Na Amiri Kilagalila
Watumishi wawili wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa mkoani Njombe waliokuwa kwenye Kamati ya Ukusanyaji wa Mapato, wamefutwa kazi mara baada ya kubainika kujihusisha na vitendo vya wizi na rushwa vilivyosababisha hasara kwa mwajiri ya zaidi ya shilingi za kitanzania milioni 13.
Uamuzi huo umetolewa jana Juni 18, 2025 na Baraza la Madiwani Ludewa baada ya kikao maalum kilichojadili masuala ya nidhamu kwa watumishi wa umma, ambapo limefikia uamuzi wa kuwachukulia hatua kali watumishi hao ni Ezekia Mligo na Peter Alphonce kwa kujihusisha na vitendo vya ukiukaji wa maadili, wizi na rushwa.
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Wise Mgina amesema hatua za kinidhamu pia zimechukuliwa kwa watumishi wengine wawili Anuciata Mapunda pamoja na Obothe Msemakweli, ikiwemo kukatwa 15% ya fedha kwenye mishahara yao kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo kama sehemu ya kuwajibika kwa uzembe uliopelekea hasara kwa halmashauri hiyo.

Nae Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Olivanus Thomas amesema watumishi wa umma wanapaswa kuwajibika kwa mujibu wa kanuni, taratibu na sheria za utumishi wa umma, huku akisisitiza kuwa halmashauri hiyo haiwezi kufumbia macho ubadhilifu.
“Hakuna mtumishi wa Ludewa, kuna watumishi wa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania” alisema Olivanus Thomas.

Kwa upande wao baadhi ya madiwani wakiongozwa na Diwani wa Kata ya Ludewa Mjini, Bi. Monica Mchiro, waliwataka watumishi wote wa halmashauri hiyo kuwa waadilifu na kuzingatia maadili ya kazi zao, ili kujenga imani kwa wananchi na kuchochea maendeleo ya wilaya.
Mwandishi: Amiri Kilagalila
Mhariri: Dominic Allen


