Na Dominic Allen
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima hapo jana akichangia mada kwenye Mkutano wa 69 wa Kamisheni ya Hali ya Wanawake Duniani (CSW69) unaofanyika jijini New York nchini Marekani, amesema kuwa Tanzania imeweka mazingira wezeshi ili kufikia usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake na wasichana.
Dkt. Gwajima ameeleza kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Katiba ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar zinatambua haki, sawa na umuhimu wa ushiriki wa wanawake katika meza za maamuzi.
Wakati akichangia mada kuhusu juhudi ambazo zimefanywa na Tanzania kufikia usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake na wasichana, Dkt. Gwajima ameongeza kuwa zipo Sera na Sheria mbalimbali ambazo zimekuwa zikichagiza kufikia malengo hayo.
Miongoni mwa Sera hizo ni ‘Sera ya Taifa ya Jinsia na Maendeleo ya Wanawake ya Mwaka 2023’ na ‘Sera ya Jinsia ya Zanzibar ya Mwaka 2016-2020’ inayofanyiwa mapitio, ‘Sera ya Taifa ya Biashara’ inayohakikisha usawa wa kijinsia kwenye biashara, pamoja na ‘Sera ya Taifa ya Elimu na Mafunzo (2014) toleo la mwaka 2023’ inayohakikisha watoto wote bila kujali jinsia au umri wanahitimu elimu na mafunzo.
Dkt. Gwajima pia amezungumzia Mkakati wa Pili wa Mfumo Jumuishi wa Fedha, ambao unatoa kipaumbele kwenye masuala ya wanawake pamoja na Kamati ya Wanawake kwenye Benki Kuu ya Tanzania.
Kwa upande wa sheria, amegusia Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa inayotaka mamlaka hizo kutenga 10% ya mapato ya ndani kwa ajili ya mikopo isiyo na riba kwa Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu, pamoja na sheria zingine.
Dkt. Gwajima amesema serikali inahakikisha takwimu za maendeleo zinazokusanywa, zinafanyiwa uchambuzi wa kijinsia kwa ajili ya matumizi yenye kusukuma maendeleo yenye usawa wa kijinsia.
Vilevile, amesisitiza juu ya ushiriki wa wadau mbalimbali wa maendeleo ili kuhakikisha Tanzania inafikia usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake na wasichana.
Mwandishi: Dominic Allen
Mhariri: Yohani Gwangway


