Na Dominic Allen
Ubalozi wa Poland nchini Tanzania kupitia ukurasa wao rasmi wa X, hapo jana Aprili 16, 2025 ulichapisha andiko kuwa siku kama hiyo mnamo mwaka 1922, Umoja wa Kisovieti (USSR) ulisaini mkataba uliyosaidia kuijenga kinguvu Jeshi la Ujerumani la Wanazi, hatimaye kuchangia kulipuka Vita vya Pili vya Dunia (1939 – 1945), na karne moja baadae Urusi inapuuzia kanuni za kimataifa, safari hii kupitia vita dhidi ya Ukraine.
Kufuatia chapisho hilo la Ubalozi wa Poland, Ubalozi wa Urusi nchini Tanzania hii leo kupitia ukurasa wao rasmi wa mtandao wa X umeijibu Poland, kuwa USSR ilisaini mkataba huo na serikali ya kidemokrasia ya Weimar Republic. Wanazi waliingia madarakani mwaka 1933.
“Ndio ujinga wa kutojua misingi ya historia. USSR ilisaini Mkataba huo na serikali ya kidemokrasia ya Weimar Republic. Wanazi waliingia madarakani mwaka 1933. Waziri wa Nje wa Ujerumani W.Rathenau aliyesainisha Mkataba huo aliuawa na magaidi wa mrengo wa kulia kuhusiana na kitendo hicho.” Umeandika Ubalozi wa Urusi nchini Tanzania.
Baada ya Ubalozi wa Urusi kuonesha kukerwa na chapisho hilo, Ubalozi wa Poland nchini umeitetea kauli yake, ukisema kuwa mkataba uliyosainiwa na Umoja wa Kisovieti (USSR) ndiyo uliyosaidia kuijenga na kulipa nguvu Jeshi la Ujerumani la Wanazi.
“Tafadhali hakikisha ukweli za kauli. Hatujaandika kuwa mkataba ulisainiwa na Ujerumani ya Nazi, bali kwamba Urusi ya Kisovieti ilisaini mkataba uliosaidia kuijengea na kuipa nguvu jeshi la Ujerumani ya Nazi na hatimaye kuchangia katika kuzua Vita vya Pili vya Dunia.” Umeandika Ubalozi wa Poland nchini Tanzania.
Ubalozi wa Urusi nchini Tanzania umekemea kitendo hicho cha Ubalozi wa Poland nchini kwa kuchapisha andiko hilo, ukisema kuwa ni upotoshaji wa historia.
“Basi miaka ya 1920 wote walikuwa na uhakika Wanazi wataongoza Ujerumani? Usipotoshe historia tafadhali” Umeandika Ubalozi wa Urusi nchini Tanzania.
Hata hivyo Ubalozi wa Urusi nchini umesema hawaangalii mjadala wa kihistoria kuhusu jeshi gani lililofaidika zaidi kutokana na ushirikiano wa kijeshi, kama ni Jeshi la Wajerumani au Wasovieti, huku wakisisitiza kuwa historia si uwanja wa uchokozi usiyokuwa na maana.
Mwandishi: Dominic Allen
Mhariri: Yohani Gwangway


