Na Yohani Gwangway
Leo inatimia mwaka mmoja tangu kufanyika kwa maandamano ya amani katika Tarafa ya Ngorongoro, huku wakazi wa eneo hilo wakisema kuwa maandamano ya amani mwaka jana yalikuja na ahadi nzuri za serikali ambazo hadi sasa kuna ahadi ambazo hazijatekelezwa.
Katika taarifa kwa Umma iliyotolewa kwa njia ya maandishi na wakazi wa eneo hilo leo Agosti 23, 2025 ambapo wakazi hao wameeleza kuwa maandamano ya mwaka jana yalivutia uamuzi wa serikali katika madai yao ya muda mrefu. Baadhi ya madai hayo yalikuwa ni kurejeshwa kwa huduma za jamii, Mamlaka ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kuacha kutoza tozo kwa magari ya wenyeji na kuchukuliwa hatua kwa waliohusika kuumiza jamii. Sehemu ya taarifa hiyo imesema hakuna yeyote aliyechukuliwa hatua hadi sasa.
“Tuliwataka serikali kuchukua hatua madhubuti kurejesha hali ya kawaida na kuimarisha imani ya jamhuri kwa ajili ya kulinda maslahi ya Wamasai wa eneo la Hifadhi ya Ngorongoro. Madai yetu ilikuwa ni kwamba serikali ichukue hatua za kisheria dhidi ya wale wote walioacha maslahi ya jamii kufanya udhalilishwaji dhidi yetu. Hadi leo, hakuna mtu yeyote aliyewajibishwa juu ya ubaguzi huo mkali dhidi yet,” taarifa iliyotolewa na Wakazi wa Ngorongoro leo.
Matokeo Chanya ya Maandamano
Taarifa hiyo imetaja baadhi ya matokeo chanya ya maandamano ya mwaka jana ikiwa na kubadilishwa juu ya maamuzi ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ambayo awali iliondoa Ngorongoro katika Daftari la Wapiga Kura. Pia taarifa hiyo imesema kuwa Mwakilishi wa jamii hiyo alikutana na Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan mnamo Disemba 01, 2024. Katika mkutano huo Mwakilishi huyo aliwasilisha taarifa ya dhuluma zinazofanywa dhidi ya wakazi wa Ngororongoro
Taarifa hiyo imeeleza kuwa baada ya mkutano kati ya Rais na Mwakilishi wa wakazi wa Ngorongoro, Rais aliunda Tume mbili ambazo zintachunguza mambo yanayoendelea Ngorongoro.
“Kutokana na mkutano huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alianzisha Tume mbili za Urais, ili kuchunguza suala la uhamisho kwenda Msomera na matumizi ya ardhi (katika wilaya yote ya Ngorongoro). Tume hizo zilitembelea maeneo yetu, na sasa tunasubiri kwa hamu ripoti ya,” ilifafanua taarifa ya Wakazi wa Ngorongoro.

Katika hatua nyingine wakazi hao wamesema kuwa Mamlaka ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) imesitisha tozo ya magari ya wenyeji kila siku na badala yake sasa magari hayo yanalipiwa kiasi cha Shilingi za Kitanzania 118,000. Hoja ya wakazi wa Ngorongoro katika jambo hili ni kuwa tozo hii iondolewe kabisa kwa sababu wao siyo watalii.
“Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro imeacha zoezi la kulipa kiasi cha tozo za kila siku kwa magari kwa wakazi wa Maasai ambao si watalii na kurejea mfumo wa zamani wa kulipa 118,000 kwa mwaka. Japo kwa upande wetu bado tunadai kuondolewa kabisa tozo hizi kwa magari ya wenyeji.”
Taarifa ya wakazi wa Ngorongoro imeeleza kuwa maandamano ya amani mwaka jana yamekuwa ni mchoro wazi kwa wengi kuelewa ukweli wa kile walichopitia kwa miaka minne iliyopita kwa kisingizio cha uhifadhi. Kwingineko taarifa inaeleza kuwa matukio yaliyorushwa eneo la Loduare, mlango mkuu wa Hifadhi ya Ngorongoro, yaliyokuwa yakichochea unyanyasaji yamepungua kwa kiasi fulani.
Hali ya Ngorongoro kwa sasa
Taarifa iliyotolewa leo imesisitiza juu ya kuendelea kwa baadhi ya madhila kwa wakazi wa Ngorongoro yakiwemo ya kukosa malisho kwa ajili ya mifugo yao kutokana na kuchomwa kwa baadhi ya maeneo, huku kukiwa na changamoto ya kupata maeneo yenye maji kwa ajili ya mifugo yao.
“Kuanzia Julai 2025 NCAA imeanza kuchoma nyasi katika maeneo ya malisho ambayo kwa kawaida yanatumiwa kwa kulisha mifugo wakati wa kiangazi, kwa lengo la kuwazuia watu kuingia katika maeneo ambayo kisheria yanaruhusiwa.”
Taarifa hiyo ilidai kuwa Mamlaka ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) imeanza kuharibu maeneo ya kunyweshea mifugo, hasa yale yanayoegemea mito isiyo ya kudumu kama njia ya kuwazuia wenyeji kufikia maji wakati wa kiangazi.
Mmoja wa wakazi wa Ngorongoro ameieleza Land Dwellers kuwa kuchomwa kwa maeneo hayo kunawaweka kwenye wakati mgumu wao na mifugo yao.
“Maeneo ya malisho bado ni changamoto, kwa sababu hawa wanaoitwa wahifadhi bado wanaendelea kuchoma maeneo ambayo tunatumia kwa ajili ya malisho. Eneo la Olduvai walichoma juzi, maeneo ambayo yanategemewa kwa ajili ya malisho kipindi cha kiangazi,” amesema mkazi huyo.

Kwa mujibu wa wakazi wa Ngorongoro, bado kuna sintofahamu juu ya kurejeshwa kwa huduma za kijamii kama vile huduma za afya, ambapo ili kupata baadhi ya huduma huwabidi kusafiri hadi Karatu, jambo ambalo ni kinyume na ahadi zilizotolewa mwaka jana na viongozi wa serikali waliomwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, wakati wa kusitishwa kwa maandamano hayo.
“Katika suala la afya, tulitarajia sana mwaka 2020 tulianzisha Jengo la Mama na Mtoto katika Kituo cha Afya cha Nainokanoka.., lakini baada ya hapo tangia hiyo ishu ya Msomera ilipoanzishwa, pesa za wananchi zilizokuwa kwenye akaunti ya Kituo cha Afya cha Nainokanoka zimehamishiwa Msomera. Mpaka leo watu wote wajawazito, wamama, wazee pamoja na watot wanapelekwa Karatu kwa ajili ya kupatiwa matibabu,” amesema Sabore Ngarusi, Mwenyekiti wa Kijiji cha Bulati, Kata ya Nainokanoka.
Wakazi wa Ngorongoro wamebainisha kuwa bado wanakumbana na changamoto ya kupata vibali kwa ajili ya kukarabati miundombinu kama vile majengo ya shule, nyumba za walimu pamoja na zahanati, ambapo wanaohusika na utoaji wa vibali hivyo ni Mamlaka ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA).
“Mimi mwenyewe ni Mwenyekiti wa kijiji, nimejitahidi sana kufuatilia vibali lakini majibu yake hatuna. Katika kijiji cha Bulati kuna vyoo vimejaa, majengo ya nyumba za walimu yanavuja, madarasa yana mashimo. Tulihitaji sana kukarabati majengo chakavu” amesema Ngarusi.
“Kama Zahanati ya Esere kwa kweli ukienda ni ajabu, inavuja, popo wanaishi, hamna kitu kinachoendelea. Shule ya Msingi Ndiani pale Kata ya Endulen bado kuna nyufa hakuna kitu kilichokarabatiwa na hata vyoo vya Shule ya Msingi Endulen hakuna ukarabati” ameeleza Lazaro Morindet, mkazi wa Kata ya Endulen.
Kufuatia madai hayo ya wakazi wa Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, Land Dwellers ilimtafuta Kamishna wa Mamlaka ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Abdul-Razak Badru ili kupata ufafanuzi zaidi, Mhifadhi alituelekeza kwa Hamis Dambaya kutoka Kitengo cha Mawasiliano cha NCAA, ambaye alisema kuwa watatoa ufafanuzi juma lijalo.
Wito wa wakazi wa Ngorongoro kwa serikali
Katika wito wao wakazi wa Ngorongoro wamesisitiza kuwa wakati huu ambapo pande zote mbili zinasubiri ripoti ya Tume zilizoundwa na Rais, ni muhimu vitendo vitakavyozidisha malalamiko vikaepukwa.
“Tunaiomba serikali, wakati tunasubiri matokeo ya Tume hizo mbili za Urais, iache mara moja sera na vitendo vinavyoendelea kukuza malalamiko ya jamii. Tuko tayari kuungana kwa nia njema na serikali ili kuhakikisha matatizo haya yanapata suluhisho la amani.” Wito uliotolewa katika taarifa hiyo.
Kukiwa bado kuna malalamiko ya ukiukwaji wa haki za binadamu dhidi ya wakazi wa Ngorongoro, wameisihi Serikali kuchukua hatua kali dhidi ya ukiukwaji huo, huku wakisisitiza suala la hekima na kuheshimu haki zao.
“ Kama raia wenye dhamana, tunatarajia serikali itarudi kuwa na hekima na kuheshimu haki zetu kama wananchi wengine wa nchi hii. Ni jukumu la serikali kutoa haki na kuchukua hatua kali dhidi ya wale wanaoendelea kuwanyanyasa watu wetu.”
Wakati wito huo ukiisihi serikali kuheshimu haki za wakazi wa Ngorongoro, Lazaro Morindet ambaye ni mkazi wa Kata ya Endulen ameikumbukusha serikali kutimiza ahadi zake ilizotoa mwaka jana wakati wa maandamano hayo ya amani.
“Ningependa kuishauri serikali kwamba makubaliano au ahadi walizozitoa, ni bora wangetimiza, isiwe ni kejeli kwamba walitukejeli baada ya kukaa siku sita porini tukapigwa na baridi, tukapigwa na njaa. Wangetimiza yale,” amesema Morindet.
Naramatisho Kandirisi, mkazi wa Olbabal ameiomba serikali kurejesha huduma za kijamii ikiwemo huduma za afya, kwa kutokana na kukosekana kwa huduma hizo, hulazimika kusafiri hadi Karatu.
“Tunaiomba serikali irudishe huduma zote zilizokuwa zikiendelea Ngorongoro. Mfano, huduma za afya za afya na shule,” wito wa Kandirisi kwa serikali.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mwaka 2022 ilianza rasmi kuwahamisha wakazi wa Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro kuelekea Msomera mkoani Tanga, ambapo miongoni mwa sababu zilizoifanya serikali kuchukua maamuzi hayo ni madai ya kuongezeka kwa idadi ya watu katika eneo hilo la hifadhi, ambao wengi wao ni jamii ya Wamasai, mifugo kuongezeka pamoja na ujenzi wa makazi holela.
Hata hivyo, wakazi wa Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro hawakubaliani na hoja hizo, huku wakiitaka serikali kufahamu kuwa upekee, uzuri pamoja na ustawi wa Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro ni umechangiwa na jamii za watu wa asili.
Mwandishi: Yohani Gwangway
Mhariri: Dominic Allen


