Waziri wa Nishati, Dkt. Juma Zuberi Homera, amesema Tanzania inaendelea kutafuta ushirikiano na wadau wa kimataifa kupitia Mkutano wa 31 wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP31), unaofanyika Antalya, Uturuki, ili kufanikisha lengo la kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.
Amesema mkutano huo umefungua fursa kwa Tanzania kujadiliana na taasisi mbalimbali za kimataifa kuhusu namna ya kuongeza uwekezaji na kuimarisha upatikanaji wa teknolojia za nishati safi ya kupikia, huku akitaja taasisi ya Sustainable Energy for All kuwa miongoni mwa wadau walioonesha utayari wa kushirikiana na nchi hiyo.
Waziri Homera ameeleza kuwa ushirikiano huo unalenga kuhakikisha huduma za nishati safi zinawafikia wananchi katika maeneo mbalimbali ya nchi, ikiwemo vijijini na mijini, ili kuongeza matumizi ya nishati hiyo na kupunguza utegemezi wa nishati zisizo safi.
Amesisitiza kuwa kufikiwa kwa lengo hilo kunahitaji ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi na taasisi za maendeleo, pamoja na kuimarisha mifumo ya upatikanaji na usambazaji wa nishati safi kwa wananchi.
Akizungumza akiwa Antalya, Uturuki, Dkt. Homera amesema Tanzania itaendelea kutumia majukwaa ya kimataifa kama COP31 kujenga mahusiano ya kimkakati yatakayosaidia kutekeleza mipango yake ya nishati na kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.
Hata hivyo Waziri Homera amebainisha kuwa matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini yameongezeka kutoka asilimia 6.9 mwaka 2021 hadi asilimia 28.6 mwaka 2025, hatua inayoonesha maendeleo katika utekelezaji wa mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia wa 2024 – 2034 ikiwa inalenga kufikia asilimia 80 kwa Watanzania ifikapo mwaka 2034.


