Na Dominic Allen
Leo Aprili 09, 2026 umetimia mwaka mmoja tangu kukamatwa kwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa, Tundu Lissu alipokuwa wilayani Mbinga mkoani Ruvuma katika shughuli za kisiasa, ambapo kukamatwa kwake kulifuatiwa na kufunguliwa kwa kesi ya uchochezi pamoja na uhaini, hatua ambayo imeendelea kuzua mjadala mpana ndani na nje ya nchi kuhusu haki, siasa na utawala wa sheria nchini Tanzania.
Katika kumbukizi ya mwaka mmoja tangu kukamatwa kwa Lissu ambaye hadi sasa bado yupo gerezani, viongozi mbalimbali wa CHADEMA pamoja na wadau wa siasa wamejitokeza hadharani kupitia mjadala katika Baraza la Kidigitali la chama hicho lililofanyika hii leo wakitoa misimamo yao, huku wakitangaza kuanza kwa kampeni kubwa ya kutaka aachiliwe huru bila masharti.
Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Bara, John Heche, akiwa ni miongoni mwa viongozi waliotoa wito wa kuhamasisha kampeni hiyo, alieleza kuwa Lissu anapitia yote hayo kwa ajili ya Watanzania.
“Lissu amekatwa kwa ajili yetu, kwa sababu wote tunaamini Lissu hana kosa, Lissu sio mkosaji, Lissu ni mtu mwema anaetupigania. Ili asikate tamaa, tunapaswa kuanzisha sasa kuanzia leo, kampeni kubwa, kwenye kila jukwaa, kwenye Facebook, kwenye Instagram, kwenye TikTok, kwenye Twitter ya kumdai Lissu,” alisema Heche.
Kauli hiyo imeweka wazi mkakati mpya wa chama hicho kutumia nguvu ya mitandao ya kijamii kama jukwaa la kueneza ujumbe na kuhamasisha umma kuungana kudai haki ya kiongozi wao.
Mbali na mitandao ya kijamii, Heche pia aliwahamasisha Watanzania wanaoishi nje ya nchi kushiriki kikamilifu katika kampeni hiyo kwa njia ya kidiplomasia na kijamii.
“Diaspora wetu, tembeleni kila ofisi kwenye nchi uliyopo kudai kuachiliwa mara moja kwa Tundu Lissu, bila masharti,” alisisitiza Heche.
Aidha, alielekeza matumizi ya mbinu mbalimbali za uhamasishaji, ikiwemo kusambaza vipeperushi katika maeneo mbalimbali, ili kuhakikisha ujumbe unawafikia wananchi wengi zaidi.
“Tuandike vipeperushi visambae kwenye masoko, kwenye post za milingoti ya umeme, kwenye majengo ya ofisi za serikali, zikiwa na picha za Lissu, lakini zikiwa na jumbe za kudai Lissu aachiwe,” aliongeza.
Kwa upande wake, Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA, Dkt. Rugemeleza Nshala, alielezea wasiwasi mkubwa kuhusu mwenendo wa vyombo vya dola tangu kukamatwa kwa Lissu, akisema kuwa kumekuwepo na ukiukwaji wa haki za binadamu dhidi ya wanachama na wafuasi wa chama hicho.
“Tokea Lissu ameshikwa, tumeona kila aina ya unyama wa Jeshi la Polisi, namna ambavyo Mahakama vilevile inaweza kuvumilia ukiukwaji wa haki za binadamu. Matendo waliyofanyiwa wanachama na wafuasi wa CHADEMA wakati kesi zinaendelea, wamepigwa, wameumizwa,” alisema Dkt. Nshala.
Aliongeza kuwa baadhi ya matukio yaliyoshuhudiwa mahakamani yanazua maswali makubwa kuhusu uwazi na haki katika mchakato mzima wa kesi hizo zinazomkabili Tundu Lissu.
“Unakuwaje na askari anavaa kininja Mahakamani? Inatuma ujumbe gani? Hii inakuambia kwamba kuna kitu kibaya kinaendelea, kwa sababu Mahakamani ni sehemu ya uwazi,” alihoji Dkt. Nshala.

Kauli za viongozi wa CHADEMA zimeungwa mkono na baadhi ya wanasiasa wa nje ya Tanzania, akiwemo Katibu Mkuu wa Chama cha Orange Democratic Movement (ODM) kutoka Kenya, Edwin Sifuna, ambaye pia ni Seneta, akieleza mshikamano wao na CHADEMA, akisisitiza kuwa hakuna msingi wa kuendelea kumshikilia Lissu.
“Tunasimama na yeye (Tundu Lissu) kusema na kushinikiza kwamba serikali hii iweze kumuachilia sasa, kwa sababu imeonekana wazi kwamba hawakuwa na kesi yoyote dhidi yake,” alisema Sifuna.
Sifuna alisisitiza kuwa chama chake kitaendelea kuunga mkono juhudi za CHADEMA katika majukwaa mbalimbali ya kimataifa. “Tunasimama na nyinyi katika mshikamano na sisi katika majukwaa yetu yote, pia tutazidi kushinikiza wito ambao umetolewa na Chama cha CHADEMA kwamba sasa aachiliwe huyu kiongozi.”

Vuguvugu la kudai kuachiliwa huru kwa Tundu Lissu halijawaacha kando vijana wa chama hicho, ambapo Katibu wa Baraza la Vijana wa CHADEMA (BAVICHA) Wilaya ya Temeke, Blessing Barabara hii leo akizungumza na vyombo vya habari alitoa wito kwa serikali kuchukua hatua ya haraka kumaliza suala hilo.
“Tunaishauri serikali, tunaitaka serikali kuifuta kesi ya Mheshimiwa Lissu, tunahitaji Mwenyekiti wetu arejee uraiani,” alisema Barabara.
Barabara alieleza kuwa hatua hiyo inaweza kufungua mlango wa mazungumzo ya kitaifa yatakayosaidia kurejesha utulivu na mshikamano nchini.
“Tutakapofanya hivyo tutakuwa fursa ya kuruhusu mazungumzo ambayo yatakwenda kuleta utulivu, amani na haki kwenye Taifa letu,” aliongeza.
Mwaka mmoja tangu kukamatwa kwa Tundu Lissu umeacha alama kubwa katika siasa za Tanzania, bado wanaharakati, wanachama na wafuasi wa CHADEMA wameendelea kusisitiza kuwa hana hatia, huku wakitaka aachiliwe haraka bila masharti. Kuanzishwa kwa kampeni hiyo kudai kuachiliwa kwa Lissu kunaashiria hatua mpya ya mapambano ya kisiasa na kisheria, ambapo CHADEMA pamoja na wadau wa haki za binadamu wameendelea kuweka shinikizo la ndani na nje ya nchi, ili kuhakikisha kiongozi wao anarejea uraiani.
Ikiwa kampeni hiyo itapata mwitikio mkubwa kutoka kwa wananchi na jumuiya ya kimataifa, inaweza kuwa na matokeo makubwa kwenye mwelekeo wa kesi dhidi ya Lissu pamoja na mustakabali wa siasa za Tanzania.
Hata hivyo wakati hayo yote yakiendelea, itakumbukwa kuwa mnamo Februari 24, 2026 kesi ya uhaini inayomkabili Lissu iliyokuwa ikiendelea katika Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, ilihairishwa kwa muda usiojulikana mpaka pale shauri la mapitio lililowasilishwa na upande wa Jamhuri katika Mahakama ya Rufaa kukamilika.
Mwandishi: Dominic Allen
Mhariri: Yohani Gwangway


