Ziwa Victoria ni chanzo muhimu cha maisha kwa maelfu ya watu wanaotegemea shughuli za uvuvi, lakini ndani ya samaki sangara anayevuliwa katika ziwa hili, kuna sehemu nyingine yenye thamani ya kibiashara, mabondo, ambapo uchunguzi wa Land Dwellers umebaini biashara hii kutowanufaisha wavuvi wazawa, faida ikienda kwa wageni.
Katika sehemu ya tatu ya makala hii, ambayo inachunguza jinsi biashara ya mabondo isivyowanufaisha wavuvi wazawa, ikimulika changamoto wanazokumbana nazo, tunaangazia na kuainisha mikakati madhubuti ya kurejesha mapato na haki ya mvuvi wa Ziwa Victoria.
Utafiti wa mwaka 2019 ulioagizwa na Taasisi ya Lake Victoria Fisheries Organisation (LVFO), kwa kushirikiana na mradi wa Shirika la Ujerumani la Ushirikiano wa Kimataifa (GIZ), unaoitwa Responsible Fisheries Business Chain, umebainisha kuwa biashara ya mabondo ya samaki sangara nchini Tanzania, Kenya na Uganda ilikuwa na thamani ya takribani Dola za Marekani milioni 86 kwa mwaka.
Kwa upande mwingine, ripoti ya mwaka 2025 ya Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) “Tathmini ya Sekta ya Uvuvi wa Maji Baridi Barani Afrika” ilinukuu taarifa ya Shirika la Chakula Duniani (FAO), kuwa sekta ya uvuvi wa maji baridi barani Afrika kwa ujumla huzalisha zaidi ya tani milioni 3.3 za samaki kwa mwaka, huku thamani iliyoongezwa ya uzalishaji huo ikikadiriwa kufikia dola bilioni 6.3 mwaka 2019.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa uharibifu wa mazalia, uchafuzi wa mazingira na shinikizo la uvuvi ni miongoni mwa changamoto zinazotishia uendelevu wa uvuvi, na inapendekeza uwekezaji katika urejeshaji wa mazalia na usimamizi bora wa rasilimali za maji. Kwa Ziwa Victoria, Benki ya Dunia inakadiria kuwa takriban dola za Marekani bilioni 1.9 zinahitajika kwa uwekezaji wa mifumo ya usafi wa mazingira katika bonde la ziwa, ikiwa ni pamoja na mipango ya majaribio katika Mwanza, Entebbe na Homa Bay.
Lakini Tanzania haina upungufu wa sheria. Sheria ya Uvuvi ya mwaka 2003, Kifungu cha 22(1), ikisomwa pamoja na Kanuni ya 20 ya mwaka 2005, inakataza wazi usafirishaji wa bidhaa za samaki bila leseni halali. Lakini kwanini biashara haramu inatajwa kufanyika katika baadhi ya maeneo, ikiwemo Sweya na Buhongwa?
Uchunguzi wetu umebaini kuwa kuna “mizizi ya uzembe” katika mamlaka za utendaji. Maafisa uvuvi na polisi wa doria katika mialo hiyo wanatajwa kushindwa kudhibiti mianya ya usafirishaji holela. Hii inasababishwa na ama ukosefu wa rasilimali za kufanyia doria.
Sima Constantine, Diwani Kata ya Mhanduna Mstahiki Meya wa Jiji la Mwanza anasema, wamekuwa wakiyaona malori yakiondoka usiku, lakini wakiuliza kuhusu tozo za halmashauri, huambiwa ni ‘mabaki’ ya viwandani wakati kiuhalisia ni rasilimali ghafi inayopaswa kulipiwa kodi ya maliasili.
Kwa mujibu wa Sima, ili kuwasaidia wananchi wa Mwanza wakiwemo wavuvi wadogo wanaokabiliwa na umaskini, Jiji limeamua kuweka kipaumbele cha kutoa mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Jiji ili Kupambana na umaskini.
“Fedha hizi zinatengwa kwa ajili ya vikundi vya vijana, wanawake, na wenye ulemavu ili kuwaongezea mitaji rasmi. Hatua hii inalenga kuwatoa wavuvi wadogo kwenye mtego wa kukopa kwa wafanyabiashara wakubwa wa mabondo wanaowanyonya,” anasema.
Balozi Dk. Bashiru Ally Kakurwa, Waziri wa Mifugo na Uvuvi anakemea vikali mifumo ya kinyonyaji ya soko huria isiyodhibitiwa ziwani. Amebainisha kuwa serikali haiwezi kuendelea kuacha sekta hii mikononi mwa mawakala wanyonyaji wanaowalisha maneno viongozi huku wakihujumu uchumi wa wavuvi wa kweli.
Dk. Bashiru anasikitishwa na ukosefu wa weledi na zana duni miongoni mwa wavuvi wadogo unaowafanya wabaki maskini. Anasema lengo la wizara ni kuongeza uzalishaji wa samaki kitaifa kutoka tani chini ya 500,000 hadi kufikia mahitaji halisi ya taifa ya tani milioni 1.2.
Tayari amekwisha waagiza watendaji wakuu wa Wizara na bodi za ushauri kuhakikisha rasilimali za uvuvi zinawanufaisha vijana na wavuvi wadogo, huku akiweka msisitizo mkubwa kupitia Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) kutoa elimu ya matumizi ya zana bora na salama ili wavuvi wavue kwa tija bila kuharibu mazingira.

Dk. Robert Kayanda, Mkurugenzi wa Ufuatiliaji na Utafiti wa Rasilimali za Uvuvi kutoka Taasisi ya Lake Victoria Fisheries Organization (LVFO), anaeleza kuwa Tanzania inapoteza siyo tu fedha, bali pia fursa ya ukuaji wa viwanda, kwani mabondo yanasafirishwa yakiwa ghafi badala ya kusindikwa nchini na kuongeza thamani.
Ukwepaji kodi huu una athari, ikiwemo Serikali za mitaa mkoani Mwanza kukosa bajeti ya kutosha kwa huduma za jamii. Pili, uvuvi haramu unaongezeka kwa sababu watu wanawinda Sangara wakubwa wenye mabondo makubwa, hali inayoharibu uwiano wa samaki ziwani na kutishia usalama wa chakula.
Ili kutatua tatizo hili, makala hii inapendekeza kuianzishwa kwa mfumo wa kufuatilia mabondo kuanzia mwaloni kupitia mfumo wa kidijitali, ili kila bondo lipewe “alama” ya kidijitali kabla ya kuuzwa.
Wizara pia inatakiwa kurekebisha Sheria ya Uvuvi ya 2003, ili Bunge liweke adhabu kali zaidi, ikiwemo kutaifisha vyombo vya usafiri na kufuta vibali vya makampuni ya kigeni yanayojihusisha na biashara haramu.
Mayalu Kasiri, Katibu wa Chama cha Wavuvi Ziwa Victoria anasema Serikali isaidie wavuvi wadogo kuunda ushirika utakaowaruhusu kuuza mabondo moja kwa moja kwenye soko la dunia badala ya kutegemea madalali.

Umaskini unaomkabili mvuvi wa Ziwa Victoria si laana ya asili, bali ni matokeo ya mfumo isiyo rafiki ya kiuchumi, ambayo kwa namna moja au nyingine huwatenga wavuvi wazawa, hasa wadogo. Ziwa Victoria lina uwezo mkubwa wa kuwakomboa wavuvi hao kiuchumi, ikiwa tu utajiri wake utasimamiwa kwa misingi ya usawa, haki, na utu.
Kurejesha haki na mapato ya mvuvi si hisani, bali ni wajibu wa kimaadili na kisheria wa serikali za nchi za Afrika Mashariki. Kwa kuimarisha vyama vya ushirika, kuweka miundombinu ya kisasa ya majokofu, kutoa ruzuku ya vifaa, na kudhibiti madalali wanyonyaji, tunaweza kugeuza mawimbi haya.
Ni wakati sasa kwa mvuvi wa Ziwa Victoria kufurahia matunda ya jasho lake na kushuhudia mabondo yakibadilisha maisha yake, familia yake, na jamii yake kwa ujumla. Ziwa Victoria lisiwe chanzo cha utajiri wa wageni na umaskini wa wenyeji, liwe chemchemi ya maendeleo endelevu kwa kila mvuvi anayelala majini kutafuta riziki.
Suluhisho la biashara ya mabondo kuwanufaisha wavuvi wazawa
Wakati kukionekana ombwe kubwa la faida kati ya wavuvi wazawa, walanguzi na viwanda vya Wachina hapa Tanzania, baadhi ya wavuvi wanaona kuwa mabadiliko ya sheria na sera ni ya muhimu, ili wavuvi wapate faida ya mabondo.
Adrew Misana anasema kuwa ni lazima sasa sheria ibadilishwe ili itambue mabondo kama biashara ya msingi, “Kama bei ya bondo ni sawa au zaidi ya samaki, kwanini tusiseme kuwa bondo ni dhahabu kwenye uvuvi? Sasa serikali inatakiwa itunge sheria kurasimisha biashara ya mabondo ili iweze kujitegemea. Biashara isifanyike kwa wizi. Baishara ifanyike kwa uwazi ili wavuvi wapate faida na serikali ipate kodi,” anasema Misana.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Wavuvi (FUO), Juvenali Mtagili anaona kuwa wazo la kubadilisha sheria ni la msingi.
“Sheria yenyewe inatambua mabondo (fish maw) kama mazao ya ziada by products. Sheria inatambua minofu kama zao la msingi. Ukiangalia kati ya kilo moja ya minofu na kilo moja ya mabonndo kitu chenye thamani ni mabondo. Serikali inaweza kuwa inapoteza mapato kwa kudharau faida halisi na bei ya mabondo katika soko la dunia. Kuna wakati bei ya mabondo huko China ilifika milioni 3 kwa kilo moja,”maoni ya Matagili kuhusu sheria.
Mwandishi: Yohani Gwangway
Mhariri: Dominic Allen


