Na Dominic Allen
Rais wa Kenya, William Ruto amesema kuwa aliwahi kutishiwa na aliyekuwa Naibu Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua, kuwa anaweza kumfanya awe Rais kwa muhula mmoja tu endapo hatampatia kiasi cha Ksh. Bilioni 10 ili kushawishi uungwaji mkono katika eneo la Mt. Kenya.
Rais Ruto amezungumza hayo hapo jana katika mahojiano na vyombo vya habari masaa kadhaa kabla ya ziara yake huko Mt. Kenya.
“Niliambiwa ninaweza kukufanya uwe Rais wa muhula mmoja, kama hutanipatia Ksh. Bilioni 10 nisimamie siasa eneo hili” alisema Rais Ruto.
Katika mahojiano hayo, Rais Ruto amekosoa vitendo vya Gachagua kupambana na baadhi ya watu ndani ya serikali ya Kenya Kwanza, jambo lililopelekea kuondolewa kwake madarakani.
“Baada ya uchaguzi, Gachagua aligeuka kuwa mlalamishi…akimtuhumu kila mtu, hata wale wadogo kama vile Dennis Itumbi, Ndindi Nyoro…alianza kutishia Wabunge, akiwaonya kuwa watakiona cha moto Disemba 2024” aliongeza Rais Ruto.
Rais William Ruto amekana juu ya yeye kuwa kichocheo kwa Rigathi Gachagua kuondolewa madarakani, akisema kuwa sheria ilifuata mkondo wake.
“Mara ya kwanza nilijaribu kuwazuia (Wabunge) lakini waliniambia kuwa wataendelea kwa baraka zangu au bila baraka zangu. Nilizuia mara mbili kuondolewa kwake, mara ya tatu walifanikiwa. Sikuweza kuwazuia” alizungumza Rais Ruto.
Rigathi Gachagua aliondolewa katika nafasi ya Naibu Rais wa Kenya na Seneti nchini humo mnamo Oktoba 17, 2024 kufuatia tuhuma za makosa 11 dhidi yake ikiwemo utovu wa nidhamu na kujilimbikizia mali.
Mwandishi: Dominic Allen
Mhariri: Yohani Gwangway


