
Mkutano wa kimataifa wa tabia nchi unaendelea huko nchini Uturuki, ukipenda uite COP 31 kwa kimombo, mkutano huu ulioanza siku ya leo novemba 9 utatafika tamati novemba 20 katika jiji la antalya ambapo masuala chungu nzima yatajadiliwa ikiwemo kusisitiza mataifa ulimwenguni, kuhamia katika matumizi ya nishati safi, pasipo kusahahu upatikanaji wa fedha za kusaidia nchi zinazoendelea kukabili athari za mabadiliko ya tabianchi.
Wawakilishi kutoka Mataifa takribani 197, hii leo watajadiliana kuhusiana na chakula,kilimo pamoja na afya, huku wakijikita zaidi katika kutazama namna ambavyo ongezeko la joto na mabadiliko ya tabianchi lilivyoathiri uzalishaji wa chakula, vyanzo vya maji pamoja na ustawi wa watu kote uduniani.
Shirika la afya ulimwenguni yaani WHO linasema mabadiliko ya tabianchi yanachangia moja kwa moja dharula za kibinadamu kutokana na ongezeko la joto, moto wa nyikani, mafuriko, na mambo mengine kadha wa kadha.
WHO inasema utafiti unaonesha kwamba watu takribani bilioni 3.6 tayari wanaishi katika maeneo yanayoweza kuathiriwa na mabadiliko ya tabianchi, si hivyo tu WHO katika chapisho lake la mwaka 2023 linalozungumzia mabadiliko ya hali hewa,inabainisha kati ya mwaka 2030 HADI 2050 mabadiliko ya tabianchi yanaweza kusababisha takribani vifo laki mbili na nusu kutokana na utapiamlo,malaria, kuhara na msongo wa mawazo unaosababishwa na kuongezeka kwa kiwango cha joto.
WHO inaeleza kwamba maeneo yatakayoathirika ni pamoja na yale yenye miundombinu dhaifu ya huduma za kiafya, hususan katika mataifa yanayoendelea ulimwenguni, huku ikipendekeza kupunguza uzalishaji wa gesi chafu na matumizi ya nishati mbadala ili kupunguza uchafuzi wa hewa.
