kuwa uhitaji wa zaidi ya watumishi 150,000 wa madaktari auwalimu 271,028 unatakiwa kuwa kipaumbele cha serikali kuliko kulipa shilingi 600,000 kwa mtu mmoja kwa kukaa tu na kufanya wajibu ambao ni wake.

    Mhe.Rais, suala la kupunguza matumzi ya serikali siyo jipya kufanyika kwani hata mwaka 2017 serikali ya Kenya ilifanya maamuzi kama haya. Tunaomba serikali yako ipokee maoni haya kwa namna chanya ya kusaidia nguvu kazi ya taifa hili ambao baadhi yao wamesota mtaani kwa miaka 10.

    e. Kuwe na Hub (Vituo) maalum za fani tofauti tofauti

    Mhe. Rais, tuna imani kuwa kama serikali italibeba jukumu hili la kuanzisha vituo maalum (Hub) za fani tofauti tofauti kwa ajili ya vijana katika maeneo mbalimbali hapa nchini, itakuwa ni fursa kwetu sisi vijana kukutana, kujifunza, kubadilishana ujuzi miongoni mwetu pamoja na kupata na kujenga mawazo mapya ambayo yataleta matunda chanya ikiwemo kuwajengea uwezo wa kuwa wabunifu na kujiajiri.

    Mhe. Rais Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana ya mwaka 2007 imeeleza kuwa ili kuondokana na tatizo la ajira nchini, Sera imelenga kukuza ujasiriaamali na kuwajengea vijana uwezo kujiajiri, kwa mantiki hiyo tunaamini kuwa kupitia vituo hivi maalum vya fani tofauti tofauti, itakuwa ni mwanzo mzuri kufikia malengo hayo.

    Tunapohitimisha barua hii ya wazi kwako tunaomba utambue kuwa sisi vijana wa UYAM ni vijana tusiokuwa na ajira Tanzania ambao hatuna shinikizo lolote la kisiasa, mapenzi, wala ushabiki na upande wowote ambao hauendani na adhima yetu ya kudai haki yetu ya ajira na mazingira yake.

    Mwisho tukutakie mahukumu mema na utekelezaji mwema, Mungu ibariki Afrika, Mungu ibariki Tanzania, Mungu wabariki vijana wote

    Ajira yetu, Utulivu wetu

    Imeandaliwa na Umoja wa Vijana wasikuwa na ajira Tanzania
    “Unemployed Youth Allied Movement”- UYAM TANZANIA
    Machi 02, 2025

    Hot this week

    Mnyonge, mnyongeni ila haki yake mpeni

    By Dorlingson Edward Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS), leo...

    CHADEMA kutoa msimamo wake kuhusu maridhiano

    By Veronica Mlyatu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetoa...

    Popular Articles

    Safari ya Mashimba katika kutetea jamii ya Wahadzabe

    Nchini Tanzania  kuna jumla ya makabila zaidi ya 120...

    Polisi waendelea kuwashikilia viongozi wa CHADEMA

    Ni siku ya kwanza tangu kukamatwa kwa viongozi wa...

    Siku ya Vijana Duniani.

    Kwa sasa ni kijana wa miaka 25 ambaye amejiajiri...

    BWAWA LA ARBA’AT  LASABABISHA MAAFA NCHINI SUDAN

    Watu 30 mashariki mwa Sudan na na wengine 60...

    Sand Mining in Tanzania: Trails of Destruction in Lake Victoria and its Environs

    By Dominic Allen On November 14th, 2021 in the Geita...

     Utekaji: Fumbo linalotushinda?

    Na Yohani Gwangway Taifa la Tanzania kwa miaka mingi limekuwa...

    Abduction: Is it a riddle we can’t solve?

    By Yohani Gwangway For many years Tanzania has been an...

    Mustakabali wa Hewa Safi kwa kila kiumbe

    Na Dominic Allen Msingi wa maisha ya viumbe hai yaani...
    LAND DWELLERS FACT CHECK HUB VERIFY FACTS STOP MISINFORMATION Trusted Fact-Checking in Tanzania Beyond What You Know VERIFY NOW

    Related Articles

    Popular Categories

    DWELLERS CHECK-HUB Verify Facts. Stop Misinformation Trusted Fact-Checking in Tanzania • Beyond What You Know VERIFY NOW