Na Yohani Gwangway
Mifuko ya Plastiki ambayo imepigwa marufuku nchini Tanzania mwaka 2019, imerejea kwa kasi kubwa sana katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Mwanza. Wananchi wanaotoka masokoni na wengine wanaununua bidhaa madukani wanaonekana kubeba mifuko hii huku uchafuzi wa mazingira ukiongezeka jambo linalohatarisha afya zao.
Matumizi ya mifuko hii katika kutunzia vyakula vya moto imeongezeka katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Mwanza. Katika nyakati za asubuhi wanafunzi wanaoenda shule hufungiwa vyakula kama chapati, maandazi, vitumbua na mihogo ikiwa bado ya moto, huku katika maeneo ya migahawani mama lishe hutumia mifuko ya plastiki kuhifadhia ugali wa moto na vyakula vingine. Hali hii inaelezwa na wataalamu kuhatarisha afya za watumiaji kwani ufungaji wa vyakula vya moto katika mifuko hii huweza kusababisha saratani.
Katika sehemu ya kwanza tunaangazia jinsi usambazaji, uuzaji na matumizi ya mifuko hii ilivyoshamiri katika Jiji la Mwanza licha ya katazo la serikali na kanuni ya usimamizi wa katazo hilo.
Uzalishaji wa Mifuko ya Plastiki
Kuongezeka kwa matumizi ya mifuko ya plastiki katika Jiji la Mwanza ni ishara kuwa kuna uzalishaji wa mifuko hii aidha ndani ya nchi au nje ya nchi. Katika uchunguzi uliofanyika, mifuko hii inazalishwa hapa Tanzania katika baadhi ya viwanda bubu, huku mingine ikiingizwa kutoka nchi jirani hasa Uganda.
Baadhi ya wafanyabiashara waliohojiwa katika makala hii walieleza kuwa wale wanaojihusisha na biashara ya mifuko kwa kiasi kikubwa huenda moja kwa moja katika baadhi ya nchi jirani na kuja kuuza katika soko la ndani kutokana na faida inayopatikana. Taarifa zingine kutoka kwa wasambazaji ni kuwa kuna viwanda vya ndani vinavyozalisha mifuko hii kwa kificho licha ya marufuku ya serikali.
Kanuni za Usimamizi wa Mazingira za Kupiga Marufuku Mifuko ya Plastiki za Mwaka 2019, kifungu cha 5, kimeweka katazo la kuingiza, kusafirisha nje ya nchi, kutengeneza, kuuza, kutunza na kusambaza mifuko ya plastiki kutokana na athari zake katika mazingira.

mbalimbali. Picha na Yohani Gwangway
Meneja wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Kanda ya Ziwa Victoria, Jerome Kayombo anasema kuwa wamewahi kukamata kiwanda kimoja cha uzalishaji jijini Mwanza katika eneo la Kisesa huku wakibandika nembo inayoonesha kuwa mifuko imezalishwa Uganda.
“Binafsi nimewahi kukamata kiwanda Mwanza ambacho kilikuwa kina mifuko ya Nembo ya Uganda. Kwa hiyo kuhitimisha moja kwa moja kuwa inatoka Uganda siyo sahihi, lakini usahihi ni kwamba ile mifuko ina nembo ya Uganda. Ninasema hivyo kwa sababu nina tukio ambalo limetokea Kisesa tu hapo ambapo mtu ana kiwanda chake bubu na ana mashine zake ambazo anaweka nembo ya Uganda” Alielezea Kayombo, Meneja wa NEMC Kanda ya Ziwa Victoria.
Katika hatua nyingine Kayombo anasema kuwa watu waliokamatwa kwa makosa ya kuzalisha na makosa mengine yanayohusiana na mifuko ya plastiki walifikishwa katika vyombo vya sheria.
Kayombo alipoulizwa endapo ana taarifa kuwa mifuko inaingizwa kutoka Uganda, alisema anajua kuwa kuna watu ambao wanavunja sheria kuingiza mifuko hii kutoka nje ya nchi lakini hawezi kusema moja kwa moja kuwa mifuko yote inatoka Uganda.
Juhudi zetu za kujua ukweli ziliwafikia baadhi ya waandishi wa habari wa Uganda ambao walitumiwa picha na majina ya makampuni ya mifuko ambayo ipo mitaani na walithibitisha baadhi ya viwanda ambavyo vinazalisha mifuko hiyo nchini mwao. Hii inathibitisha kuwa baadhi ya mifuko inaingizwa kutoka nchini Uganda. Mifuko hiyo ikiwa na nembo for industrial use only yaani “kwa ajili ya matumizi ya viwanda tu”.
Lakini ushahidi wa kuonesha haya bado ungalipo. Miaka miwili iliyopita, yaani mwaka 2021, Jeshi la Polisi jijini Mwanza lilikamata shehena ya magunia 40 ya mifuko hii kutoka Uganda. Baadaye aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Suleiman Jaffo alipongeza umakini wa Jeshi la Polisi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa kumkamata mfanyabiashara aliyeingiza shehena hiyo kutoka Uganda.
Mwaka 2024, shehena nyingine ya magunia 80 yenye mifuko ya plastiki milioni 11,200,000 ilikamatwa na kuripotiwa na The Chanzo hapa jijini Mwanza.
Miongoni mwa chapa ya makampuni yaliyowahi kukamatwa jijini Mwanza ni PACHA Investment Limited, Twin Source Agro Limited kutoka Wankulukuku Kampala. Mifuko mingine inaonekana kuzalishwa na kampuni ya Toco and CO Limited kutoka hapa hapa Tanzania.

Shirika la International Union for Conservation of Nature (IUCN) kwa kushirikiana na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) pamoja na Life Cycle Initiative mnamo January, 2021 walitoa ripoti yenye jina la National Guidance for Plastic Pollution Hotspotting and Shaping Action ambayo ilichunguza hali la uchafuzi wa mazingira utokanao na plastiki nchini Tanzania.
Ripoti inaonesha kuwa kwa mwaka 2018, tani 315,000 taka za plastiki zilizalishwa nchini Tanzania, ambapo katika mwaka huo takriban tani 29,000 za taka za plastiki ziliingia kwenye bahari, mito na maziwa nchini Tanzania.
Kwa mujibu wa Shirika la Mazingira ya Umoja wa Mataifa (UNEP), takriban tani milioni 460 za plastiki huzalishwa kila mwaka, ambapo theluthi mbili ya uzalishaji huo ni kwa ajili ya bidhaa za muda mfupi hivyo huishia kuwa takataka. Miongoni mwa bidhaa hizi za platiki ni mifuko ya plastiki.
Uingizwaji
Jiji la Mwanza linaonekana kufikika kirahisi na nchi zote za Afrika Mashariki katika biashara haramu ya mifuko ya plastiki. Ripoti yenye jina ‘Illegal Trade and Smuggling of Plastic Bags in the East African Bloc’ iliyotolewa mwaka 2022 na Shirika la Nipe Fagio (Tanzania) kwa kushirikiana Bio Vision (Uganda), Global Initiative for Environment & Reconciliation (Rwanda) na Kituo cha Haki na Maendeleo ya Mazingira (Kenya) ilionesha kuwa baadhi ya mifuko hii huingizwa kutoka Uganda.
Je, uingizwaji unafanyikaje?
Land Dwellers imefanya uchunguzi wa kina na kubaini mnyororo biashara ya mifuko ya plastiki kuanzia uzalishaji wake hadi kuwafikia watumiaji wa mwisho ambao ni wananchi.
Mnyororo wa mifuko ya plastiki huanzia kwenye viwanda bubu vilivyopo ndani na nje ya nchi ambavyo huzalisha mifuko hii, na baada ya hapo huchukuliwa na wafanyabiashara wakubwa na kuisambaza katika maduka ya makubwa na sehemu zingine ambazo hutumika kwa ajili ya kuhifadhia mifuko hii.
Maduka makubwa huwauzia wasambazaji wadogo wadogo wa mifuko ya plastiki ambao hutumia usafiri wa baiskeli, pikipiki na mabegi ya migongoni kusambaza katika maduka ya rejareja, masokoni na mitaani.
Kutoka kwenye maduka ya rejareja, masokoni na mitaani hapo ndipo huelekea kwa watumiaji wa mifuko hii ambao ni wananchi. Mifuko hutumika kubebea bidhaa madukani, vyakula migahawani na kwa matumizi mengine.

Katika kufanya biashara hii, kumekuwa na mbinu nyingi ambazo hutumika kuingiza mifuko ya plastiki kutoka nje ya nchi. Kwa mujibu wa mahojiano na msambazaji (ambaye yeye siyo mwingizaji), mifuko hupita katika mipaka isiyo rasmi huku wakati mwingine ikipita katika Ziwa Victoria bila mamlaka kuwa na taarifa.
Meneja wa NEMC kanda ya Ziwa Victoria anasema kutokana na jiografia ya Jiji la Mwanza, baadhi ya wafanyabiashara wanaingiza mifuko hii kupitia ziwani jambo linaloleta ugumu kutambua kama ni wavuvi au ni wavunja sheria.
“Jiji letu lina Ziwa Victoria na kuna shughuli nyingi zinafanyika ziwani, huwezi hata kufahamu wakati mwingine unaweza kuona mtumbwi kumbe unasafirisha mifuko ya plastiki” Kayombo, NEMC.
Uhifadhi
Biashara ya mifuko ya plastiki inaonesha aina mpya ya uvunjifu wa sheria hasa katika utekelezaji wake. Katika kufanya uhifadhi kwa mifuko ambayo tayari imezalishwa na kuingizwa hapa nchini, wafanyabiashara hawa wanatumia mahoteli, nyumba za kuishi, nyumba ambazo bado zinajengwa na maeneo mengine kama sehemu ya kuhifadhia.
Wakati akijibu mbinu zinazotumika kuhifadhi mifuko hii, Meneja wa NEMC Kanda ya Ziwa Victoria alisema kuwa watu wamekuwa wakitumia mbinu mbalimbali katika kuhifadhi mifuko hii.
“Tumekamata mifuko kwenye nyumba ya kawaida ya kuishi, tumekamata kwenye mahoteli, kuna hoteli tulikamata robota zaidi ya 40, kesi nyingine tulikamata mifuko kwenye kiwanja cha mtu kimezungushiwa kuna kibanda cha walinzi, wewe ukipita nje unasema hii ni site (eneo) ya mtu anakuja kujenga, lakini usiku watu wanafanya biashara” Meneja Kayombo
Licha ya maelezo haya kutoka NEMC katika uchunguzi wetu na mahojiano na baadhi ya wasambazaji, tumegundua kuwa kwa sasa katika Jiji la Mwanza baadhi ya wauzaji wa mifuko mbadala maarufu kama mifuko ya Magufuli, ndiyo wanaohusika kusambaza mifuko plastiki. Baadhi ya maduka haya huficha mifuko ya plastiki na kuonesha kana kwamba wanauza mifuko iliyoruhusiwa ili wasigundulike kirahisi.
Uuzaji na Usambazaji wa Mifuko ya Plastiki jijini Mwanza.
Katika Jiji la Mwanza mifuko ya plastiki inasambazwa kutoka kwenye maduka au maeneo ya uhifadhi kwa kutumia aina nyingi za wasambazaji ili kuwafikia wanunuzi ambao wapo maeneo ya dukani na masokoni. Baadhi ya njia ambazo zinatumika ni pamoja na kutumia pikipiki kusambaza, kutumia baiskeli pamoja na matumizi ya vijana ambao hubeba mabegi migongoni kama Wamachinga kumbe ni wasambazaji.
Mahojiano yaliyofanyika na watu ambao wanafanya usambazaji kwa kutumia baiskeli yalionesha watu hawa ambao baadhi yao husambaza mikate na bidhaa za madukani ndiyo wamekuwa kiungo muhimu katika kutoa mifuko ya plastiki kwa wauzaji wa jumla na kusambaza kwa maduka moja moja au maeneo ya masokoni.
Ahmed ambaye si jina halisi, yeye ni msambazaji ambaye anafanya usambazaji kwa kutumia baiskeli huku akilenga wanunuzi ambao wana maduka.
“Mimi ninafuata mzigo (mifuko) mjini. Wauzaji wa pale mjini wametukariri sisi ambao ni wasambazaji. Wakiona sura mpya hawawezi kuuza. Maduka mengi ni yale ambayo huuza mifuko ya kawaida au bidhaa za madukani”. Alisema Ahmed ambaye ni msambazaji wa mifuko.
Watumiaji waliozungumza walitaja kuwa mifuko hii inauzwa na kusambazwa na watu wenye baiskeli au pikipiki ama wakati mwingine wakikosa hao wasambazaji wao hufuata madukani
“Hii mifuko sisi tunanunua kwa hao wanaotembeza. Unakuta wengine wana baiskeli na wengine wana pikipiki. Tukikosa kwa hao tunafuata madukani”. Maelezo ya mama lishe katika eneo la Nyamalango
Baadhi ya njia zinazotumika kusambaza mifuko hii zimekuwa nyingi kwa mujibu wa watu mbalimbali. Baadhi ya njia hizi ni magari, maboti, mabasi ya abiria pamoja na magari maalum kwa ajili ya usafirishaji.
“Tumekamata mifuko kwenye mabasi, kwenye magari yakiwa yanasafirishwa. Tumekamata mpaka kwenye magari ya samaki, wewe unajua kuwa ni samaki kumbe huko ndani ni mifuko ya plastiki, tumekamata maboti, kwa maana nyingine ninachokuambia ni kuwa route (njia) siyo ya aina moja, ziko za aina nyingi na zinahitaji ushirikiano”. Meneja wa NEMC Kanda ya Ziwa Victoria akieleza mbinu zinazotumika katika usafirishaji wa mifuko ya plastiki.
Utumiaji
Baada ya mifuko hii kuingia katika maeneo ya masoko na maduka ya kawaida, mifuko hii inakuwa haiuzwi tena bali hutumika kama vifungashio kwa bidhaa mbalimbali. Katika maeneo ya masoko hufungiwa nafaka, matunda au bidhaa nyingine wakati katika maeneo ya madukani hufungiwa bidhaa mbalimbali.
Utumiaji wa mifuko ya plastiki iliyopigwa marufuku siyo suala linalofanyika kwa kificho, masokoni, madukani na maeneo ya migahawani mifuko hii inaonekana kutapakaa.
Katika mazungumzo na baadhi ya wakazi wa Jiji la Mwanza, inaonekana wazi kuwa mifuko ya plastiki hutumika kama vifungashio huku ikitumika katika maeneo ya migahawa kubebea chakula. Rajabu Khamis ni mkazi wa Buhongwa, yeye anaeleza maeneo ambayo mifuko hii inatumika
“Mifuko hii meupe mara nyingi sana naiona. Lakini ile mifuko meusi na bluu kwa sasa hivi haionekani. Maeneo ambayo naona mifuko hii meupe (transparency) inaonekana ni kama madukani ukinunua kitu, mahotelini mama ntilie wanatumia kufungia chakula na maeneo ya site (maeneo ya kazi za ufundi), hayo ni maeneo ambayo mimi ninaiona.” Alieleza Rajabu Khamis, mkazi wa Buhongwa.
Maeneo ambayo mifuko hutumika
Masoko
Katika masoko makubwa ya jiji la Mwanza kama Soko la Kirumba, Buhongwa na Mirongo, matumizi ya mifuko ya plastiki ambayo hutumika kama vifungashio yameshamiri. Mifuko hii inaonekana ikifungiwa bidhaa mabalimbali katika masoko kama vile nyanya, matunda na nafaka za aina mbalimbali.
Katika mahojiano maalum ambayo yalifanyika na wafanyabiashara wa masoko haya, ilionekana kuwa kuna uelewa mdogo juu ya mifuko gani imepigwa marufuku. Mariam Said ni mfanyabiashara katika soko la Buhongwa ambaye anasema mifuko iliyopigwa marufuku siyo hii inayoonekana.
“Sidhani kama mifuko hii ndiyo ilipigwa marufuku. Sisi hapa tuliacha kutumia ile mifuko iliyopigwa marufuku na sasa hivi tunatumia hii mifuko ya Magufuli (Mifuko mbadala) pamoja na hii meupe ambayo ni kama tu vifungashio.” Alisema Mariam
Kwa wafanyabiashara wengine ambao walijaribu kueleza uelewa wao ilionekana hawaelewi kama kuna tatizo la kutumia mifuko hii huku wengine wakionekana kujua kuwa imepigwa marufuku lakini wanaitumia kwa sababu ipo.

Katika nyakati za asubuhi ambapo usafi hufanyika katika masoko ya Jiji la Mwanza, tumeshuhudia kwa nyakati tofauti mifuko hii ikiwa miongoni mwa taka zilizopo. Mifuko plastiki yenye rangi za bluu ambayo kwa kawaida huwa ni migumu pia ilionekana. Mifuko hii hujulikana kama “Malboro” kwa wafanyabiashara wengi.
Jambo hili liliongeza udadisi wa kujua kama mifuko hiyo imeanza kutumika upya ambapo tumeshuhudia mifuko hii ikiwa kwa mfanyabiashara mmoja. Baada ya kufahamu jambo hili, tulimtafuta Mwenyeki wa soko la Buhongwa Ndugu Sylvester Kadoya Makoye kujua kwa nini kuna matumizi ya mifuko hii katika eneo lake.
“Mimi niseme tu kwangu binafsi, siwezi kuzuia kwa sababu mifuko ipo na inatumika kwa sasa sijui inapotokea mimi, lakini ipo kwa wafanyabiashara wangu. Labda serikali kuu itengeneze tu mbinu kuziba kwenye shina lake inapotekea (chanzo) kwa sababu ipo inatumika kweli” Alijibu Makoye

Wauzaji katika maduka
Katika maduka mbalimbali katika Jiji la Mwanza mifuko ya plastiki inatumika kwa kiwango kikubwa. Katika maduka 50 yaliyotembelewa na Land Dwellers kama sehemu ya kujua kiwango cha matumizi, maduka 45 yalikuwa na mifuko hii.
Kwa wamiliki au wauzaji wa maduka mifuko hii inatumika kufungia bidhaa mbalimbali kama karanga, sabuni, mchele, unga, mafuta maharage na nyinginezo. Katika mazungumzo na Land Dwellers asilimia kubwa ya wamiliki wa maduka walionesha kufahamu kuwa mifuko hii imepigwa marufuku lakini walidai wanaitumia kwa sababu wateja wanahitaji na pia ni bure, kama ni mifuko mingine mteja anatakiwa anunue.
“Kusema ukweli wateja wengi wanapenda kununua kwenye duka ambalo wanajua hata asipokuwa na hela ya mfuko, basi atafungiwa bidhaa yake kwenye huu mfuko mweupe. Kwa hiyo kuvutia wateja ndiyo maana mimi ninaitumia”. Alisema muuzaji ambaye hakuwa tayari kutajwa jina lake
Wananchi mbalimbali waliohojiwa katika makala hii walieleza namna ambavyo mifuko hii inatumika. Maelezo yao yalionesha uhalisia wa tatizo hili kwani hakuna anayejali wala kuchukua hatua licha ya matumizi yasiyo na kificho katika maeneo yote ya umma.
“Hii mifuko inatumika madukani, masokoni, na migahawani. Ukienda kama sokoni inatumika kama vifungashio. Kwa mfano ukienda sokoni kununua nyanya unawekewa humo. Ukienda migahawani kwa mama lishe wanafungia ugali ili kutunza joto, wanafungashia na chapati. Ukienda dukani wanafungashia bidhaa kama mchele na kadhalika”. Maoni ya Lilian Jones ambaye ni mkazi wa Buhongwa
Migahawani
Wakazi wa Jiji la Mwanza kama ilivyo kwa maeneo mengine ya Tanzania, wanatumia ugali kama miongoni mwa chakula chao kikuu. Baadhi ya watumiaji wakubwa wa ugali ni watu ambao hufanya kazi zinazotumia nguvu. Kutokana na ukweli kuwa baadhi yao hawali kwa wakati, basi ugali huo unahitajika kubaki kuwa wa moto kwa muda mrefu.
Matumizi ya mifuko ya plastiki sasa ni makubwa katika migahawa jijini Mwanza. Wafanyabiashara wengi wa migahawa hutumia mifuko hii kutunzia ugali na kufunikia aina nyingine za chakula ili kisipoe. Katika mitaa mingi ya jiji hili kumeshuhudiwa matumizi makubwa ya mifuko hii katika kutunzia chakula cha moto.
“Yaani hapa ninafunga ugali ili kutunza joto, yaani ninafanya hivi ili ugali usipoe nikimaliza naweka maji jikoni kwenye sufuria lingine. Ina maana hata mteja akifika anakuta ugali ni wa moto”. Alieleza mpishi mmoja katika eneo la Nyamalango

Katika kujaribu kuelewa kama wafanyabiashara hawa (mama lishe) wanaelewa athari za mifuko hii, mama huyu ambaye alikutwa akifunga ugali alijibu kwa kifupi.
“ Aaah, athari kwa kweli sijui, athari sijui”
Baada ya kuona hali halisi ya matumizi ya mafuko ya plastiki, Land Dwellers ilijaribu kupata maoni juu ya utumiaji huu kutoka kwa wataalamu na wasimamizi wa sheria. Afisa Afya Jiji la Mwanza, Audiphace Sabbo anasema kuwa wanapambana kutoa elimu huku wakiwajibisha wale wanaotumia.
“Kama Halmashauri ya Jiji la Mwanza sisi idara ya Afya tunazuia matumizi ya mifuko ya plastiki iliyozuiliwa na serikali. Ni kweli kuwa licha ya marufuki hii, bado kuna watu watukutu ambao bado wanatumia mifuko hii, na kama nilivyosema sisi wataalamu kazi yetu ni kuhakikisha isitumike. Kwa hiyo huwa tunachukua hatua kama tukikuta ipo sokoni au tukikuta mama lishe amefungia chakula, tunaichukua na tunaiharibu”. Kauli ya Audiphace Sabbo, Afisa Afya wa Jiji la Mwanza.
Madhara ya utumiaji wa mifuko ya plastiki
Mifuko ya Plastiki ambayo hutengenezwa kutokana na mabaki ya nishati ijulikanayo kama mafuta ghafi (crude oil), hayawezi kurejelezwa katika matumizi. Athari za matumzi ya mifuko hii zimegawanyika katika sehemu kuu nne ambazo ni athari za mazingira, athari za kiafya kwa binadamu, athari kwa viumbe hai pamoja na athari za kiuchumi.
Athari katika mazingira
Mifuko Plastiki katika Jiji la Mwanza inaonekana kuzagaa na kuchafua mazingira hasa katika maeneo ya masokoni, kando ya ziwa na kwenye baadhi ya mifereji ya maji. Utupaji wa mifuko hii baada ya kutumika unafanya mazingira kuwa mabaya na kukosa mvuto kwa wageni au watalii ambao wanafika katika jiji hili kwa mara ya kwanza.
Baadhi ya wakazi wa Mwanza waliohojiwa walieleza jinsi mazingira yanavyokuwa machafu kutokana na utupaji wa mifuko ya plastiki baada ya kutumika.
Kwenye mazingira yetu ya kawaida tunaangalia labda kwenye vyanzo vya maji unaikuta, ukienda ziwani utaikuta, kwenye mitaro utakuta imeziba. Kwa hiyo ni uchafuzi wa mazingira kwa sababu inazagaazagaa tu kila mahali”. Alisema Lilian Jones ambaye ni mkazi wa Mwanza.
Chapisho la Baraza la Taifa la Mazingira NEMC la mwaka 2023 lenye kichwa cha habari “Katazo la Mifuko ya Plastiki na Hali ya Matumizi ya Mifuko Mbadala” mifuko ya plastiki huchukua miaka 400 hadi 1000 kuoza ardhini.
Kwa mujibu wa UNEP na UICN mwaka 2018, tani 315,000 taka za plastiki zilizalishwa nchini Tanzania, ambapo katika mwaka huo takriban tani 29,000 za taka za plastiki ziliingia kwenye bahari, mito na maziwa nchini Tanzania. Katika Jiji la Mwanza, ziwa Victoria ndiyo huathirika pakubwa kutokana na mito mingi kusomba taka za plastiki na kupeleka ziwani.

Katika baadhi ya maeneo ya Jiji la Mwanza mifuko hii imetupwa katika mito na mifereji ya maji jambo linaloweza kusababisha kuziba kwa mifereji na baadhi ya njia za maji. Katika eneo la mto Mirongo ambao huupeleka maji yake ziwa Victoria, mifuko ya plastiki inaonekana kuelea na mingine kupelekwa ziwani.
Meneja wa NEMC Kanda ya Ziwa anasema kuwa jamii inatakiwa kuelewa athari hizi ambazo kama zikitokea watakaoathirika ni wao.
“Kitu cha kwanza ambacho watu wengi wanatakiwa kufahamu ni kuwa mifuko ya plastiki haiozi, yaani ukizalisha mfuko wa plastiki leo hapa, hadi uishe kabisa inaweza kuwa miaka 200 hadi 300. Kwa maana hiyo itabaki kwenye mazingira”. Meneja wa NEMC akifafanua.
Athari kwa viumbe hai
Mifuko ya Plastiki ambayo imetupwa katika mazingira imekuwa na athari mbalimbali kwa viumbe wa nchi kavu na pamoja na viumbe wa majini.
Tovuti ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira inasema mifuko hii pia huathiri mifumo ikolojia ya bahari ambapo na inakadiriwa 100,000 viumbe bahari na ndege bahari millioni moja kila mwaka wanakufa kwa kula mifuko ya plastiki kote duniani.
Baadhi ya tafiti zinaonesha kuwa chupa ya plastiki pamoja na mifuko ya plastiki inapoingia katika vyanzo vya maji pia huliwa na samaki ambao baadaye hutumiwa na binadamu. Utafiti wenye jina la ‘First evidence of Microplastics in the African Great Lakes: Recovery Lake Victoria Nile Perch and Nile Tilapia (2015)’ uliofanywa na watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine, Chuo Kikuu cha Dodoma, Taasisi ya Makumbusho ya Taifa ya Denmark na Chuo Kikuu cha Roskilde, ulibaini kuwa samaki 1 kati ya 5 katika Ziwa Victoria wana chembechembe za plastiki kwenye matumbo yao.
Kwa samaki jamii ya sangara (Nile Perch), asilimia 55% ya samaki waliofanyiwa utafiti walionesha kuwa na chembechembe za mifuko ya plastiki. Tafiti za madhara ya chembechembe hizi kwa binadamu bado zinaendelea kwa mujibu wa NEMC.
Jiji la Mwanza ambalo lipo pembezoni mwa Ziwa Victoria linahatarisha usalama wa viumbe wa majini hasa samaki kutokana na utumiaji wa mifuko ya plastiki ambayo mara nyingi husombwa na maji hadi ziwani baada ya kutumika. Kwa mujibu wa NEMC mifuko hii huathiri matumbawe ambayo ni makazi na mazalia ya samaki
“Ziwani kuna samaki, kuna vyura, kuna mamba, kuna mimea, kuna kila kitu.hiyo yote ilivyoumbiwa asili yake haitakiwa kusumbuliwa. Sasa ikitokea kuwa umepeleka mifuko ya plastiki ambayo haiozi, kama hilo eneo samaki anatafutia chakula, maana yake hawezi kupata tena. Kama hilo eneo ilikuwa na mazalia ya samaki, maana yake hawezi kuzaa tena”. Meneja wa NEMC akizungumzia madhara kwa viumbe hai na ikolojia kwa ujumla.

Kuna ushahidi kuwa dunia hupoteza wanyama wa majini 100,000 kila kutokana na uchafuzi wa mazingira. Miongoni mwa uchafuzi huo ni pamoja na taka za plastiki.
Athari za mifuko ya plastiki kwa afya za binadamu
Tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa mifuko ya plastiki ina athari kwa afya ya binadamu hasa pale ambapo inatumika kutunzia joto la chakula, kubebea chakula cha moto na wakati mwingine kuchomwa ambapo hutoa moshi mchafu wenye athari katika mfumo wa upumuaji wa binadamu.
Wataalamu mbalimbali wanaendelea kufanya utafiti juu ya madhara ya mifuko hii lakini kwa sasa tayari baadhi wanasema kuna uwezekano wa mtu kupata saratani kama atatumia chakula cha moto kilichohifadhiwa katika mifuko hii.
“Madhara ya mifuko ya plastiki ni makubwa sana, mojawapo ni kansa (saratani), ambapo binadamu anapata saratani, kwa hiyo tunapiga marufuku matumizi ya mifuko hii katika kufungashia vyakula pamoja na matumizi mengine ya kufungia bidhaa” Audiphace Sabbo, Afisa Afya Jiji la Mwanza

Wataalamu wa afya wanasema kuwa ni rahisi mifuko hii kubeba na kusambaza viumbe vamizi na bacteria. Katika chapisho la Baraza la Mazingira la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) hii ni miongoni mwa athari za kutumia mifuko hii na kuitupa katika mazingira
Nje ya mifuko hii kusambaza bacteria kama itatupwa hovyo, tafiti zimeonesha kuwa inapochomwa moshi wake una madhara (casinogenic compounds), pia mifuko ina kemikali za polychlorinated biphenyl, styrene na bisphenol ambazo zinaweza kusababisha maradhi ya kansa kwa binadamu. Hayo yameelezwa katika Jarida la NEMC la Agosti 02, 2023 lenye jina ‘Katazo la Mifuko ya Plastiki’.
Kutokana na ugumu wa mifuko hii katika kuoza, utupaji wake katika mifereji ya maji husababisha mifereji kuziba ambapo uwepo wa maji machafu unasababisha magonjwa ya tumbo ikiwemo kipindupindu.Hii ni kwa mujibu wa Taasisi ya National Institutes of Health (NIH) nchini Marekani kupitia chapisho lake la 2024.
Samaki wenye chembechembe za plastiki wakiliwa na binadamu yanaweza kusababisha matatizo ya kiafya. Jambo hili bado halijawekwa wazi na wanasayansi wakati tafiti mbalimbali zikiendelea kufanyika
Madhara ya kiuchumi
Mifuko ya Plastiki hutolewa bure kwa watumiaji ambao wananunua bidhaa masokoni pamoja na madukani. Kwa maana hii wengi hufikiria kuwa mifuko hii haina gharama. Kiuhalisia gharama za mifuko hii hutokana na athari zake katika mazingira, mifugo, binadamu lakini hata malighafi yake ya utengenezaji
Kwa takriban wananchi 20 waliohojiwa 18 walikuwa hawaelewi athari za kiuchumi wakisema kuwa mifuko hii wanapewa bure kwahiyo kwao hawatoi hela yoyote. Wachache waliobaki walisema kuwa pengine itaharibu taswira ya Jiji la Mwanza na kuathiri utalii wa jiji.
Wakati ikionekana kuwa wananchi hawana uelewa, wataalamu wa mazingira wanasema kuna athari ya matumizi ya mifuko hii kiuchumi ikiwemo kuharibu ubora wa ardhi, kuua wanyama ambao wanategemewa kiuchumi na hata gharama za kufanya usafi inapozagaa.
“Lakini mfuko wa plastiki ukishakaa, hauwezi kuruhusu kitu kupenya. Ikikaa shambani ki kwamba hilo shamba limeshapoteza ubora wake, ile kufaa kwa ajili ya kilimo. Kwa madhara yake yako kwenye kilimo, yako kwenye mifugo na kuna uchafuzi wa kawaida”. Meneja NEMC kuhusu madhara ya kiuchumi.
Tafiti mbalimbali zimefanyika na kuonesha kuwa kuna athari za kiuchumi za matumizi ya mifuko hii. Hasara zake zinaonekana kuwa kubwa kuliko faida zake. Mchoro ufuatao unaonesha athari za kiuchumi za matumizi ya mifuko hii kwa muhtasari

Mwandishi: Yohani Gwangway
Mhariri: Dominic Allen


