Na Amiri Kilagalila
Mafundi ujenzi mkoani Njombe wameiomba Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuliangalia upya kundi hilo liweze kupata bima za afya, ili kuwa na uhakika wa afya zao pindi wanapokutana na changamoto kazini.
Wakizungumza na Land Dwellers katika mkutano uliyofanyika Njombe Mjini, Septemba 23, 2025 ambao uliwakutanisha mafundi hao kujadili masuala ya usalama wao kazini, baadhi ya mafundi akiwemo Victor Mahenge ambaye ni fundi rangi kutoka Halmashauri ya Mji wa Makambako pamoja na Maria Kionaomela kutoka Njombe Mjini, wamesema mafundi wamekuwa wakifanya mambo makubwa kwenye sekta ya ujenzi lakini wanakumbana na changamoto za kiafya pindi wanapokuwa wakitekeleza majukumu yao.
“Mafundi wengi tunapata changamoto kazini lakini inakuwa ni siri yetu ila tukipata bima zitatusaidia kwa maana hata tukipata shida kwenye ufundi itakuwa rahisi kupata huduma ya afya,” amesema Mahenge.

Kwa upande wake Maria Kionaomela ameeleza kuwa kutokana na kipato kidogo wanachokipata, bima za afya zitakuwa na msaada mkubwa katika maisha yao ya kila siku.
“Tunaumwa, umoja unakuwa hakuna lakini pia na kipato ni kidogo, ila tukiwa na bima itakuwa ni msaada mkubwa kwetu” ameeleza Kionaomela.
Kwa kuona umuhimu wa kundi hilo la vijana linalojishughulisha ili kukuza uchumi pamoja na maendeleo ya taifa, sekta binafsi zimeanza kutoa bima za afya kwa lengo la kuunga mkono juhudi za serikali katika kuimarisha sekta ya afya na kuwaletea maendeleo Watanzania.
Derick Mmasi ambaye ni mwakilishi kutoka Magic Builders International Ltd mara baada ya kuwa na mkutano wa pamoja na mafundi wa mkoa wa Njombe, amebainisha kuwa watatoa bima za afya kwa mafundi 500 nchini, ili kuwapa uhakika wa maisha.
“Kwa mwaka huu tunaenda kugawa bima kwa mafundi 500, kwa sababu ni jamii ambayo inafanya kazi katika mazingira hatarishi na mkakati wetu ni kuendelea kutoa bima zaidi ya 500” amesema Mmasi.

Mwandishi: Amiri Kilagalila
Mhariri: Dominic Allen


