Na Dominic Allen
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan leo Machi 27,2025 amepokea Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2023/24 kutoka kwa Charles Kichere pamoja na Taarifa ya Mwaka ya Utendaji Kazi wa Taasisi ya Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
Katika ripoti hiyo ya CAG mengi yameibuliwa, na miongoni mwa hayo ni hasara ambayo mashirika ya serikali yalipata kwa mwaka wa fedha wa 2023/24, ambapo Shirika la Reli Tanzania (TRC) lilipata hasara ya kiasi cha Tsh. Bilioni 224, ikiwa ni mara mbili zaidi ya hasara liliopata shirika hilo kwa mwaka 2022/23 ambayo ilikuwa ni bilioni 102.
“Shirika la Reli Tanzania (TRC) lilipata hasara ya Tsh. Bilioni 224 ikilinganishwa na hasara ya Tsh. Bilioni 102 ya mwaka uliyopita” amesema Charles Kichele.
Kichere amesema kuwa hasara hiyo imesababishwa na uhaba wa vichwa vya treni na mvua kubwa uliyopelekea njia kufungwa kwa miezi minne, na endapo shirika hilo lisingepata ruzuku hasara ingekuwa ni Tsh. Bilioni 253.

Kwa upande wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), limepata hasara ya Tsh. Bilioni 91.8, ikiwa ni ongezeko la asilimia 62 kutoka bilioni 56.6 kwa mwaka 2022/23.
“Hasara hii imetokana na gharama kubwa za matengenezo ya ndege itilafu za injini ambapo ndege aina za airbus zilikaa muda mrefu bila kufanya kazi zikisubiria injini” amebainisha Charles Kichele.
Kichere ameongeza kuwa bila kutolewa ruzuku ya serikali ya Tsh. Bilioni 99.8, ATCL ingepata hasara ya Tsh.191.6.
Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) lilipata hasa ya Tsh. Bilioni 27.78 kwa mwaka wa fedha 2023/24 kulinganisha na hasara ya Tsh. Bilioni 4.32 kwa mwaka 2022/23, ambapo ongezeko hilo limetokana na kupanda kwa gharama baada ya kuhamishwa kwa Mkongo wa Taifa na Kituo cha Taifa cha Data.
Ripoti hiyo ya CAG imebainisha kuwa hadi kufikia Juni 30, 2024, deni la serikali lilifika kiasi cha Tsh. Trilioni 97.35 kutoka Tsh. 82.25 kwa mwaka wa fedha 2022/23, ambalo ni ongezeko la asilimia 18.36.
Hata hivyo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa serikali ipo tayari ipo tayari kufanyia kazi maoni na mapendekezo ambayo yametolewa katika Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2023/24 pamoja na Taarifa ya Mwaka ya Utendaji Kazi wa Taasisi ya Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
Mwandishi: Dominic Allen
Mhariri: Yohani Gwangway


