Mahakama: Lissu hakulenga kuitishia Serikali
Mahakama Kuu Masjala-Ndogo ya Dar es Salaam imesema upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha kiini cha pili cha kosa la uhaini wa kuitishia Serikali linalomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleoa (CHADEMA) Taifa, Tundu Lissu.
Mahakama Kuu imeeleza kuwa hakuna ushahidi wa moja kwa moja unaonesha kwamba kauli zilizotolewa na mshatakiwa (ambaye ni Tundu Lissu), zililenga kuitishia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Imesema msimamo wa ‘No reforms, No election’ ni kauli ya kisiasa iliyolenga kuhamasisha umma kususia uchaguzi na sio kuitishia Serikali.
Akisoma hukumu hiyo, kiongozi wa jopo la majaji watatu waliosikiliza kesi hiyo, Jaji Dunstan Ndunguru, amesema kosa la kuitishia Serikali lina viini vitatu vinavyopaswa kuthibitishwa na upande wa mashtaka.
Amevitaja ni mshtakiwa kuwa katika utii wa Jamhuri, kujenga nia ya kuitishia Serikali na kudhihirisha nia hiyo kwa kuchapisha maandishi au machapisho au kwa kitendo cha siri kinachojidhihirisha.
Jaji Ndunguru amesema viini viwili vya mwisho ndivyo vilivyokuwa na ubishani katika kesi hiyo na kwamba uthibitisho wake ndio ungeamua iwapo Lissu ana hatia au hana hatia.
Ikiendelea na uchambuzi wa viini vya kosa la kuitishia Serikali, Mahakama imeeleza kwamba upande wa utetezi ulitaka maneno hayo yapimwe katika muktadha wa kisiasa ikiwemo kuelezea msimamo wa kisiasa wa CHADEMA na mtazamo huo uliungwa mkono na shahidi wa 2,3,4 na 5.

