Na Fredrick M. justine
Historia ya Deni la Taifa la Tanzania ni hadithi ndefu ya matumaini, makosa na maamuzi ya kisera yaliyojengwa juu ya ahadi ya maendeleo. Tangu kupata uhuru mwaka 1961 chini ya uongozi wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Tanzania ilikumbatia fikra za Ujamaa na Kujitegemea. Katika kipindi hicho, nchi iliweka kipaumbele kwenye maendeleo ya watu: elimu ya bure, afya ya msingi kwa wote na miundombinu ya vijijini. Ingawa rasilimali zilikuwa chache, serikali haikutegemea mikopo kwa kiwango kikubwa. Badala yake, wananchi waliitwa kujenga taifa kwa nguvu zao kupitia “Operesheni Vijiji” na juhudi za kitaifa za uzalishaji. Kwa Nyerere, deni lilikuwa chaguo la mwisho. Katika kipindi chake, deni la taifa lilikuwa chini ya shilingi za kitanzania trilioni 3 (sawa na takriban dola za kimarekani bilioni 3) – deni dogo kwa taifa changa, linalojitahidi kujitegemea.
Baada ya kuondoka madarakani kwa Mwalimu Nyerere mwaka 1985, Rais Ali Hassan Mwinyi alichukua madaraka wakati ambapo nchi ilikuwa katika changamoto ya kiuchumi. Alikumbatia sera za soko huria na kuruhusu mikopo ya kigeni kwa ajili ya mageuzi ya kiuchumi. Katika kipindi chake, deni la taifa lilipanda hadi kufikia zaidi ya shilingi za kitanzania trilioni 5.5 (dola za kimarekani bilioni 5) kufikia mwaka 1995. Mfumo wa uchumi wa soko huria uliletwa, lakini kwa gharama ya kuanza utegemezi wa mikopo ya nje, pamoja na masharti ya mabeberu wa kifedha.
Rais Benjamin William Mkapa (1995–2005) alikumbatia mageuzi ya kina ya kiuchumi na kupokea msamaha wa deni chini ya mpango wa HIPC. Deni lilishuka hadi chini ya shilingi za kitanzania trilioni 4, lakini baada ya hapo lilianza kupanda tena. Kwa wakati wa kuondoka kwake, deni lilikuwa limeongezeka hadi shilingi za kitanzania trilioni 7. Licha ya nidhamu ya kifedha aliyosifiwa nayo, baadhi ya mikataba ya ubinafsishaji ilizua sintofahamu kubwa, na mashirika ya umma yaliuzwa kwa bei ya kutia shaka. Uwekezaji wa nje ulishamiri, lakini mamlaka ya kiuchumi ya taifa ikaanza kuvuja kwa kasi.
Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete (2005–2015) alirithi deni lililokuwa katika mwelekeo wa kupanda. Serikali yake ilijikita katika kukuza uchumi na kuboresha huduma za kijamii. Hata hivyo, hadi anatoka madarakani, deni la taifa lilikuwa limeongezeka hadi shilingi za kitanzania trilioni 27. Miradi ya maendeleo ilikuwepo, lakini pia kulikuwa na matumizi yasiyoeleweka, na kiwango cha ufisadi kiliongezeka. Kikwete alirithi ushawishi mkubwa wa IMF, huku taifa likichukua mikopo mingi isiyo na ufanisi mkubwa kiuchumi.
Rais Dkt. John Pombe Magufuli (2015–2021) aliingia kwa kauli mbiu ya “Hapa Kazi Tu.” Alijikita katika miradi mikubwa ya kimkakati kama SGR, Bwawa la Julius Nyerere na miundombinu. Deni la taifa lilipanda kutoka shilingi za kitanzania trilioni 27 hadi zaidi ya shilingi za kitanzania trilioni 53 katika kipindi chake. Licha ya ongezeko hilo, miradi ya maendeleo ilikuwa inaonekana wazi, na matumizi ya serikali yalidhibitiwa kwa kiwango kikubwa. Hata hivyo, uzito wa madeni hayo uliendelea kubebwa na wananchi wa kawaida.
Baada ya kifo cha Rais Magufuli mwaka 2021, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alirithi uchumi uliokuwa katika mpito. Katika juhudi za kufufua uchumi baada ya UVIKO-19, mikopo mipya ya ndani na nje ilianza tena kwa kasi. Hadi Juni 2025, Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba alitangaza kuwa deni la taifa limefikia zaidi ya shilingi za kitanzania trilioni 105, ongezeko la zaidi ya asilimia 46 ndani ya miaka minne tu. Kinachosikitisha ni kuwa fedha hizi hazijaelekezwa kwenye miradi mipya ya maana, bali kwenye matumizi ya kawaida kama magari ya kifahari, misafara, safari zisizoisha na mishahara ya viongozi. Wakati huo huo, huduma za afya, elimu, maji na kilimo zinaendelea kudorora.
Katika mazingira haya, wananchi wanaoendelea kubeba mzigo huu wa madeni wanapaswa kuelewa kuwa wao ndio dhamana ya kila deni. Wanapokopeshwa kama taifa, si viongozi wanaowajibika binafsi, bali wananchi wa kawaida: mama ntilie, mkulima wa pamba, mwalimu wa shule ya kata, fundi viatu, na vijana wanaotafuta ajira.
Kwa muktadha wa kimataifa, viongozi wa Pan-Africanism walitoa onyo kali kuhusu hatari ya madeni. Thomas Sankara wa Burkina Faso alisema “Deni ni mikataba ya kifisadi kati ya viongozi wa Afrika na mabepari wa kimataifa. Tunalipa deni ambalo halikuleta maendeleo. Deni ni ukoloni wa kisasa.”
Sankara alipinga vikali mikopo ya IMF na World Bank, akifuta magari ya kifahari ya serikali, kukataa posho zisizo na maana, na kuhimiza uzalishaji wa ndani.
Kwame Nkrumah wa Ghana alitangaza wazi kuwa “Afrika haitakuwa huru hadi ijikomboe kiuchumi.”
Nkrumah alisema kuwa mikopo na misaada kutoka kwa mabeberu ni njia ya kuikandamiza Afrika kiakili na kiuchumi, huku wakipora madini, ardhi na nguvu kazi.
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mwenyewe, akiwa Geneva mnamo mwaka 1980, alinukuliwa akisema, “Ni upuuzi kwa mataifa masikini kuendelea kulipa madeni kwa mataifa tajiri, wakati hali zao za maisha ni duni. Tunakopa ili tulipe madeni ya zamani, huu ni wendawazimu.”
Mwalimu Nyerere alisisitiza kuwa Afrika haipaswi kuwa mfungwa wa mikataba ya kifedha isiyoleta tija wala kuimarisha uwezo wa ndani wa uzalishaji.
Kwa muktadha wa Biblia, Neno la Mungu linaonya kwa ukali juu ya hatari ya madeni.
“Tajiri humtawala maskini, naye mwenye deni ni mtumwa wa mwenye kumkopesha.” – Methali 22:7
Hili ni onyo la msingi la kifalme na kiroho – kuwa mataifa yanapokopa bila mipango ya uzalishaji au maadili ya uwajibikaji, yanajiweka katika utumwa wa kifedha. Katika Kumbukumbu la Torati 28:12, Mungu aliwaahidi Israeli kuwa watawakopesha mataifa, lakini hawatakopa, ikiwa wataishi kwa utii na haki. Maana yake ni kwamba kukopa kulikuwa ishara ya laana, ya uasi au utepetevu wa kiutawala.
Ni dhahiri kwamba Taifa lisipokumbuka misingi ya kiroho na maadili ya kiuchumi, linaweza kujikuta limefungwa kwa minyororo ya madeni isiyoisha. Tunapokopa bila kuwashirikisha wananchi, bila kuwajibika kwa fedha hizo, na bila kutengeneza msingi wa uzalishaji wa ndani, basi tunajiuza kwa karatasi za benki – mikataba ya kifisadi inayoendelea kuufunga uhuru wetu.
Leo ni wakati wa kuamka. Wananchi lazima watambue kuwa wao si watazamaji, bali ni wadhamini wa taifa hili. Ni lazima waulize: Deni linaenda wapi? Kwanini hatuoni miradi? Rasilimali zetu ziko wapi? Kwa nini watoto wetu wanasomea kwenye shule zisizo na madawati, huku viongozi wetu wakinunua magari ya shilingi za kitanzania milioni 500?
Wito huu si wa kisiasa tu – ni wa kiroho, kiuchumi, na kijamii. Afrika haihitaji misaada ya kifedha – inahitaji fikra huru, uadilifu na uongozi wa kiroho.
“He who feeds you, controls you.” –Thomas Sankara
“Mwenye deni ni mtumwa wa mwenye kumkopesha.” – Methali 22:7
(Maoni binafsi ya Mtetezi wa haki za binadamu, Fredrick M. Justine)


