Na Amiri Kilagalila
Mbunge wa Jimbo la Lupembe mkoani Njombe, Edwin Swalle amewaomba wakazi wa kijiji cha Nyombo katika jimbo hilo kuwa na imani na serikali juu ya ujenzi wa kiwango cha lami barabara ya Kibena – Kidegembye yenye urefu wa kilomita 42, kwa kuwa tayari serikali imeshatangaza zabuni kwa ajili ya ujenzi.
Swalle ameeleza hayo jana Mei 28, 2025 wakati akizungumza na wakazi wa kijiji cha Nyombo Kata ya Ikuna, ambapo amesema haijawahi kutokea katika jimbo hilo ikatangazwa zabuni ya ujenzi wa barabara hiyo lakini kwa sasa serikali imeshatangaza na hakuna mwenye uwezo wa kuifuta zabuni.
“Niwaambie Wananyombo haijawahi kutokea katika jimbo hili ikatangazwa tena ya ujenzi wa lami tangu Lupembe imeundwa, ndiyo imetangwa kwa mara ya kwanza mwaka huu, ninaomba tuipe nafasi serikali kwasababu ukishatangaza tenda huwezi kufuta lazima kazi itafanyika” amesema Swalle.

Katika mkutano huo Swalle ametoa nafasi kwa Mhandisi Charles Masuka kutoka Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) ili aweze kutoa ufafanuzi kinachoendelea juu ya barabara hiyo kwa kuwa nyumba zao zimekuwa zikichafuka vumbi.
Kwa upande wake Mhandisi Masuka ameeleza kuwa kinachoendelea kwa sasa ni utathmini kwa wananchi waliopisha barabara, kwa ajili ya ulipaji wa fidia ili mkadarasi atakapopatikana kazi iendelee.

Nao baadhi ya wakazi wa Nyombo wamemshukuru Mbunge Edwin Swalle pamoja na serikali kwa kuendelea kufanikisha kuanza ujenzi wa barabara hiyo, ambapo wamesema kuwa kukamilika kwake itakuwa ni chachu kubwa ya maendeleo kwa wilaya ya Njombe.
Mwandishi: Amiri Kilagalila
Mhariri: Dominic Allen


