Na Wakili Boniface Mwabukusi
Katika nyakati za uchaguzi, taifa letu hujaa kelele, ahadi na vilio bandia vya mashujaa wa kisiasa waliolala wakati wa dhiki, lakini sasa wanajivika mavazi ya uzalendo ili warudishe imani ya wananchi kwao. Ni kipindi ambacho kila kona huchipuka mashujaa wa ghafla wale waliokaa kimya tulipolia, waliotabasamu tulipoteseka, sasa wanakuja kutuambia wamesikitika kwa hali ya nchi, wakitamani tuwaamini kuwa wako nasi.
1. Mashujaa wa ghafla waliolia tulipolia, lakini hawakuwapo tulipoumia
Wapo wanaojifanya kuguswa na matatizo yetu ya kidemokrasia, kiuchumi, na kijamii. Lakini historia inatufundisha kuwa tulipokandamizwa, walitazama kwa ukimya kwasababu walikuwa wala kunde nasisi tulibaki kuwa watupa Maganda.
Walishiriki kufubaza haki na kununua wapinzani kama karanga walijifanya hawasikii kilio chetu cha maumivu ulikuwa muziki mororo uliosindikiza usingizi wao baada ya kuvimbiwa na utamu wa hatamu za madaraka.
Waliona misiba na malalamiko yetu kama tamthilia ya runinga leo wanataka tusahau mateso yetu na tujiunge nao kulia msiba waliochangia kuumba. Machozi yao si ya dhati, ni machozi ya mamba wenye kiu ya hatamu za madaraka.
2. Tulipoteswa hawakukemea, leo wanalia kwa hofu ya kukosa uongozi
Tulipokamatwa bila sababu, kupigwa, kutekwa, na kushtakiwa kwa makosa ya kutungwa, walikaa kimya. Hawakutuunga mkono, hawakutufariji, hawakujitokeza hata kuhoji udhalimu huo. Na waliutekeleza bila hofu. Leo, eti wanataka tulie pamoja “uchungu wa Taifa” lakini huu si uchungu wao bali ni woga wa kukosa nafasi, woga wa kupitwa na upepo wa mabadiliko. Wanalia kwa sababu si wao tena wanaoshika hatamu wansona giza mbele yao na si kwa sababu ya uchungu wa kweli kwa wananchi.
3. Tulipodai Katiba Mpya walileta Ukatiba, leo wanajificha nyuma ya hoja za mabadiliko na eti kutetea haki za wananchi wanao kandamizwa
Tulipodai utawala bora, walitetea nguvu ya dola.Wakasema watatumia dola kubaki madarakani. Wakati damu zetu zikimwagika, wao walikuwa kimya, au walishabikia ukandamizaji. Leo wamevaa koti la Utetezi wa haki za binadamu lakini kimsingi wanajitetea wenyewe kuhusu matumbo yao na kutaka tuwasikilize kana kwamba walikuwa pamoja nasi ila historia haifutiki kwa maneno matamu ya kisiasa. Wanalia, lakini ni kilio cha kukosa fursa, si cha huruma.
4. Kilio cha kimaslahi, si kilio cha utu
Hawa mashujaa bandia walikataa hata kusimama kwa ajili ya haki za binadamu. Tulipodhulumiwa, walitoa kauli za kusuasua. Walipoona misaada ya wafadhili inahatarika, walilalama kwa woga wa kupoteza rasilimali, si kwa uchungu wa mateso yetu. Leo wanajifanya sauti ya haki, lakini ni sauti yenye usongo wa matamanio ya madaraka.
5. Kelele zao ni kero, si matumaini tuwe makini
Uchungu wao si wetu. Kilio chao si kilio cha wananchi.Tukiwanyamazisha si kwa sababu ya upendo bali kwa sababu kelele zao zinaudhi, si kuponya. Sisi tumeishi kwenye ukweli wa mateso, wao wameishi kwenye ukimya wa hila. Mashujaa wa kweli walikuwa kwenye uwanja wa vita; hawa wa leo walikuwa kwenye kivuli cha usalama wakisubiri nafasi ya kurudi mezani.
6. Tulipolinda rasilimali walituita wahaini leo wanakuja na nyimbo za utaifa
Tuliposimama kupigania maliasili zetu, walituona wasumbufu. Hawakuguswa na uharibifu wa mikataba mibovu wala mateso ya wachimbaji wadogo. Leo wanakuja na sera za kizalendo, wakijidai walikuwa nasi lakini historia ya ukimya wao ni sauti kubwa ya unafiki wao.
Huu si wakati wa kulia na kila anayelia. Huu ni wakati wa kutambua waliolia nasi wakati wa giza, waliopigana nasi bila kutafuta sifa, walioteseka nasi kwa ajili ya haki. Mashujaa wa kweli hawahitaji vichwa vya habari matendo yao yanabaki kwenye myoyo ya watu.
Mashujaa wa bandia walitukimbia tulipohitaji sauti zao na sasa hawapaswi kututumia kama ngazi ya kuingia madarakani.
Maoni ya Wakili Boniface Mwabukusi
Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS)


