Na Dominic Allen
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gerald Mweli ametoa wito kwa Maafisa Ugani kutoa huduma pamoja na ushauri bora kwa wakulima nchini, ili kuleta matokeo chanya kwenye Sekta ya Kilimo.
Katibu Mkuu, Mweli amezungumza hayo hapo jana katika uzinduzi wa mafunzo ya Maafisa Ugani katika Chuo cha kilimo cha MATI Mlingano wilayani Muheza, Tanga.
Mafunzo hayo yamehusisha Maafisa Ugani kutoka Bagamoyo, Lushoto, Kigamboni pamoja na Ubungo, ambapo yamelenga kuwajengea uwezo wa kuwafikia wakulima zaidi ya milioni 13 kwa kutumia mbinu shirikishi ikiwemo mifumo ya kidijitali na mashamba darasa.
“Serikali imetoa vifaa muhimu kama pikipiki, vishikwambi na vifaa vya kupimia afya ya udongo kwa Maafisa Ugani ili kuongeza ufanisi katika huduma zinazotolewa.” Amesema Katibu Mkuu, Mweli.

Mweli ameongeza kuwa mafunzo hayo pia yamelenga kutengeneza Maafisa Ugani waliobobea katika mazao husika.
“Tunataka kutengeneza Maafisa Ugani waliobobea kwenye mazao husika, tunataka mtu akitoka hapa analijua zao hilo vyema kama mkulima.” Amezungumza Mweli.
Katibu Mkuu, Gerald Mweli pia alizindua na kukabidhi nyumba ya Afisa Ugani wa Kilimo katika kijiji cha Masaika, wilayani Pangani mkoani Tanga ambayo imegharimu kiasi cha Tsh. Milioni 41.5.
Mwandishi: Dominic Allen
Mhariri: Yohani Gwangway


