Na Amiri Kilagalila
Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Njombe imeziagiza kamati za siasa katika wilaya zote mkoani humo kuwachukulia hatua wanachama pamoja na viongozi wote wa chama hicho wanaoandika maneno yenye kukejeli na kutukana viongozi mitandaoni.
Akitoa taarifa ya kikao cha kawaida cha Kamati ya Siasa kilichofanyika jana mkoani humo, Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Mkoa wa Njombe, Josaya Luoga amesema kuwa kikao hicho kilichokuwa na lengo la kujadili mambo mbalimbali ya chama lakini pia kimetoa maelekezo hayo ili kudhibiti sintofahamu zinazotengenezwa na kuharibu kazi za chama.
“Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya Mkoa imetoa maelekezo kwa Kamati za Siasa za Wilaya na Kamati za Maadili kuhakikisha zinafanya kazi ya kuwaita watu wote wanaochapisha mitandaoni maneno yanayoashiria kutengeneza sintofahamu kwenye makundi sogozi na kuwachukulia hatua” amesema Luoga.
Luoga ameongeza kuwa katika kuhakikisha chama kinakuwa na utulivu, wanachama watakaobainika kukutwa na makosa ya kutoa maneno ya kejeli katika mitandao ya kijamii watachukuliwa hatua kali.
“Wale wote ambao wataonekana kweli wameandika na kuthibitika watachukuliwa hatua kali kuhakikisha chama kinakuwa tulivu kuelekea uchaguzi 2025 tuwapate viongozi ambao watakwenda kufanya kazi za wananchi kwa utulivu” ameeleza Luoga.
Aidha, Josaya Luoga ametoa wito kwa wanachama na viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kuchukua tahadhari na maandishi yanayochapishwa katika mitandao ya kijamii, ambapo amewasihi kuandika maneno yanayolenga umoja na mshikamano wa chama.
Mwandishi: Amiri Kilagalila
Mhariri: Dominic Allen


