Na Fredrick M. Justine
Katika siku za karibuni, Taifa limekuwa shahidi wa kile kinachoendelea kati ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini na chama kikuu cha upinzani, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA). Hatua zilizochukuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa Jaji Francis Mutungi, ikiwemo kufungia ruzuku ya chama, kufuta uteuzi wa viongozi wakuu na kuhoji uhalali wa mchakato wa uchaguzi mkuu wa ndani wa chama, zimeacha maswali mengi kuhusu hatima ya demokrasia na haki ya wananchi ya kuwa na chama kinachowakilisha sauti yao ya kweli.
Ni muhimu kuanzia kwenye ukweli kwamba uchaguzi mkuu wa ndani ya CHADEMA uliyofanyika mwezi Januari mwaka huu ulikuwa ni wa uwazi, uhuru na haki. Taifa zima lilishuhudia na dunia iliona namna ambavyo demokrasia ya viwango ilitekelezwa, ambapo Tundu Lissu alichaguliwa kwa kura halali na Freeman Mbowe alikubali matokeo kwa moyo wa heshima na busara ya kiuongozi. Mchakato huo ulikuwa mbele ya Naibu Msajili, mabalozi, wanahabari, na umma wa Watanzania.
Baada ya uchaguzi wa ndani ya chama kukamilika, kulifanyika uteuzi wa viongozi wa juu ikiwemo Wajumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA kuwa kufuatia Katiba ya chama. Lakini mmoja wa aliyekuwa kiongozi wa CHADEMA, Lembrus Mchome alipinga na uteuzi wa viongozi hao, na moja ya hoja zake ni kuwa akidi haikukamilika na kufikia hatua ya kuandika barua kwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini.
Hoja za Bw. Mchome zilijibiwa na uongozi wa CHADEMA, tena kwa vielelezo vya akidi na majina ya wajumbe halali, na hakukua na kosa la kikatiba lililothibitishwa. Licha ya chama kujibu kile kilichodaiwa na Mchome, lakini Msajili wa Vyama vya Siasa ameendelea kupigilia msumari wa hatua kali kuchukuliwa dhidi ya CHADEMA, akimaanisha kuwa ni kama vile chama hakikufuata taratibu. Sasa, kuna dalili wazi kwamba kinachoandaliwa ni mkakati wa kufuta usajili wa CHADEMA.
Watu wengi wamependekeza njia ya “muda mfupi ya usalama” ni kwamba CHADEMA iitishe Baraza Kuu jipya na uchaguzi wa Katibu Mkuu na Wajumbe wa Kamati Kuu, ili “kumridhisha Msajili”. Je, huo ndiyo ukweli? Je, tutakuwa hatuhalalishi hila na uzushi wa Msajili?
Kwa chama kilichojengwa juu ya msingi wa ukweli, haki, demokrasia, na uwazi, hatuna sababu ya kupindisha ukweli au kulaghai, hata kwa hofu ya kupoteza usajili. Kufanya hivyo ni kusaliti mchakato halali na watu waliouamini.
Leo hii, ruzuku imefungwa. viongozi walioteuliwa kihalali wamefutwa. Viongozi wa zamani kutoka Zanzibar wamefungua kesi Mahakama Kuu ya Tanzania kudai shughuli za chama zisimamishwe. Mradi wa kisiasa wa “CHAUMMA” unajaribu kutumia mwanya huu kudhoofisha chama, bila kusahau kesi ya uhaini dhidi ya Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Tundu Lissu imewekwa mbele ili kumnyonga kisiasa hadi mwisho.
Lakini swali kuu ni hili; Endapo tutakubali madai ya Msajili wa Vyama vya Siasa Jaji, Fransic Mutungi, mnadhani hila hizi zitakoma? Je, tukiitisha Baraza Kuu la Chama kwa hofu, Msajili atatupenda na kuturuhusu tuendelee na siasa? Hasha, atakuja na hila mpya na mbinu mpya, lengo ni moja; kuvunja, kusambaratisha, kuua CHADEMA.
Hivyo basi, hatuna budi kusimama katika msingi wa ukweli na uhalali. Kila hatua ya mchakato wa uchaguzi ilikuwa halali. Kama Msajili wa Vyama vya Siasa atathubutu kufuta chama, basi wanachama wote nchini pamoja na Watanzania wema, watasimama kulinda chama chao. Na wasipofanya hivyo, sisi viongozi tutasimama, kwa jasho na damu hadi tone la mwisho.
Na iwapo wananchi wenyewe watasaliti dhamira hii, basi wajue wamekubali kuishi chini ya utawala wa ulaghai, uonevu, na hila zisizozingatia haki wala demokrasia ya kweli.
Tutakuwa hatuna deni. Vita tumepigana, imani tumeilinda na mwendo tumemaliza.
(Haya ni maoni binafsi ya Mwanaharakati Fredrick M. Justine)


