Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Kisultan ya Oman, zimetia saini Mkataba wa Kuondoa Utozaji Kodi ya Mapato Mara Mbili na Kuzuia Ukwepaji Kodi, ujulikanao kama ‘Agreement for the Elimination of Double Taxation with Respect to Taxes on Income and Prevention of Tax Avoidance and Evasion’.
Mkataba huo umesainiwa mjini Mascut, Oman na Waziri wa Fedha wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, na Mwenyekiti wa Mamlaka ya Mapato ya Oman, Bw. Nasser Al-Jashmi.
Dkt. Nchemba amesema kuwa kusainiwa kwa mkataba huo ni hatua muhimu kwani itafungua uchumi wa nchi kwa kuvutia uwekezaji wa kimataifa.
Ameongeza kuwa mkataba huo utawezesha wawekezaji na wafanyabiashara wanaofanya shughuli kati ya Tanzania na Oman kutozwa kodi mara moja pekee badala ya kutozwa mara mbili kwa mapato ya aina moja, hali ambayo awali ilikuwa ni kikwazo kwa ustawi wa biashara kwa pande zote mbili.
Dkt. Nchemba amesema mkataba umelenga kuvutia uwekezaji wa mitaji mikubwa kutoka Oman kuja kuwekeza Tanzania, hususan kupitia kampuni kubwa zinazomilikiwa na familia za kifalme, sambamba na wawekezaji binafsi ambapo kupitia uwekezaji huo Tanzania inatarajia kunufaika na ukuaji wa sekta za uzalishaji, maendeleo ya viwanda, na kuongezeka kwa ajira kwa wananchi.
Kusainiwa kwa mkataba huo kunawawezesha wawekezaji wa Kitanzania kuwekeza nchini Oman bila vizuizi vya kikodi, huku wakilindwa na mkataba huo ili kuepusha kulipishwa kodi mara mbili.
Hatua hiyo pia inatoa fursa kwa wafanyabiashara wa Tanzania kupanua shughuli zao katika masoko ya kimataifa, hasa katika ukanda wa Ghuba.


