Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango leo Disemba 16, 2024 ameitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kukabiliana vyema na vitendo vya rushwa katika Uchaguzi Mkuu wa 2025 na kumwulika zaidi matumizi ya mitandao na simu katika kuhamisha pesa za rushwa.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Viongozi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC), ambapo ameongeza kuwa ni muhimu kujizatiti kupambana na vitendo hivyo vya rushwa ambavyo vina madhara makubwa kwa maendeleo ya Taifa kwa kuwa Viongozi wanaochaguliwa kwa njia ya rushwa hawawezi kukemea vitendo vya rushwa, kutatua kero za wananchi pamoja na kusimamia vema miradi ya maendeleo.
Katika hatua nyingine amewataka viongozi na watumishi wa TAKUKURU kuwa mfano wa kuigwa kwa kuwa na mienendo mizuri, kufuatilia tuhuma mbalimbali kwa umakini na bila upendeleo na kusisitiza umuhimu wa kufanya maamuzi kwa haki na kutumia madaraka kutatua kero za wananchi kwa manufaa ya umma na siyo binafsi.
Makamu wa Rais pia ametoa wito kwa TAKUKURU kuzingatia kufanya kazi kwa misingi ya sheria, kanuni na taratibu, kujituma na kutanguliza maslahi ya Taifa mbele ili taasisi hiyo iwe na ufanisi.
Dkt. Mpango vilevile ametilia mkazo suala la kuimarisha mifumo ya kuchunguza, kuzuia na kuadhibu wanaobainika kujihusisha na vitendo vya rushwa kwa mujibu wa sheria na kuzitaka ofisi zote za TAKUKURU nchini kuunganishwa na mifumo ya TEHAMA pamoja na kuwajengea uwezo na mbinu za kisasa za uchunguzi na uendeshaji wa kesi za rushwa watumishi wa TAKUKURU wanaotekeleza jukumu la kuzuia na kupambana na rushwa.


