Na Dominic Allen
Chama cha ACT Wazalendo kimelaani vikali vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu katika operesheni za kuwaondoa kwa nguvu wananchi katika maeneo yao nchini Tanzania.
Katika taarifa iliyotolewa leo na chama hicho imesema kuwa kimesikitishwa na tukio la hivi karibuni la Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupanga kuvifuta vitongoji vya Mahasa na Kabukuyungu katika kijiji cha Kalilani mkoani Kigoma.
ACT Wazalendo imeeleza kuwa serikali kwa kushirikiana na Mamlaka ya Hifadhi ya Mahale imekuwa ikiendesha operesheni za kijeshi kuwaondoa wananchi katika maeneo yao tangu mwaka 2023, jambo lililopelekea watu watatu kupoteza maisha, ambao ni Fedhali Kalabula, Warutundu Kasimu pamoja na Omari Yusufu.
Licha ya serikali kusema kuwa wananchi wa Mahasa na Kabukuyungu katika kijiji cha Kalilani kuwa wameshalipwa fidia zao, lakini kwa mujibu wa ACT Wazalendo kiasi cha Tsh. Bilioni 1.68 iliyotolewa kwa ajili ya kuwalipa fidia wananchi hao iliishia mikononi mwa watu wachache wasiohusika huku walengwa wa fidia hizo kuambulia patupu.
ACT Wazalendo imeitaka serikali kusitisha operesheni za kuwaondoa wananchi kijiji cha Kalilani na maeneo mengine, pamoja na kufanya uchunguzi wa mauaji ya raia, uporaji wa ardhi na uharibifu wa mali za wananchi.
Vilevile imeitaka serikali kuwawajibisha waliohusika na vitendo hivyo vya ukiukaji wa haki za binadamu, kuweka wazi mpango wa matumizi ya ardhi na kuhakikisha kuwa wananchi wanashirikishwa ipasavyo katika kila hatua.
Mwandishi: Dominic Allen
Mhariri: Yohani Gwangway


