Na Amiri Kilagalila
Wakati Kanisa Katoliki Tanzania likiadhimisha ya Jubilei ya Miaka ya 2025 ya Ukristo ulimwenguni, Hospitali ya St. Joseph Ikelu iliyopo Kata ya Utengule, Halmashauri ya Mji wa Makambako mkoani Njombe imeendelea kutoa huduma ya vipimo bure kwa wananchi wenye nia ya kujua afya zao ili waweze kuanza matibabu.
Akizungumza wakati zoezi la vipimo likiendelea, daktari wa hospitali hiyo, Dkt. Polikap Nyengela amesema kuwa vipimo vinavyotolewa ni pamoja na kipimo cha kisukari, macho, tezi dume, saratani ya matiti, shinikizo la damu pamoja na hali ya lishe.
Dkt. Nyengela ameongeza kuwa lengo la kutoa huduma hiyo bure ni kurejesha kwa jamii kile walichokipata ili kuwasaidia wananchi kutambua hali zao za kiafya.
“Tunarudisha kwa jamii kile ambacho tumefanikiwa kukipata, na zoezi hili tunalifanya kwa muda wa siku mbili, tarehe 01 – 02 Mei, 2025” amesema Dkt. Nyengela.

Aidha, Dkt. Nyengela amebainisha kuwa kwa sasa watu wengi wanakumbwa na magonjwa ya kisukari pamoja na shinikizo la damu, hali ambayo inapekekea kuathirika kwa mifumo ya mwili na kusababisha wengi wao kuishi na magonjwa kwa muda mrefu bila kujua kama wanaumwa kutokana na kutokuwa na desturi ya kupima afya zao mara kwa mara.

Hata hivyo Dkt. Nyengela ametoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kutumia dawa bila kupata vipimo sahihi vya wataalamu wa afya, kwa sababu wanaweza kupata madhara kutokana na kutumia dawa ambazo sio sahihi.
Mwandishi: Amiri Kilagalila
Mhariri: Dominic Allen


