
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Bara, John Heche, ametoa pole kwa familia ya Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu, kufuatia kifo cha kaka yake, Wakili Alute Mughwai Lissu, huku akieleza masikitiko yake kutokana na changamoto anazopitia Lissu katika kudai haki.
Heche ameyasema hayo jijini Arusha, katika misa takatifu ya kumuaga marehemu Alute iliyofanyika katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Theresia, ambapo ameeleza kuwa Lissu amepitia mengi katika harakati zake za kutetea haki, ikiwemo kujitetea Mahakamani, kunyimwa haki ya kuonana na mawakili wake pamoja na kukabiliwa na kesi ya uhaini ambayo baadaye ilitupiliwa mbali, huku akihukumiwa kifungo cha miaka minne kwa kosa la uchochezi.
Aidha, Heche amesisitiza umuhimu wa kulinda utawala wa sheria, akieleza kuwa utawala wa sheria unapoporomoka nchini, hakuna mfumo unaoweza kuhakikisha haki inatendeka, kwani watu wanaweza kuamua kwenda moja kwa moja kwa majaji na mahakimu bila kufuata taratibu zilizowekwa.
Akitoa wito kwa wananchi kuiombea familia ya Lissu ili iweze kuvumilia kipindi hicho kigumu cha maombolezo, pia ameongeza kuwa Watanzania wanapaswa kuungana katika kujenga taifa linalozingatia haki na utawala wa sheria, akisisitiza kuwa jukumu la Serikali ni kusimamia utaratibu na kuhakikisha haki inatendeka badala ya kutumia mamlaka yake kuwaadhibu au kuwakomoa watu.
Kaka yake Tundu Lissu, Wakili Alute Mughwai Lissu, alifariki dunia Novemba 01, 2026, katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Selian jijini Arusha, alipokuwa akipatiwa matibabu, ambapo mazishi yake yalicheleweshwa baada ya familia kuamua kusubiri kwanza hukumu ya kesi iliyokuwa ikimkabili Tundu Lissu, ili ndugu na jamaa waweze kuhudhuria kesi hiyo kabla ya kuendelea na taratibu za mazishi.
