Na Dominic Allen
Mkurugenzi wa Oganaizesheni, Mafunzo na Uchaguzi CHADEMA, Mwl. John Pambalu hii leo ameeleza kuwa amesikitishwa na kitendo cha Jeshi la Polisi Tanzania kumzuia kuonana na kiongozi wa chama hicho Mhere Mwita ambaye anashikiliwa katika Kituo cha Polisi Kati (Central Police) Dar es salaam kwa tuhuma za uchochezi.
Kwa mujibu wa Mwl. Pambalu, alipofika katika kituo hicho kwa ajili ya kumuona Mhere, OCS ASP Sofia Dilunga alimzuia kufanya hivyo kwa madai kuwa hawezi kumruhusu hadi pale atakapopata maelekezo ya ruhusa kutoka kwa wakuu wake.
“Lakini jambo la kusikitisha Afande OCS ASP Sofia Dilunga amenikatalia kumuona akasema nitamuona tu ikiwa ataelekezwa na wakuu wake tuweze kumuona.” Amesema Mwl. Pambalu.
Mwl. Pambalu amesisitiza kuwa Mhere anapaswa kupewa haki ya kuoana na ndugu zake, kwani siyo mhaini huku akilitaka Jeshi la Polisi kumuachilia huru.
“Nimefanikiwa kumpata Afande Aziz lakini sijapata msaada wowote. Muhere Mwita sio muhaini mpeni haki yake ya kuonana na ndugu zake. Muachieni huru Muhere.” Amesisitiza Mwl. Pambalu.
Kufuatia malalamiko hayo aliyotoa Mwl. John Pambalu, Land Dwellers imefanya juhudi za kumtafuta Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, SACP Jumanne Muliro bila mafanikio kutokana na simu yake kutokuwa hewani.
Kabla ya kuletwa katika Kituo cha Polisi Kati (Central Police) Dar es salaam, Mhere Mwita alikamatwa na Jeshi la Polisi mkoani Geita, ambapo taarifa ya kukamatwa kwake ilitolewa na Katibu wa CHADEMA Kanda ya Victoria, Zacharia Obad mnamo Machi 28, 2025.
Mwandishi: Dominic Allen
Mhariri: Yohani Gwangway


