Na Dominic Allen
Mjumbe wa Baraza Kuu la Jumuiya ya Wazazi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Dr. Ally Mandai ameongoza matembezi yaliyofanyika Chamwino jijini Dodoma ya kuhamasisha kushiriki Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, ambapo pia amepata nafasi ya kuwa mgeni rasmi kwenye Kikao cha Baraza la Wazazi wa chama hicho Wilaya ya Chamwino kilichofanyika leo katika Ukumbi wa Serikali ya Kijiji ya Chamwino, jijini Dodoma.

Akiwa Chamwino, Dr. Mandai alipokelewa na viongozi wa Jumuiya ya Wazazi wa Wilaya, wanachama pamoja na vijana wa hamasa wakiwa wamebeba mabango yaliyoandikwa jumbe mbalimbali nyingi zikiwa ni za “October Tunatiki” na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mbali na matembezi hayo yaliyofanyika katika mitaa ya Chamwino Dr. Mandai alitumia baraza hilo kuwahasa wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kutenda haki katika kipindi hiki cha Uchaguzi Mkuu, kushiriki uchaguzi na kulinda amani ya nchi.

Mwandishi: Dominic Allen


