Na Dominic Allen
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), Halima Mdee amewataka viongozi na watumishi wa Umma kutekeleza wajibu wao kwa ufasaha ili kuboresha utoaji wa huduma kwa jamii.
Katika taarifa iliyotolewa leo na ukurasa rasmi katika mtandao wa X, imesema kuwa wito huo wa Mdee umetolewa wakati wa ziara iliyofanywa na Kamati hiyo kukagua miradi mbalimbali ya afya na elimu inayotekelezwa Halmashauri ya Kyela, mkoani Mbeya, amesema
“Kila mmoja atekeleze wajibu wake kwa wakati na kwa ufasaha, viongozi hawatakuwa na haja ya kuja kukagua” amesema Mdee.
Ameongeza kuwa kutokana na ukubwa wa nchi haiwezekani kwa kiongozi mmoja kutembelea kila mahali kutoa huduma, hivyo majukumu hayo yamekabidhiwa kwa Watumishi wa Umma ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma stahiki.
Aidha, amewataka Watumishi wa Umma kutekeleza maelekezo yanayotolewa na Kamati ya Kudumu ya Bunge na kuhakikisha wanazitatua dosari zinazobainishwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa kutoa taarifa sahihi.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Dkt. Festo Dugange, amesema Ofisi yake imechukua maelekezo yote yaliyotolewa na Kamati na itayasimamia kikamilifu katika utekelezaji wake.
Pia, Dkt. Dugange amewataka Watumishi wa Umma kuhakikisha fedha zinazotolewa kwa ajili ya miradi ya maendeleo zinatumika ipasavyo ili miradi hiyo ikamilike kwa wakati na kuzingatia thamani ya fedha.
Mwandishi: Dominic Allen
Mhariri: Yohani Gwangway


