Na Yohani Gwangway
Miaka mitano ya upigaji marufuku uzalisha, uhifadhi, usambazaji, uuzaji na utumiaji wa mifuko ya plastiki nchini Tanzania imekuwa na mabonde na milima. Wakati tangazo la marufuku linatolewa mwaka 2019 na baadaye kutungiwa kanuni mwaka huo huo, jamii ilionesha mwitikio mkubwa wa kuacha matumizi ya mifuko ya plastiki.
Hata hivyo, kwa sasa matumizi haya yamerudi upya na kwa kasi. Swali la msingi ni kulikoni? Kwa nini sasa? Katika sehemu ya pili ya makala hii tunamulika chanzo cha tatizo la kutosimamiwa kwa marufuku ya serikali ya mwaka 2019 na kanuni zake za mwaka huo na maboresho ya mwaka 2022. Pia tutamulika wanaowajibika katika usimamizi, mianya na uzembe unaosababisha matumizi ya mifuko kuendelea.
Kwa baadhi ya wananchi ambao wao wanatumia mifuko hii, inaonekana wana uelewa mdogo katika kufahamu aina halisi ya mifuko iliyopigwa marufuku, huku wakiwa pia hawaelewi athari za kutumia mifuko ya plastiki. Uelewa huu mdogo unaonekana kuwa miongoni mwa sababu za wananchi kuendelea kutumia mifuko hii
“Watu wa mazingira wamekuwa wazito sana kutembelea hapa mtaani. Lakini wao wangekuwa wanaenda bega kwa bega na wananchi, naona hili suala la mifuko lingetibiwa tena lote. Kwa mfano mimi binafsi, sina kumbukumbu kama nilishawahi kukutana na afisa yoyote akielezea madhara ya hii mifuko ambayo ni transparency au hata madhara tu yake kwa mazingira”. Alisema Rajabu, mkazi wa Mwanza.
Kwa Rajabu, maafisa mazingira katika ngazi ya chini hawawajibiki ipasavyo na wakati mwingine hata hawafahamiki mtaani. Jambo hili linafanya vita dhidi ya mifuko ya plastiki kuwa ngumu zaidi.
Licha ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 kuweka usimamizi hadi ngazi ya chini kabisa ambayo ni ya kitongoji, Tyson Cosmas ambaye anaishi jijini Mwanza anasema tangu yeye aanze kuishi hapa takriban miaka mitatu sasa hajawahi kuona maafisa wa mazingira katika maeneo yao.
“Toka nimekuwepo sijawahi kuwaona. Na kiukweli sidhani kama wanatekeleza majukumu yao ipasavyo. Hivi ni vitu ambavyo vinahitaji elimu katika jamii, lakini hatujawahi kuona hata wakitoa elimu au neno lolote kwa hiyo ni watu tu tunatumia mifuko hii” Tyson akieleza uwajibikaji wa maafisa wa mazingira ngazi za chini.
Elimu ikiwa inaonekana ndiyo kilio cha wananchi walio wengi, kwa baadhi ya wachache kuna sababu za kiuchumi. Ahmed (jina siyo halisi) ni msambazaji ambaye yeye anasema anafanya kazi ya kusambaza mifuko kutokana maisha duni na kukosa mtaji wa kufanya kazi nyigine.
“Labda niseme kitu kimoja kwa sababu kulingana na maisha na mazingira, kiukweli mimi hii biashara nilikuwa sina ramani yeyote. Baadaye mtu akanambia, bwana ukifanya biashara ya mifuko utapata hela.” Ahmed akieleza sababu inayomfanya kuuza mifuko ya plastiki.
Uzembe na rushwa kwa baadhi ya maafisa wa Jeshi la Polisi na mamlaka za usimamizi unafanya udhibiti wa mifuko hii kuwa mgumu. Ahmed anasema akikamatwa na polisi anatakiwa kutoa rushwa kuanzia elfu hamsini ili aachiwe. Na wakati mwingine akikosa hela huwa anawaachia polisi au mgambo ambao wao wenyewe huuza mifuko hiyo.
“Zaidi wanaokamata ni polisi na mgambo. Kuna wale polisi ambao hawana sare (uniform), hao ndio wanaokamata. Yaani wakikukamata ukiongea nao vizuri, unawapa hela wanaondoka, usipotoa hela wanakunya’ganya mzigo halafu wanaenda kuuza”. Maelezo ya Ahmed kuhusu ukamataji wa polisi.
Suala hili ambalo linaonekana kutatiza uwajibikaji na kupunguza juhudi za kuzuia utumiaji wa mifuko hii, inaonekana kukithiri kiasi cha kuwa na kiwango maalum cha pesa ambazo polisi hupokea ili kuwaachia wasambazaji. Kwa mujibu wa Ahmed, pesa yoyote chini ya elfu hamsini haipokelewi.
“Ili uachiwe labda utoe zaidi ya elfu hamsini, na kama mzigo ni mdogo ni bora tu kuwaachia. Kwa mfano kama piece 25 hizo ni bora tu kuwaachia”. Alieleza Ahmed.
Swali ni je, kama usambazaji wa mifuko hii unaonekana kuwa kitega uchumi kwa baadhi ya wasimamizi wa sheria, ni lini kutakuwa na uwajibikaji na umakini wa kusimamia sheria?
Hadi makala hii inakamalishwa hatukupata ushirikiano kutoka kwa Jeshi la Polisi jijini Mwanza kutokana na tuhuma za baadhi ya askari kuwaachia wenye makosa kwa kupokea rushwa.
Tunajaribu kufahamu kutoka kwa mamlaka ya Jiji la Mwanza juhudi ambazo zinafanyika katika usimamizi wa sheria huku wakiwa na wajibu wa kutoa elimu. Afisa Afya katika Jiji la Mwanza, Audiphace Sabbo anasema kuwa mwingiliano wa watu katika Jiji la Mwanza ni mkubwa kiasi kwamba elimu inatakiwa ifanyike mara kwa mara.
“Kama nilivyosema mwingiliano wa watu katika halmashauri yetu ni mkubwa, kwa hiyo suala la elimu linatakiwa kupewa kipaumbele. Leo unaweza kuelimisha watu kuhusu madhara ya mifuko ya plastiki watu wakaelewa kabisa, lakini baada ya siku mbili tatu unakuta watu wengine ambao ni tofauti kabisa na wale ambao uliwaelimisha, kwa hiyo sisi kama Halmashauri ya Jiji tunafanya utoaji wa elimu kuwa suala endelevu”. Alisema Audiphace Sabbo, Afisa Afya Jiji la Mwanza.
Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira.
Kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004, Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira lina majukumu makubwa katika kusimamia na kuhifadhi mazingira. Moja ya kazi ya baraza hili ni pamoja na kutoa elimu kwa wananchi. Kutokana na hoja ya wananchi kuwa hawana elimu, tulitaka kufahamu namna gani baraza hili linatekeleza majukumu yake ya kisheria.
“NEMC tumefanya mambo mengi sana na kwanza ni kuelimisha. Kwa hiyo la kwanza ni kueleimishana kuhusu kifungashio ni nini au ni bidhaa gani ya plastiki imeruhusiwa na kwa nini imeruhusiwa. Lakini la pili kuelimishana kuhusu madhara na kadhalika. Kwenye kuelimishana tumeweka vituo kwa mfano, ukienda uwanja wa ndege wa Dar es Salaam unakuta kuna watu wetu lakini pia kuna mabango kwa ajili ya wageni wanaoingia ambao tumewakea kipaumbele ili wajue kuwa hivi vitu haviruhusiwi” Jarome Kayombo, Meneja wa NEMC Kanda ya Ziwa Victoria.
Licha NEMC kusema kuwa inatoa elimu kwa jamii kuhusu madhara ya mifuko ya plastiki, lakini hali halisi hapa jijini Mwanza bado wananchi wanauelewa mdogo juu ya hilo. James Elisante Makondeko ambaye ni mkazi wa Mabatini, Mwanza anasema katika eneo analoishi hawajawahi kupatiwa elimu kuhusu mifuko ya plastiki na madhara yake.
“Kwa upande wangu mimi sijawahi kuona elimu inatolewa ya madhara ya mifuko ya plastiki sana sana mimi ninavyojua mifuko iliyokatazwa ni ile mingine (malboro) lakini hii hapa (meupe) tunaendelea kuitumia” Alisema James, bila kuwa na ufahamu kuwa hata hiyo meupe anayoizungumzia nayo pia imepigwa marufuku.

Nchini Tanzania sheria mama inayosimamia mazingira ni Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya Mwaka 2004. Sheria hii ndiyo kwa kiasi kikubwa imetoa mwongozo wa mamlaka za utekelezaji pamoja na maafisa wake. Vifungu cha 35, 36,37 na 38 vinaeleza mamlaka zitakazotekeleza sheria hii pamoja na kanuni zake. Miongoni mwa wanaotajwa ni Afisa Mazingira Jiji, Afisa Mazingira Mji, Afisa Mazingira Kata, na Maafisa wengine hadi ngazi ya Kitongoji.
Lakini pia katika Sheria hii vifungu vya 16,17, na 18 vinazungumzia kuanzishwa, malengo na kazi ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira.
Lengo la kuanzishwa kwa Baraza 17 (1) Lengo na madhumuni ya kuanzishwa kwa Baraza ni kusimamia udhibiti, utekelezaji, uzingatiaji, upitiaji upya na upelembaji wa tathmini ya athari kwa mazingira na, kwa ajili hiyo, litawezesha ushirikishwaji wa umma katika uamuzi kuhusu mazingira, kutekeleza usimamizi wa jumla na uratibu wa masuala yote ya mazingira yaliyoelekezwa kwa Baraza kwa mujibu wa Sheria hii au Sheria nyinginezo zilizotungwa na Bunge.
Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) lina nafasi kubwa ya utekelezaji wa sheria na kanuni zinazopitishwa nchini Tanzania. Lakini baraza hili halina maafisa kila sehemu jambo ambalo linafanya usimamizi huu uwe mgumu kwao. Meneja wa NEMC Kanda ya Ziwa ambayo husimamia mikoa 6 anasema Baraza hilo halina zaidi ya wafanyakazi 300 nchi nzima kwahiyo linategemea sana ushirikiano wa taasisi zingine katika kutekeleza majukumu yao.
“Siyo kwamba najitetea, naomba nieleze hali halisi. Nimesema NEMC wafanyakazi wote hata hatufiki 300, Kanda ya Ziwa hapa kwenye mikoa 6 wafanyakazi wote tuko 23, kwa hiyo hata tukigawana ni wafanyakazi wanne kwa kila mkoa. Je, wataweza kuwepo Misungwi, Magu, sijui Kwimba. Haiwezekani, ndiyo maana kilio chetu tunaomba sana kila mtanzania aamke, ajue haya mazingira ni ya kwake yeye”. Kayombo akifafanua.

Nje na baraza hili, Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 inatambua uwepo wa mtaalamu wa mazingira katika kila mkoa ambaye atakuwa na majukumu ya kushauri masuala ya mazingira katika mkoa husika. Lakini inaonekana watu hawa hawafiki kwa jamii kutokana na maoni yaliyotolewa na wananchi kuhusiana na usimamizi wa mazingira katika maeneo yao
Maafisa wa mazingira katika maeneo husika
Sheria inatambua uwepo wa maafisa katika ngazi za Wilaya, Mji, Kata, Mtaa/Kijiji pamoja na Kitongoji. Watu hawa ni maafisa mazingira ambao miongoni mwao ni wataalmu wa mazingira wenye majukumu ya kushauri namna usimamizi wa mazingira unavyotakiwa kufanyika katika maeneo yao.
Majukumu ya kiuwajibikaji kwa maafisa hawa yanapatikana katika kifungu cha 40 cha Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004.
“Kazi za Ofisa Usimamizi Mazingira wa Mji, Kata, Kijiji, Mtaa na Kitongoji itakuwa ni kuratibu kazi zote na shughuli zinazolenga kuhifadhi mazingira kwenye eneo la mji, kata, mtaa, kijiji na kitongoji, au kadiri itakavyokuwa ndani ya Wilaya ya eneo husika”. Sheria inaeleza.

Kuzagaa kwa mifuko ya plastiki mtaani kunaibua maswali ya uwajibikaji kwa maafisa hawa. Je, wanatekeleza majukumua yao ipasavvo? Meneja wa NEMC Kanda ya Ziwa Victoria anasema kila mtu angekuwa anatekeleza wajibu wake huenda usimamizi wa marufuku ya plastiki nchini Tanzania ingefanikiwa kwa kiasi kikubwa.
“Sheria inasema pale kwa mkuu wa mkoa kunatakiwa kuwe na mtaalamu wa mazingira yaani Regional Environmental Management Expert, kwenye wilaya kuna afisa mazingira, ukienda kwenye ngazi ya kata na mtaa huko kuna kamati za mazingira, kwa hiyo ukiangalia sheria mfumo umenyooka, kama hawa watu wangekuwa wanafanya kazi kusingekuwa na mfuko wa plastiki”. Maelezo ya Kayombo, meneja wa NEMC Kanda ya Ziwa.
Wakati NEMC wakieleza majukumu ya maafisa na wataalum wa mazingira katika maeneo mbalimbali, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Usafi wa Mazingira Jiji la Mwanza, Desderius Polle anaeleza kuwa wao wamekuwa wakishirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa masoko pamoja na serikali.
“Tunashirikiana na uongozi wa kata, tunashirikiana na maafisa afya wa kata, tunashirikiana na wenyeviti wa masoko kwa ajili ya kupata taarifa kama kuna jambo lolote linaenda kinyume na usafi wa mazingira, wao ndiyo mabalozi wa kwanza wa kutoa taarifa na sisi tunachukua hatua kwa haraka, kwa hiyo ushirikiano ni mkubwa jinsi chain (mfumo) ilivyo”. Alisema Desderius Polle, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Usafi wa Mazingira Jiji la Mwanza.
Katika uchunguzi huu, inaonekana wazi kuwa maafisa mazingira hawazungumzwi kabisa hasa katika ngazi ya chini na badala yake wanatajwa maafisa afya jambo ambalo ni kinyume na Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004.
Kamati za Kudumu ya Mipango Miji na Mazingira
Sheria ya Usimamizi wa Mazingira (2004) kifungu cha 37 (1) inazungumzia kuhusu kamati mbili muhimu za kusimamia masuala ya mazingira. Kamati hizo ni Kamati ya Kudumu ya Mipango Miji na Mazingira iliyoanzishwa chini ya kifungu cha (1) cha fungu la 42 la Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji) ya mwaka 1982, pamoja na Kamati ya Kudumu ya Masuala ya Uchumi, Ujenzi na Mazingira iliyoazishwa chini ya kifungu cha (1) cha fungu la 74 la Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya) ya mwaka 1982.
Kamati hizi zina majukumu kadhaa ambayo yamewekwa kisheria. Kifungu cha 41 cha Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 kinataja majukumu ya Kamati za Usimamizi wa Mazingira za Jiji, Manispaa, Wilaya, Mji, Kata, Kijiji, Mtaa na Kitongoji
Kila Kamati ya Usimamizi wa Mazingira inayohusu eneo ilimoanzishwa, itakuwa na madaraka ya-
Miongoni mwa majukumu ya kamati hizi ni kuanzisha uchunguzi na upelelezi kuhusu tuhuma yoyote inayohusu mazingira na utekelezaji au ukiukwaji wa masharti ya Sheria hii, kumtaka mtu yeyote kutoa maelezo au taarifa kuhusu suala lolote linalohusu mazingira na kutatua migogoro kati ya watu binafsi, makampuni, wakala, asasi zisizokuwa za kiserikali, idara au asasi za Serikali, inayohusu majukumu, kazi, uwezo, wajibu au shughuli zao chini ya Sheria hii.
Majukumu mengine ni kukagua na kuchunguza makazi, mtaa, gari, ndege au sehemu nyingine yoyote au kitu kinachoaminika au kuna sababu za msingi kuamini kuwa kichafuzi au vitu vingine vinavyoaminika kuwa vichafuzi vimewekwa au vinasafirishwa, kumtaka mtu yeyote aondoe kwa gharama yake, kitu au dutu yoyote kutoka mahali popote panapoaminika kuwa kitu au dutu hiyo inaweza kuhifadhiwa kwa usalama au kuharibiwa bila kuleta madhara kwa afya na Kufungua kesi za madai au jinai dhidi ya mtu yeyote, kampuni, wakala, idara au asasi inayoshindwa au kukataa kufuata agizo lolote.

Licha ya majukumu haya, uchunguzi wa Land Dwellers umefuatilia kamati hizi katika ngazi za vitongoji, mtaa na kata katika jiji la Mwanza na kugundua kuwa hazipewi kipaumbele na wala hawakutani mara kwa mara kuweka mipango ya utunzaji wa mazingira katika ameneo yao. Tumetembelea vitongoji vitatu na mitaa wawili ambapo tulizungumza na baadhi ya wajumbe wa kamati hizi. Licha ya kuwa hawakuwa tayari kutajwa majina na maeneo yao, lakini walieleza changamoto ya kamati hizi katika maeneo yao.
Miongoni mwa mambo yaliyoibuliwa ni pamoja na kamati hizi kukosa malengo au mipango hivyo kusubiri kuvunjwa kwa sheria ndiyo ionekane wanafanya kazi. Mikakati ya mapema inakosekana jambo linalofanya kuwe na ugumu katika kutekeleza wajibu wao.
“Kamati ipo, ila haipewi hata kipaumbele. Wanakamati hawajui hata majukumu yao. Ni mara chache sana tunapanga mipango ya mazingira. Mimi naona tu labda huko juu inafanya kazi, ili huku ngazi za chini hizi kamati ni majina tu” Alieleza mmoja wa wanakamati katika kata ya Buhongwa jijini Mwanza ambaye hakutaka kutajwa jina.
Idara zinazotakiwa kushirikiana kutekeleza marufuku ya mifuko ya plastiki
Kifungu cha 14 cha Kanuni za Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2019 ya Katazo la mifuko ya plastiki inataja wizara, taasisi, mamlaka na idara zaidi ya 10 katika kusimamia marufuku ya mifuko ya plastiki nchini Tanzania. Kwa mujibu wa kanuni hiyo baadhi ya wizara, taasisi na mamlaka niWizara ya Viwanda na Biashara, Mamalka ya Chakula na Dawa (TMDA), Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA, Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Idara ya Uhamiaji Tanzania.
Taasisi na mamlaka zingine ni Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali pamoja na Jeshi la Polisi.

Mwandishi: Yohani Gwangway
Mhariri: Dominic Allen


