Na Dominic Allen
Waziri wa Afya, Jenista Mhagama ametoa wito kwa wadau mbalimbali kuendelea kuiunga mkono Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika masuala ya urutubishaji wa vyakula nchini, ili kuhakikisha vyakula vinakuwa na vitamini zote zinazohitajika katika makuzi ya watoto na jamii kwa ujumla.
Waziri Mhagama amezungumza hayo jana Agosti 14, 2025 akiwa jijini Dar es Salaam wakati akipokea gari iliyotolewa na Shirika la SANKU kwa Wizara ya Afya, ambalo litasaidia katika masuala ya usafiri ili kufikia malengo ambayo Taifa limejiwekea kwenye urutubishaji wa vyakula nchini.
“Eneo kubwa ambalo nadhani kama Serikali tuendelee kusaidiana kwa karibu, tunahitaji sana zile mashine zinazotumika kuchanganyia virutubishi kwa wazalishaji wa chakula. Kuongeza virutubishi kwenye chumvi, kwenye mafuta ya kula, kwenye unga wa ugali, lakini kuongeza virutubishi kwenye unga wa ngano, na hizo ndizo nafaka ambazo zinatumika kwa kiasi kikubwa,” amesema Waziri Mhagama.
Mbali na uhitaji wa mashine za kurutubisha vyakula, Waziri Mhagama pia amesisitiza kuwa bado kuna umuhimu wa kuendeleza ushirikiano kati ya Serikali na wadau kufanikisha upatikanaji wa vifaa ikiwa ni pamoja na vyombo vya usafiri.

Aidha, Waziri Mhagama amebainisha maeneo matatu ya muhimu ambayo Wizara ya Afya imekuwa ikiyatilia mkazo linapokuja suala la urutubishaji wa vyakula ili kufanikiwa katika mapambano dhidi ya utapiamlo, hasa kwa watoto wadogo, wajawazito pamoja na wasichana walio kwenye rika balehe ambao wanaandaliwa kuwa wazazi.
“Kwetu sisi kama Wizara na Serikali, maeneo yafuatayo ndiyo maeneo ya msingi na muhimu sana. Jambo la kwanza ni usalama wa aina ya virutubishi vitakavyotumika nchini, eneo la pili, vinapatikanaje na kwa muda gani, lakini eneo la tatu, vinalenga kurutubisha nini kwa kuzingatia mahitaji ya nchi yetu,” ameeleza Waziri Mhagama.
Vilevile, Waziri Mhagama amesema kuwa urutubishaji wa vyakula utasaidia kuwa na jamii ya watoto wawe na ukomavu wa akili, kupunguza vifo vya watoto wachanga pamoja na vifo vya uzazi, ambapo pia amesisitiza juu ya kutumia vyakula vya asili vyenye ubora unaolingana na virutubishi vinavyotumika kurutubisha vyakula.
Mwandishi: Dominic Allen
Mhariri: Yohani Gwangway


