Nini chanzo? Kutonufaika kwa wavuvi wazawa, biashara ya mabondo

Jiji la Mwanza, linalosifika kama kitovu cha uchumi wa Kanda ya Ziwa, limegeuka kuwa uwanja wa kilio na maswali yasiyo na majibu kwa wavuvi wazawa. Licha ya rasilimali kubwa ya maji na uwepo wa Ziwa Victoria, sekta ya uvuvi inakabiliwa na dhoruba kali.

Miongoni mwa mambo yaliyoibuliwa na uchunguzi wa Land Dwellers, ni  biashara hii ya mabondo ya samaki yatokanayo na samaki aina ya sangara kutowanufaisha wavuvi wazawa, huku kukiwa na tuhuma biashara haramu, za ukwepaji wa kodi, na mamlaka husika zikinyooshewa kidole kwa kushindwa kutimiza wajibu wao ipasavyo.

Pamoja na ukweli kwamba kifungu cha 22 (1) cha Sheria ya Uvuvi ya Mwaka 2003 kinakataza wazi ukusanyaji na usafirishaji wa bidhaa za samaki bila leseni, lakini utekelezaji wake ni duni. Wasimamizi mwaloni wanashindwa kuzuia mianya inayotumiwa na raia wa kigeni, hali inayozua maswali kuhusu uadilifu na uwezo wa doria huku mapungufu makuwa ya uwajibikaji kiutawala na kisheria.

Taarifa rasmi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi hivi karibuni

Katika hotuba ya Mwaka 2024/2025, Waziri wa Mifugo na Uvuvi alieleza maendeleo mbalimbali yanayohusiana na sekta ya uvuvi. Katika maendeleo yaliyotajwa ni pamoja na viwanda vilivyoanzishwa hapa nchini kuchakata bidhaa za samaki ikiwemo mabondo

“Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2024/2025, Wizara imeendelea kuthibiti ubora na usalama wa mazao ya uvuvi kwa kufanya kaguzi 943 kwenye viwanda 47 vya kuchakata mazao ya uvuvi, viwanda 17 vya mabondo, maghala 135 ya kuhifadhia mazao yaliyokaushwa, maghala ya ubaridi (cold storage) 53, vituo 37 vya kuhifadhia samaki hai wa mapambo, mialo 33 ya kupokelea samaki, 64 mipaka, maeneo ya viwanja vya ndege na masoko ya samaki nchini. 89.”

Licha ya hotuba hii kuonesha kuwa kuna mafanikio lukuki katika sekta ya uvuvi, bado kitendawili cha nani ananufaika katika biashara ya mabondo hapa nchini kinakosa majibu.

“Mheshimiwa Spika, katika kuthibiti ubora wa mazao ya uvuvi, jumla ya vyombo 782 vya kusafirisha mazao ya uvuvi (magari na maboti) vilikaguliwa na kupewa cheti cha ubora (Approval Certificate) baada ya kukidhi vigezo. Aidha, vibali vya kusafirisha mazao ya uvuvi ndani ya nchi (Movement Permit) 54,638 vilitolewa. Sanjari na hivyo jumla ya vyeti vya afya 12,293 (Export Health Certificate) vilitolewa kwa mazao ya uvuvi yanayosafirishwa nje ya nchi.”

Upotevu wa rasilimali za uvuvi hapa Tanzania

Adrew  Misana (siyo jina halisi), Mvuvi kutoka kisiwa cha Ukara anasema kwa ujumla biashara ya mabondo inakabiliwa na magendo ikiwemo kutoroshwa kutoka Tanzania kwenda Uganda. Misana anasema walanguzi wengi katika visiwa vya Ukerewe hawana leseni na wanauza kwa wafanyabiashara wa Uganda ambao wao wanasafirisha kwenda China.

“Sidhani kama tunapata hata nusu ya faida ya mabondo. Walanguzi wengi hapa wanasafirisha mabondo kwenda Uganda. Ukiangalia wengi wao hawana leseni. Hawa waganda wana viwanda vya kuchakata ili wasafirishe kwenda china. Serikali bado haijajipanga kuthiibiti biashara hii ili ilete faida,” anasema Andrew Misana.

Wakati wavuvi wakieleza matukio haya, mwaka 2024, Utafiti wa Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali  wenye jina Performance Audit Report on the Management of Fisheries in the Country, ulionesha kuwa kuna mianya inayosababisha upotevu wa rasilimali za uvuvi hapa nchini.

Katika ukurasa wa 12, ripoti ilionesha kuwa  asiliamia 72.9 ya vyombo vya uvuvi  nchini Tanzania havikusajiliwa. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, vyombo 20,885 kati ya 28,615 vilikuwa havina usajili. Ripoti hii ilionesha kuwa makadirio ya hasara kutokana na vyombo hivyo kutokusajiliwa ni Bilioni 15.16.

Ukurasa wa 15 wa ripoti hii unaonesha kuwa takwimu za samaki zilikusanywa kutoka maeneo 59 tu kati ya 595 ya kutua samaki hapa nchini Tanzania, jambo linaloonesha upotevu wa rasilimali hizi kutokana na usimamizi mdogo.

Pia, ukurasa wa 93 wa ripoti hii, CAG alionesha udhaifu wa usimamizi wa kanzidata na ubora wa taarifa za uvuvi. Taarifa muhimu kama mavuno ya samaki, ukubwa wa samaki, mapato na takwimu zingine hazikuwa za kuaminika.

Hali inayoonekana katika ripoti ya CAG ya mwaka 2023, ndiyo hii inayoelezwa na wavuvi katika Ziwa Victoria ambao wanaona wavuvi hawanufaiki kutokana na usimamizi usioridhisha wa mamlaka za uvuvi ikiwemo maafisa uvuvi katika maeneo husika.

Kwa mujibu wa Sheria ya Uvuvi, Na. 22 ya Mwaka 2003, sheria haitaji moja kwa moja “Maafisa Uvuvi wa Mkoa” au “Maafisa Uvuvi wa Wilaya” kwa majina, bali inaweka mfumo unaowapa mamlaka kupitia Mkurugenzi wa Uvuvi na maafisa wanaoteuliwa chini ya kifungu cha 5. Pia inaruhusu mamlaka za serikali za mitaa kuteua maafisa wa kutekeleza sheria hizo.

Kifungu cha 5(1) kinaeleza kuwa Serikali inapaswa kuteua maafisa wa kuhakikisha usimamizi wa uvuvi unafanyika kwa ufanisi, kwa tija na kwa kuzingatia sheria. Kifungu cha 5(2) kinaeleza kuwa maafisa hao hupewa majukumu na Mkurugenzi wa Uvuvi na hupangwa katika ofisi au taasisi mbalimbali kwa ajili ya usimamizi sahihi wa rasilimali za uvuvi.

Aidha, Kifungu cha 5(5) kinamtaka Mkurugenzi kuteua maafisa wa usajili na leseni, maafisa wa utekelezaji wa sheria pamoja na Wakaguzi wa Samaki, huku Kifungu cha 5(6) kikieleza kuwa maafisa hao wanawajibika kwa Mkurugenzi wa Uvuvi.

Sheria hiyo pia, kupitia Kifungu cha 5(8), inampa Mkurugenzi mamlaka ya kukabidhi baadhi ya majukumu yake kwa maafisa wa umma au mamlaka za serikali za mitaa. Vile vile, Kifungu cha 5(9) kinaruhusu mamlaka za serikali za mitaa kuteua maafisa wenye sifa ili kutekeleza majukumu waliyopewa chini ya sheria hiyo, huku Kifungu cha 5(10) kikisisitiza kuwa maafisa hao wanapaswa kufuata maelekezo na miongozo inayotolewa na Mkurugenzi wa Uvuvi.”

Wakati sheria inahitaji ushirikiano kati ya mamlaka za juu na zile zilizopo chini ili kusimamia rasilimali za uvuvi ikiwemo mabondo, baadhi ya viongozi wa ngazi za mitaa wanaona kuwa maafisa wa ngazi za juu hawawashirikishi ili kuangalia ni namna gani wavuvi wazawa na wadogo wanalindwa katika maslahi yao.

Maafisa wawili wa ngazi ya kata ambao hawakuwa tayari kutajwa majina yao, wamezungumzia jambo hili wanasema wao wanabaki kwa majina tu na hawashirikishwi katika mambo muhimu ya kimaamuzi.

“Kifungu cha 8 kinaitaka Ofisi ya Mkurugenzi kuhakikisha mamlaka za serikali za mitaa zinashirikishwa na zinafahamishwa kuhusu usimamizi wa uvuvi, na endapo kutatokea mgongano au usimamizi usioridhisha, sheria inaweka utaratibu wa mashauriano na hatua za kurekebisha hali hiyo,” ameeleza mmoja wa viongozi wa kata.

Mhandisi, Nelson Mfinanga, Diwani wa Kata ya Buhongwa, jijini Mwanza, anasema kuwa kumekuwa na athari za kiusalama, mianya ya kiutawala, na maumivu ya kiuchumi yanayowakuta wananchi na wachuuzi wadogo katika ngazi ya kata na mitaa yote ya Mwanza kutokana na hali hii ya utoroshaji wa rasilimali ziwani.

Kwa mujibu wa Mfinanga, fedha zinazopotea kupitia utoroshaji wa mabondo zingekuwa zinakusanywa kihalali na halmashauri, zingesaidia kujenga miundombinu ya kijamii kama vifaa vya shule kwa watoto maskini, hospitali, na vituo imara vya polisi kwa ulinzi wa wafanyabiashara.

“Inasikitisha kuona rasilimali za mabilioni zinatoroshwa ziwani huku halmashauri zetu zikikosa mapato ya kutosha kuboresha huduma za jamii. Serikali inaposhindwa kudhibiti biashara ya mabondo, maana yake inawanyima wananchi wetu haki ya kupata elimu bora na usalama wa maisha yao. Lazima kuwepo na udhibiti wa pamoja, na viongozi wa ngazi zote tushirikiane kuvunja hii mitandao ya uhalifu inayowanyonya wavuvi wetu,” anasema.

Ripoti ya utafiti ya shirika lisilo la kiserikali la kimataifa la Trade Records Analysis of Flora and Fauna in Commerce (TRAFFIC) iliyofanyika kati ya mwaka 2012 hadi 2019 inayoitwa “A rapid assessment of the trade in fish swim bladders from Africa to Hong Kong SAR,” inabainisha kuwa usafirishaji wa mabondo kutoka nchi za Afrika Mashariki hauripotiwi kikamilifu.

Ripoti inabainisha kuwa wakati data rasmi zikionyesha Tanzania ilisafirisha mabondo ya sangara yenye thamani ya dola za Marekani milioni 77.9 kwa njia ya kisheria katika mwaka 2019 pekee, TRAFFIC ilionyesha kuwa ukosefu wa namba maalum za utambuzi wa forodha na mitandao ya magendo husababisha kiasi kikubwa cha mabondo kupita bila kukaguliwa. Hali hii inasababisha nchi kupoteza mapato makubwa ambayo hayajawekwa kwenye hesabu rasmi kwenda kwenye mitandao haramu ya mipakani.

Takwimu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi inaonesha kuwa kabla ya mdororo mkubwa wa soko la giza, sekta ya Sangara nchini Tanzania ilikuwa inaingiza zaidi ya dola za Kimarekani milioni 280 kwa mwaka huku thamani ya soko la ndani la kilo moja ya sangara mzima ni kati ya TZS 8,000 hadi 12,000, lakini thamani ya mabondo yaliyokaushwa hufikia dola 1,000 hadi 7,700 kwa kilo yakifika masoko ya kifahari ya Hong Kong.

Taarifa ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ya mwaka wa fedha 2023/2024 inaonesha kuwa pamoja na changamoto hizi, sekta nzima ya uvuvi bado inachangia takriban 1.8% ya Pato la Taifa (GDP) na mauzo ya jumla ya TZS bilioni 493, ikionyesha fursa kubwa iliyopo katika soko la mabondo kama likidhibitiwa kikamilifu.

Biashara ya mabondo ya samaki imekuwa dhahabu mpya ya Mwanza. Mabondo haya husafirishwa kwenda mataifa ya Asia, hasa China na Hong Kong, ambako hutumika kutengeneza nyuzi za upasuaji wa kitabibu, vyakula vya kifahari, na gundi ya ndege.

Dk. Ismael Kimirei, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) anaonya kuwa uvuvi haramu na unaolenga samaki wakubwa wa sangara hasa majike kwa ajili ya kupata mabondo makubwa, unahatarisha hifadhi ya samaki (fish stocks) ndani ya Ziwa Victoria.

“Kumvua samaki huyu kwa ajili ya bondo lake maana yake ni kuua kizazi kijacho cha samaki ndani ya Ziwa Victoria. Ndani ya miaka kumi ijayo, viwanda vya minofu Mwanza vinaweza kufungwa kwa kosa hili la kiutawala,” anasema.

Tafiti za TAFIRI zinaonyesha kuwa uvuvi usio endelevu unaoendeshwa kwa mbinu haramu unahatarisha ikolojia ya Ziwa Victoria. Ili kuzuia upotevu wa mapato na kulinda mustakabali wa rasilimali hizi, lazima kuwepo na mifumo thabiti ya kidijitali ya kufuatilia mazao ya uvuvi tangu yanapovuliwa hadi sokoni, pamoja na kuimarisha doria za kisayansi ziwani.

Dk. Beda Mwang’onde, Mhadhiri Mwandamizi katika fani ya Elimu ya Viumbe Hai Wadogo sana na Elimu ya Vimelea katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) nchini Tanzania, anasema kuwa ni lazima jamii za wavuvi na wachuuzi wadogo zipewe elimu ya usimamizi endelevu wa rasilimali.

“Uwindaji wa fujo wa samaki kwa ajili ya mabondo pekee hauharibu tu uchumi wa taifa, bali unaharibu usalama wa chakula na kuua ajira za wazawa mkoani Mwanza. Ili ziwa liendelee kuwa salama na lenye tija, serikali lazima isimamie sheria kikamilifu kulinda viumbe vya majini,” anasema.

Hata Diwani wa Kata ya Buhongwa, anathibitisha kuwa wavuvi wanapata faida kidogo sana kutokana na changamoto za leseni na tozo, huku uvuvi haramu ukiathiri mapato yao. Serikali za mitaa zinashindwa kutenga bajeti ya kutosha kwa ajili ya doria, jambo ambalo linawapa nafasi wafanyabiashara wa China kutumia mifumo isiyo rasmi. Hii inasababisha serikali kupoteza mapato ya kodi kila mwaka ambayo yangeidhaidia jamii kupata huduma bora.

Uchunguzi unaonesha kuwa kuna ombwe la usimamizi kutoka kwa viongozi wa wizara na wabunge katika kuimarisha sera za ulinzi wa rasilimali. Kushindwa kwa viongozi wa kisiasa kuziba mianya ya kisheria kumeruhusu soko hili kutawaliwa na raia wa kigeni ambao baadhi yao hawaingizi miamala yao katika mifumo rasmi ya kodi ya serikali. Kushindwa kwa mifumo ya usimamizi si tu suala la sheria, bali ni ukosefu wa uwajibikaji wa dhati katika ngazi zote za kiutawala na kisiasa.

Mwandishi: Yohani Gwangway
Mhariri: Dominic Allen

Hot this week

Mnyonge, mnyongeni ila haki yake mpeni

By Dorlingson Edward Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS), leo...

CHADEMA kutoa msimamo wake kuhusu maridhiano

By Veronica Mlyatu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetoa...

Popular Articles

Safari ya Mashimba katika kutetea jamii ya Wahadzabe

Nchini Tanzania  kuna jumla ya makabila zaidi ya 120...

Polisi waendelea kuwashikilia viongozi wa CHADEMA

Ni siku ya kwanza tangu kukamatwa kwa viongozi wa...

Siku ya Vijana Duniani.

Kwa sasa ni kijana wa miaka 25 ambaye amejiajiri...

BWAWA LA ARBA’AT  LASABABISHA MAAFA NCHINI SUDAN

Watu 30 mashariki mwa Sudan na na wengine 60...

Sand Mining in Tanzania: Trails of Destruction in Lake Victoria and its Environs

By Dominic Allen On November 14th, 2021 in the Geita...

 Utekaji: Fumbo linalotushinda?

Na Yohani Gwangway Taifa la Tanzania kwa miaka mingi limekuwa...

Abduction: Is it a riddle we can’t solve?

By Yohani Gwangway For many years Tanzania has been an...

Mustakabali wa Hewa Safi kwa kila kiumbe

Na Dominic Allen Msingi wa maisha ya viumbe hai yaani...
LAND DWELLERS FACT CHECK HUB VERIFY FACTS STOP MISINFORMATION Trusted Fact-Checking in Tanzania Beyond What You Know VERIFY NOW

Related Articles

Popular Categories

DWELLERS CHECK-HUB Verify Facts. Stop Misinformation Trusted Fact-Checking in Tanzania • Beyond What You Know VERIFY NOW