Na Dr. Bravious Kahyoza
Sekta ya ufugaji nchini Tanzania imepata mabadiliko makubwa chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, hasa katika uwanda wa mauzo ya nyama nje ya nchi. Mabadiliko haya yametokana na mikakati bora ya kufungua masoko ya kimataifa, ambapo mauzo ya nyama yameongezeka kutoka tani 1,774 mwaka 2020/21 hadi tani 14,701 mwaka 2025.
Mafanikio haya, yalitajwa na Rais Samia katika hotuba yake ya kuhitimisha shughuli za Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Juni 27 2025, na kudhihirisha mafanikio makubwa kwenye sekta ya uvuvi chini ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita.
Itakumbukwa kuwa kabla ya utawala wa Rais Samia mwaka 2021, Tanzania ilikuwa na utendaji wa kiwango cha chini katika mauzo ya nyama nje ya nchi. Wakati huo, nchi ilikuwa inauza tani 1,774 za nyama kwa thamani ya dola za Marekani milioni 4.2, sawa na Shilingi bilioni 10.92.
Ingawa hii ilikuwa ni hatua ya maana, mauzo haya yalikuwa chini sana ikilinganishwa na uwezo mkubwa wa sekta ya ufugaji nchini. Changamoto za kimsingi zilizokuwa zinazuia ukuaji wa sekta hii ni pamoja na upungufu wa masoko ya kimataifa yaliyokuwa ya uhakika, miundombinu dhaifu ya usindikaji wa nyama, na mifumo duni ya usafirishaji wa nyama kwa mazingira ya baridi.

Mafanikio ya kipekee mwaka 2025
Kufikia mwaka 2025, juhudi za Rais Samia za kufungua masoko ya nyama nje ya nchi zimezaa matunda makubwa ambayo yamestawisha watanzania wengi. Mauzo ya nyama yameongezeka kwa kiwango cha ajabu hadi tani 14,701, zenye thamani ya dola za Marekani milioni 61.4, sawa na Shilingi za Kitanzania bilioni 159.64.
Ongezeko hili linawakilisha mara nane ya mauzo ya mwaka 2020/21, jambo ambalo linaonyesha maboresho ya kimsingi katika sekta ya ufugaji. Mauzo haya makubwa yamekuwa yakitokana na ufunguzi wa masoko ya kimataifa, hasa katika nchi za Mashariki ya Kati, Asia, na pia baadhi ya nchi za Afrika.
Mikakati ya Serikali kuimarisha Sekta ya Ufugaji
Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia imepanga na kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuimarisha sekta ya ufugaji na kuongeza mauzo ya nyama nje ya nchi.
Mojawapo ya mikakati muhimu zaidi ni kufungua masoko ya kimataifa kupitia diplomasia ya kiuchumi. Serikali imefanya makubaliano ya biashara na nchi za nje, hasa nchi za Ghuba kama Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Qatar, ambazo zimekuwa wateja wakuu wa nyama ya Tanzania.
Mbali na hayo, Serikali imewekeza kiasi kikubwa katika maboresho ya miundombinu ya usindikaji wa nyama. Uongozi wa Rais Samia umeanzisha viwanda vya usindikaji wa nyama vya kisasa na mifumo ya usafirishaji baridi (cold chain) ili kuhakikisha nyama inawafikia wateja katika hali salama na ya ubora wa juu. Hatua hii imekuwa muhimu katika kukidhi mahitaji ya masoko ya kimataifa.
Kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Serikali imetoa mafunzo ya kisasa kwa wafugaji kuhusu mbinu za ufugaji wa kisasa. Mafunzo haya yamejumuisha mbinu za uchukuzi wa mifugo, njia za kumudu magonjwa, na mbinu za kuboresha uzalishaji wa nyama. Serikali pia imeanzisha mifumo ya usimamizi wa ubora wa nyama, ikiwa ni pamoja na vyeti vya kimataifa vya ubora, ili kuhakikisha nyama ya Tanzania inakidhi viwango vya masoko ya kimataifa.
Sekta ya Ufugaji na maendeleo nchini Tanzania
Ongezeko la mauzo ya nyama hadi tani 14,701 na thamani ya Shilingi bilioni 159.64 limechagia katika maendeleo ya uchumi wa Tanzania. Mapato ya dola za Marekani milioni 61.4 yameimarisha hazina ya fedha za kigeni, ambazo zimewezesha Serikali kuwekeza katika miradi ya maendeleo kama miundombinu, afya, na elimu. Hii imekuwa ni mchango mkubwa katika kuimarisha uchumi wa nchi kwa jumla.
Wafugaji wa ng’ombe, mbuzi, na kondoo wamepata faida kubwa kutokana na ongezeko la soko la nyama. Jambo hili limeboresha maisha yao ya kiuchumi na kuwapa uwezo wa kuwekeza katika kilimo, biashara, na elimu kwa watoto wao.
Sekta ya nyama pia imechangia ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja, ikiwa ni pamoja na wafanyakazi katika viwanda vya usindikaji, usafirishaji, na biashara za nyama. Hii imechangia kupunguza kiwango cha ukosefu wa ajira nchini.
Mikoa yenye wafugaji wengi kama Arusha, Manyara, Shinyanga na Dodoma imepata maendeleo ya kiuchumi kutokana na ongezeko la mauzo ya nyama, ambapo maendeleo haya yamechangia kupunguza umaskini vijijini na kuimarisha uchumi wa mikoa hiyo.
Mikakati ya Serikali kutatua changamoto katika Sekta ya Ufugaji
Licha ya mafanikio haya makubwa, sekta ya ufugaji bado inakabiliwa na changamoto kadhaa ambazo zinahitaji umakini wa ziada. Magonjwa ya mifugo, gharama za juu za usindikaji wa nyama, na hitaji la kuimarisha miundombinu ya usafirishaji ni baadhi ya changamoto hizo. Serikali inalenga kushughulikia changamoto hizi kwa kuimarisha huduma za mifugo kupitia kliniki za mifugo na chanjo za wanyama.
Serikali pia inalenga kuwekeza zaidi katika viwanda vya usindikaji wa nyama vya kisasa na kuendelea kufungua masoko mapya ya kimataifa kupitia makubaliano ya biashara. Lengo la Serikali ni kuongeza mauzo ya nyama hadi kufikia tani 20,000 na thamani ya dola za Marekani milioni 100 ifikapo mwaka 2030.
Juhudi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kufungua masoko ya nyama nje ya nchi zimebadilisha kabisa sekta ya ufugaji nchini Tanzania. Mafanikio haya ya kuongeza mauzo ya nyama kutoka tani 1,774 mwaka 2020/21 hadi tani 14,701 mwaka 2025, na thamani ya Shilingi za Kitanzania bilioni 159.64, yameonyesha uongozi bora na mikakati sahihi ya kiuchumi.
Mbali na hayo, pia yameimarisha uchumi wa wafugaji, yameongeza fedha za kigeni, na yamechangia maendeleo ya kiuchumi ya taifa kwa jumla. Serikali imeendelea na maboresho ya miundombinu na uhamasishaji wa masoko ya kimataifa, ambapo sekta ya ufugaji inategemewa katika kukuza uchumi wa Tanzania.
Mwandishi: Dr. Bravious Kahyoza
Mhariri: Dominic Allen


