Chama cha ACT Wazalendo kimesema kuwa Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana ya chama hicho, Abdul Nondo amekutwa na kiwango kikubwa cha sumu mwilini ambapo madaktari wa hospitali ya Aga Khan bado hawajafahamu kama sumu hiyo imetokana na athari za kuteswa au alipewa kitu chenye sumu na waliomteka.
Taarifa juu uwepo wa sumu mwilini mwa Abdul Nondo imetolewa leo Disemba 4, 2024 na Katibu wa Habari na Uenezi wa Ngome ya Vijana ya chama hicho, Mwl. Philbert S. Macheyeki ambapo ameongeza kuwa Nondo alifanyiwa upasuaji mdogo wa unyayo siku ya jana baada ya kuonekana kuwa na mivunjiko midogo midogo.
Kwa mujibu wa chama cha ACT Wazalendo hali ya mwanasiasa huyo bado haijatengamaa kutokana na majeraha na maumivu makali, hivyo jopo la madaktari wanaendelea kumpatia matibabu.
Nondo alitekwa mnamo siku ya Jumapili ya Disemba 01, 2024 maeneo ya Stendi ya mabasi ya Magufuli, jijini Dar es Salaam na kupatikana usiku wa siku hiyo akiwa ametelekezwa maeneo ya Coco Beach ambapo alipatiwa msaada na wasamaria wema waliompeleka katika ofisi za ACT Wazalendo, Magomeni kisha kupelekwa katika hospitali ya Aga Khan.


