Na Fredrick M. Justine
Sakata la iwapo Simba SC na Yanga SC watacheza au hawatacheza mechi yao ya Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara limegeuka kuwa mjadala wa kitaifa. Tangu tamko la Yanga SC la kususia mechi hiyo, hadi Simba SC kudai wataingia uwanjani. Mjadala huo umeenea kwenye kila kona ya nchi, kutoka mitandao ya kijamii hadi kwenye vyombo vya habari. Lakini kwa macho ya ndani zaidi, hili si suala la mpira tu, ni kivuli cha jamii yetu, na namna tunavyoshindwa kuelewana hata kwenye mambo mepesi kama dakika 90 za burudani.
Michezo ni burudani, ni sehemu ya utani wa jadi, sehemu ya kuimarisha mshikamano wa kijamii, na kwa wengine ni njia ya kutuliza akili kutoka kwenye misongo ya maisha ya kila siku. Endapo Simba SC na Yanga SC, timu zenye historia ndefu ya ushindani wa kiungwana wameshindwa kuelewana juu ya mechi moja ya Ligi Kuu, hali hiyo inatufundisha mengi kuhusu namna tunavyoshughulikia tofauti zetu katika jamii yetu. Kama kwenye mpira tu, jambo ambalo kimsingi haligusii maisha ya watu moja kwa moja, watu hawawezi kufikia mwafaka, je, itakuwaje kwenye masuala makubwa zaidi kama katiba, uchaguzi au mgawanyo wa rasilimali?
Tatizo si Simba SC wala Yanga SC, bali ni tabia ya kutokuwa na utamaduni wa maridhiano. Tunazidi kujenga jamii isiyo tayari kusikiliza upande mwingine. Kila kundi linakazana kushinda hoja, si kuelewana. Na zaidi ya hapo, tunashuhudia kile ambacho kwa muda mrefu kilikuwa kinatajwa kwa sauti ya chini, siasa kuingilia michezo. Kauli ya msemaji wa Yanga SC, Ally Kamwe, aliyedai kuwa “kuna kiongozi mkubwa aliamuru mageti ya Uwanja wa Taifa yasifunguliwe”, si kauli ya kawaida, hii inaashiria kuwa si tu Tume ya Huru ya Taifa ya Uchaguzi haiko huru, bali pia hata Bodi ya Ligi haiko huru. Maamuzi ya kisera ndani ya mpira yamevamiwa na maslahi ya kisiasa.
Hali hii ni ya hatari, kwa sababu inapoharibu uhuru wa michezo, inaua maana ya ushindani wa haki na inachochea chuki kati ya mashabiki, badala ya kuleta mshikamano. Wanasiasa kuingilia michezo si tu haifai, ni sumu kwa jamii inayojitafuta kwenye misingi ya haki, usawa na utawala bora. Mpira unapaswa kuwa eneo la furaha, la kujenga urafiki wa jadi, si jukwaa la maamuzi ya kisiasa yasiyo na uwazi.
Kinachoonekana ni kwamba wakati taifa linakabiliwa na madai halali ya marekebisho ya kisiasa, kama kauli maarufu ya “No Reform, No Election”, mijadala ya michezo kama huu wa Simba na Yanga inageuzwa kuwa kivuli kinachofunika hoja nzito. Hii ni hatari sana, kwa sababu historia imetufundisha kuwa watawala wanaposhindwa kujibu hoja, huibua burudani kama kisingizio cha kuwanyamazisha watu. Wanatoa sherehe badala ya mabadiliko, kelele za uwanjani badala ya majadiliano ya Bungeni.
Hili linaendana kabisa na nadharia ya kale ya Dola la Kirumi, ‘Bread and Circus’. Katika nyakati za machafuko au ukandamizaji, watawala wa Roma waligawa chakula cha msaada na kuandaa michezo ya ‘gladiator’ ili kuwazuia watu kufikiri kuhusu haki, maisha bora, au mfumo wa utawala. Leo, badala ya mkate na ‘gladiator’, tuna televisheni, mechi na propaganda mitandaoni.
Wananchi wanapaswa kuelewa kuwa si kila kelele ya mpira ni kwa sababu ya kandanda. Si kila tamko la “tunacheza” au “hatuchezi” ni la kisoka. Kuna wakati michezo hutumiwa kama kisingizio cha kuondoa macho ya watu kwenye mambo ya msingi. Wakati Simba SC wanasema “tunacheza” na Yanga SC wanasema “hatuchezi”, sisi kama taifa hatupaswi kuridhika kushabikia upande mmoja tu bila kuuliza: Kwa nini tunashindwa kuelewana? Kwa nini mechi ya dakika 90 iwe chanzo cha kutishiana, kuonyesha ubabe au kutoa matamko yanayochochea mashaka zaidi kuliko matumaini?
Tunahitaji mpira, lakini zaidi ya mpira, tunahitaji maridhiano. Tunahitaji mechi bora, lakini zaidi ya mechi tunahitaji taasisi huru, tume huru, bodi huru. Tunahitaji mabao uwanjani, lakini zaidi ya hapo tunahitaji ushindi wa haki katika siasa, uchumi, na maisha ya kila siku ya Mtanzania. Turejee kwenye misingi ya michezo, burudani, mshikamano na heshima.
Wakati tunapenda kandanda, tusiache kupigania mabadiliko ya kweli. Tusiache kuuliza maswali magumu. Tusiache kuamini kuwa taifa linaweza kuwa bora zaidi—ndani ya dakika 90 za mpira, na nje ya muda huo pia.
(Maoni binafsi ya Mtetezi wa haki za binadamu, Fredrick M. Justine)


