Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Mabadiliko ya Tabianchi (UN Climate Change) limezindua mfumo mpya wa kutambua na kufuatilia mchango wa kampuni, taasisi za kifedha, miji na mamlaka za maeneo mbalimbali katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, unaolenga kuongeza uwazi na uwajibikaji katika utekelezaji wa ahadi za kufikia uzalishaji halisi sifuri wa gesi joto (Net-Zero).
Uzinduzi huo umefanyika Novemba 12, 2026, wakati wa Mkutano wa 31 wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP31), unaofanyika Antalya, Uturuki. Mfumo huo unaoitwa Net-Zero Recognition Framework (NZRF) umeanzishwa ili kuwezesha wadau wasio wa kiserikali kuweka wazi ahadi zao za kupunguza uzalishaji wa gesi joto, mipango wanayotumia kutekeleza ahadi hizo pamoja na hatua walizopiga kuelekea kufikia malengo yao.
Uzinduzi wa mfumo huo umefuatia kipindi cha majaribio cha mwaka mmoja na ni sehemu ya juhudi za kuimarisha uwazi katika utekelezaji wa hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi zinazochukuliwa na wadau nje ya mifumo ya serikali.
Akizungumzia uzinduzi huo, Katibu Mtendaji wa UN Climate Change, Simon Stiell, amesema mfumo huo ni nyenzo muhimu ya kuongeza uwazi na uwajibikaji, akieleza kuwa kupitia jukwaa la NAZCA, kampuni, taasisi za kifedha, miji na mamlaka za maeneo mbalimbali zitaweza kuweka wazi mipango yao ya kufikia uzalishaji halisi sifuri na kutoa taarifa kuhusu maendeleo ya utekelezaji wake.
Jukwaa la NAZCA limekuwa likikusanya taarifa kuhusu hatua zinazochukuliwa na wadau wasio wa kiserikali katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi tangu mwaka 2014, hatua inayolenga kuongeza ufuatiliaji wa ahadi na kuimarisha uwajibikaji katika juhudi za dunia za kupunguza uzalishaji wa gesi joto.


