Na Mwandishi wetu
Mnamo Juni 29, 2025 Dkt. Catherine Joachim ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Afya na Mazingira Umoja wa Wazazi Taifa, Jumuiya ya Chama cha Mapinduzi (CCM), alikabidhiwa fomu ya kuomba ridhaa ya kugombea nafasi ya Ubunge Viti Maalum Wazazi Tanzania Bara. Hatimaye baada ya kufanyika Kikao cha Kamati Kuu ya CCM chini ya Mwenyekiti wa Chama Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Kamati Kuu imemuamini Dkt. Catherine na kulirejesha jina lake kwa upande wa Tanzania Bara.
Dkt. Catherine Joachim ni nani?
Dkt. Catherine Joachim ni daktari wa binadamu, mbobezi katika uimarishaji wa huduma za afya na mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka 25 katika masuala ya uongozi nchini, kisera na utekelezaji ambao umekuwa na matokeo chanya kwa jamii.
Akitumia taaluma yake na uzoefu ipasavyo, Dkt. Catherine kwa nyakati tofauti tofauti amefanya kazi katika Sekta ya Umma na Binafsi, akichangia katika utekelezaji wa Sera ya Afya, lishe na uratibu kwa kisekta nchini.
Kada huyu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), amekuwa akijitoa kwa chama na jumuiya zake zote, wengi wanamuona kuwa ni tunu na mfano wa kuigwa, Jumuiya ya Wazazi inajivunia uwepo wake kutokana na utendaji kazi na kujitoa kwake.

Baada ya Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kuonesha imani kwake na kulirejesha jina lake kwa upande wa Tanzania Bara, Dkt. Catherine ameweka vipaumbele ambavyo atahakikisha anavitekeleza endapo atachaguliwa kuwa Mbunge wa Viti Maalum Wazazi Tanzania Bara;
Dkt. Catherine amesema kuwa endapo atapata ridhaa na kuchaguliwa katika nafasi hiyo ya Ubunge wa Viti Maalum Wazazi Tanzania Bara, kupitia sauti ya wazazi katika ngazi zote anachangia kwa vitendo utekelezaji na ufuatiliaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2025 – 2030.
Pia atahakikisha anashiriki ipasavyo katika kutekeleza na kufuatilia mikakati ya Jumuiya ya Wazazi, ili kuimarisha jamiii kuanzia ngazi ya familia, kwani ndiyo msingi wa Taifa, huku akiwaunganisha wazazi na fursa za kiuchumi , uwekezaji na ujasiriamali lengo likiwa ni kuwajengea uwezo wa kujitegemea.
Mbali ya hayo yote, kuchaguliwa kwa Dkt. Catherine kutatoa nafasi ya kumwezesha kuwakilisha sauti ya wazazi katika mabaraza na ngazi za maamuzi ya kitaifa.
Duru mbalimbali za kisasa nchini zinamtaja kama kiongozi mwenye maono, mpenda watu asiye na makundi, mpatanishi na si mchonganishi, mwenye uwezo wa kusimama na kutetea maslahi ya Jumuiya ya Wazazi na watu wake. Mpambanaji katika masuala ya elimu ,uchumi na maendeleo, mwenye uthubutu wa kufanya jambo kwa ajili ya wengine.
Wadadisi wa mambo wamebainisha kuwa Dkt. Catherine ana nafasi kubwa katika uchaguzi huu, akiwa na ushawishi na mwenye mvuto, hivyo kumpoteza ni kupoteza rasilimali muhimu katika Jumuiya ya Wazazi. Na wanakubaliana na hilo wamesema Dkt. Catherine Joachim anatosha na wanatamba nae.
Mhariri: Dominic Allen


